Dar es Salaam. Mamia ya wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) wameripotiwa kuuawa katika operesheni za siri Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kuuawa kwa wanajeshi hao katika operesheni hiyo kunapingana na msimamo wa Serikali ya Rwanda inayodai askari wake hawahusiki wala kushiriki katika mzozo unaoendelea kati ya M23 na DRC.
Vyanzo mbalimbali vya kijasusi, kijeshi na kidiplomasia vinasema idadi ya wanajeshi wa RDF waliouawa ni kubwa, huku wakidai walikuwa wakisaidia mashambulizi yanayofanywa na waasi wa M23 ndani ya DRC.
Picha za setilaiti zilizopigwa katika makaburi ya kijeshi yaliyoko Kigali, nchini Rwanda, zinaonyesha makaburi mapya yasiyopungua 600 yaliyopatikana tangu waasi wa M23, wanaodaiwa kuungwa mkono na RDF, walipoanza operesheni zao ndani ya DRC miaka mitatu iliyopita.
Maofisa wawili wa juu wa kijasusi wenye taarifa za kina kuhusu RDF wamesema idadi halisi ya vifo vya wanajeshi wa Rwanda huenda ikafikia maelfu, ingawa ni vigumu kuthibitisha idadi kamili kutokana na hali ya usiri inayozunguka operesheni hizo.
Taarifa hizo zinaibua maswali mapya kuhusu ushiriki wa Rwanda katika mapigano yanayoendelea DRC, kwa kuwa imekuwa ikikanusha mara kadhaa kuhusika.
Wakati huo, Serikali ya Kinshasa imeendelea kuishutumu Rwanda kwa kuunga mkono makundi ya waasi, hasa M23, jambo linaloongeza mvutano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo jirani.
Mashirika ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, yanakabiliwa na shinikizo la kuchukua hatua na kuchunguza kwa kina madai hayo, hasa kwa kuzingatia athari za kibinadamu na kiusalama zinazoweza kujitokeza katika ukanda huo wa Maziwa Makuu.
Moja ya vyanzo vya uhakika kimeeleza idadi ya wanajeshi wa Rwanda waliouawa katika mashambulizi Mashariki mwa DRC ni kubwa kiasi kwamba miili mingine ilizikwa kwa siri kwenye makaburi ya pamoja.
Imeelezwa familia za wanajeshi waliouawa zilipewa majeneza matupu baada ya miili ya wapendwa wao kushindwa kurejeshwa nyumbani.
“Siyo askari wote waliopoteza maisha DRC walirejeshwa nyumbani, hasa wale waliokufa katika maeneo yenye mapigano makali. Baadhi yao walizikwa kwenye makaburi ya pamoja DRC,” kimeeleza chanzo hicho.
Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa majeruhi na vifo vya wanajeshi wa Rwanda ni vingi kiasi kwamba jengo jipya limejengwa katika Hospitali ya Kijeshi ya Kigali ili kukabiliana na wingi wa majeruhi.
Aidha, chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo kimeripotiwa kujaa kupita kiasi.
Hali hiyo inazidi kufichua uhalisia wa kiwango cha ushiriki wa Rwanda katika mapigano hayo, kinyume na madai ya Serikali ya Kigali kwamba hawana wanajeshi kwenye eneo hilo la mgogoro.
Mvutano huo unaweza kuongeza shinikizo kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zaidi kuchunguza na kushughulikia hali ya usalama katika eneo la Maziwa Makuu.
Rwanda imeendelea kukanusha madai kuwa majeshi yake yamevuka mpaka na kuingia DRC. Serikali ya Kigali imekanusha mara kwa mara kuhusika na kuunga mkono waasi wa M23 na haijawahi kukiri kuwa wanajeshi wake wamepoteza maisha katika mzozo huo.
Hata hivyo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema jeshi la Rwanda lipo kwenye udhibiti wa moja kwa moja wa waasi wa M23, ambao mwezi uliopita waliteka jiji la Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, na sasa wanadhibiti eneo kubwa la DRC linalokadiriwa kuwa karibu nusu ya ukubwa wa Rwanda yenyewe.
Emmanuel Ngabo, anayeongoza kikundi cha Muungano wa Wanyarwanda Wanaotaka Mabadiliko (ARC), amesema amepokea taarifa nyingi kutoka kwa wazazi waliopoteza wapendwa wao, zikionyesha idadi kubwa ya Warwanda wameuawa.
