MOTO wa straika wa Al Nassr ya Saudi Arabia, Clara Luvanga haupoi na safari hii anawania tuzo ya mchezaji bora wa mwezi mbele ya Waarabu.
Tuzo hizo zinatolewa kila mwezi zikiangazia wachezaji watatu wanaofanya vizuri kisha kupigiwa kura na kumjua mshindi wa tuzo hiyo.
Clara ni Mtanzania pekee anayeingia katika tuzo hizo dhidi ya Mmoroco, Iptissam Jraidi wa Al Ahli na MCameroon, Ajara Njoya anayekipiga Al Qadsiah.
Clara aliingia kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kucheza mechi nne, dakika 360 na kufunga mabao nane na asisti mbili chama lake likishinda mechi zote.
Njoya kwenye mechi nne, amecheza dakika 360 akifunga mabao nane na asisti moja chama lake likishinda mechi mbili, sare moja na kufungwa moja huku Iptissam akifunga mabao tisa kwenye dakika hizo huku Al Ahli ikishinda mechi tatu na kupoteza moja.
Msimu huu ni mara ya pili nyota huyo kuwania tuzo hizo na awali ilikuwa ya goli bora la wiki na alishindwa kupenya mbele ya Waarabu.
Hadi sasa ndiye mshambuliaji kinara wa mabao akiwa nayo 12 kwenye mechi 13 ilizocheza timu hiyo.