“Kuna miili mingi inayohitaji kushughulikiwa. Kuna familia nyingi zinazongoja maziko kiasi kwamba wanaruhusiwa kukaa makaburini kwa dakika 30 pekee,” amesema Ngabo (si jina halisi) ameongeza; “majeneza huwa yamefungwa muda wote, ama kwa sababu mwili wa askari umeharibika vibaya kiasi cha kutotambulika, au kwa sababu hakuna mwili ndani ya jeneza.”
Matukio hayo yanazidi kuzua wasiwasi kuhusu mustakabali wa usalama katika eneo la Maziwa Makuu, huku jumuiya ya kimataifa ikitarajiwa kushinikiza pande zinazohusika kutafuta suluhisho la kudumu la mzozo huo.
Picha za setilaiti zilizopigwa Agosti 2021 kabla ya kuanza kwa mgogoro wa M23 na nyingine ya Desemba 15, 2024 kabla ya waasi kuteka Goma Januari 27 mwaka huu, zinaonyesha ongezeko la makaburi katika makaburi ya kijeshi ya Kanombe.
Maeneo mawili maalumu yanaonyesha ongezeko la makaburi tangu mzozo huo uanze. Kaskazini mwa makaburi hayo, kuna makadirio ya makaburi mapya 100, hali iliyosababisha idadi ya makaburi katika eneo hilo kuongezeka mara mbili.
Kusini mwa makaburi hayo, makaburi mapya 500 yanaonekana wazi. Idadi kubwa zaidi ya makaburi inakadiriwa kuchimbwa baada ya picha hiyo kuchukuliwa mwishoni mwa mwaka jana, ingawa mawingu yalizuia upatikanaji wa picha mpya ya eneo hilo.
Mwezi uliopita kulishuhudiwa umwagaji damu zaidi katika mzozo huo, ambapo waasi wa M23 wakishirikiana na RDF waliteka miji ya Minova na Sake, pamoja na Goma.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa mapigano ya kuwania Goma yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 2,900.
Chanzo cha kijasusi kimeeleza kumekuwa na ongezeko la taarifa za vifo vya wanajeshi wa RDF. “Tumekuwa tukipokea ripoti nyingi kuhusu majeruhi katika hospitali za kijeshi na maeneo ya maziko,” kilisema.
Chanzo cha kijeshi kimeongeza kuwa uwezo wa jeshi la DRC, pamoja na matumizi madhubuti ya ndege zisizo na rubani na nguvu ya anga, kumesababisha vifo vingi.
Ingawa maelfu ya wanajeshi wa Rwanda wamepelekwa pia Msumbiji na Jamhuri ya Afrika ya Kati, vyanzo vinasema vifo vya RDF katika maeneo hayo ni vichache.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa walikadiria kuwa hadi Desemba wanajeshi 4,000 wa Rwanda walikuwa ardhini DRC, lakini vyanzo vya kijasusi vinaamini idadi hiyo ni kubwa zaidi, pengine zaidi ya 7,000.
Familia za Rwanda zilizohojiwa kuhusu mzozo huo hazikutaka kuzungumzia kupoteza watoto wao. Hata hivyo, Mnyarwanda aliye uhamishoni barani Ulaya alisema amezungumza na familia mbili wiki iliyopita ambazo zimepoteza watoto wao vitani.
“Maziko yanapangwa haraka sana na jeshi. Marafiki wa familia hawapati nafasi ya kuwaaga marehemu, kama ilivyo kawaida katika utamaduni wetu,” alisema.
Ngabo, ambaye yuko uhamishoni Ufaransa, alisema, “Nimechapisha matangazo mengi ya maziko ya wanajeshi wa Rwanda waliouawa Congo.”
Ingawa Rwanda imekuwa ikinyamaza kuhusu vifo vya wanajeshi wake upande wa magharibi ya mpaka, Rais Paul Kagame alivitaja vifo hivyo katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka, akiziahidi familia kuwa madhabahu yao hayatakuwa bure.
Chanzo cha kidiplomasia kimesema kauli hiyo ya Kagame inaashiria kuwa kiwango cha vifo kimekuwa tatizo.
Hata hivyo, Serikali ya Rwanda imetumiwa anwani ya maswali kuhusu taarifa hizo, lakini haijatoa majibu.