Dar es Salaam. Mwili wa Mtukufu Aga Khan IV umezikwa leo, Februari 9, 2025, katika mazishi ya faragha yaliyofanyika katika mji wa Aswan, nchini Misri.
Mwanamfalme Rahim, ambaye ndiye Aga Khan V na Imam wa 50 wa Ismailia, pamoja na wanafamilia wengine, wakiwemo viongozi wa jumuiya ya Ismailia duniani, wameshiriki mazishi hayo.
Gavana wa Aswan, Meja Jenerali Dk Ismail Kamal, ameshiriki shughuli zote za mazishi katika mji huo kama heshima kwa Mtukufu Aga Khan IV.
Jeneza lililobeba mwili wa Mtukufu Aga Khan IV limesafirishwa kwa boti kwenda kwenye kaburi la babu yake, Aga Khan III, lililopo katika eneo binafsi.
Mwili wa Mtukufu Aga Khan IV umezikwa kwa muda katika kaburi la babu yake hadi kaburi jipya litakapojengwa kama mahali pake pa kupumzika kwenye ardhi iliyo karibu.
Hafla ya mazishi imefanyika kwa taratibu zote za Kiislamu, na baada ya kumalizika, viongozi walipata nafasi ya kutoa salamu za pole kwa familia.
Baada ya mazishi, Gavana wa Aswan, Meja Jenerali Dk Ismail Kamal, alimkabidhi Mwanamfalme Rahim Aga Khan V mfano wa ufunguo wa Jiji la Aswan kama ishara ya heshima kwake na kumkaribisha rasmi.
Misri ilikuwa kituo cha Fatimid Caliphate kilichoongozwa na Imam wa Ismailia kuanzia karne ya 10 hadi 11. Fatimid Imam-Caliphs walilifanya jiji la Cairo kuwa kituo kikubwa cha kujifunza, utamaduni na biashara.
Kuunga mkono masuala kama elimu na sanaa kuliwasaidia kuendeleza sayansi, uchoraji, na falsafa. Alama zao bado zinaonekana leo kutokana na utajiri wa kihistoria na utamaduni katika eneo hilo.

Mji wa Aswan ni eneo alilozikwa Sultan Mahomed Shah Aga Khan III na mkewe Mata Salamat.
Wote wawili, wakati wa uhai wao, walikuwa na uhusiano mzuri na wakazi wa Aswan, uhusiano ambao uliendelezwa na marehemu Mwanamfalme Karim na familia yake kupitia kazi za taasisi za Om Habibeh Foundation na Aga Khan Foundation.
Mtukufu Aga Khan (88) alifariki dunia Jumanne, Februari 4, 2025, jijini Lisbon, Ureno, akiwa amezungukwa na familia yake.
Baada ya kifo cha Mtukufu Aga Khan IV, mwanaye Rahim Al-Hussaini alitangazwa Jumatano, Februari 5, 2025, kurithi mikoba na kuwa Imam wa 50 wa madhehebu hayo, kwa mujibu wa wasia wa baba yake.
Enzi za uhai wake, Mtukufu Aga Khan IV alifahamika kutokana na mchango wake katika shughuli zinazochangia kuimarisha ustawi wa maisha ya binadamu katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.
Kiongozi huyo, aliyezaliwa Desemba 13, 1936, Geneva, Switzerland, katika familia ya Aly Khan na Joan Yarde-Buller, ni mzaliwa wa Uingereza. Aliishi maisha yake ya utoto jijini Nairobi, Kenya.
Kutokana na kuishi katika ukanda wa Afrika Mashariki, mchango wake ulionekana kwa kuanzisha taasisi za Aga Khan zilizoletea tija na manufaa mbalimbali kwa umma katika ukanda huo.

Kutokana na shughuli za kielimu, Aga Khan alijikuta nchini Switzerland, ambako alipata elimu ya dini katika Shule ya Le Rosey, kisha akaenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.
Wakati baba yake anafariki dunia, yeye alikuwa masomoni akibobea katika Imani ya Kiislamu katika chuo hicho.
Huku akiwa mrithi wa 49 wa nafasi ya Imam wa madhehebu ya Ismailia, Aga Khan IV alikatisha ndoto yake ya kuwa mchezaji wa soka na kuendelea na elimu katika ngazi ya Uzamivu (PhD) chuoni Harvard.
Alilazimika kukatisha ndoto hizo baada ya kuteuliwa kurithi mikoba ya uongozi wa kiroho wa mamilioni ya waumini wa madhehebu hayo, ambayo yalikuwa yamesambaa maeneo mengi ulimwenguni, hususan India, Kenya, Pakistan, Bangladesh, Misri, Canada na Jumuiya ya Kisovieti (Urusi).
Akiwa kiongozi wa kiroho, alitwishwa jukumu la kuwa Imam wa 49 wa madhehebu ya Shia Ismailia, wadhifa ambao aliutumikia kwa dhati.
Hata hivyo, wajibu wake haukuishia kuwa kiongozi wa kidini pekee, bali alikuwa mwanzilishi wa shughuli mbalimbali zilizoleta mabadiliko ulimwenguni, hususan kwenye sekta ya afya, utamaduni, elimu, habari na maendeleo ya jamii katika kanda zote duniani.
Maeneo mengine aliyoyagusa moja kwa moja ni pamoja na sekta ya uwezeshaji kiuchumi, ambapo alibua mikakati ya kuongeza ustawi katika jamii.
Mtukufu Aga Khan ameacha nembo isiyofutika maeneo mbalimbali duniani, hususan nchini Kenya na Tanzania, ambako alianzisha taasisi mbalimbali zilizoletea mchango mkubwa katika maisha ya raia wa nchi hizo.
Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Shule za Aga Khan, Chuo Kikuu cha Aga Khan, vyote vilianzishwa ikiwa ni ishara ya kujitoa kwake kuikomboa jamii ya eneo husika.
Pia, alianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Aga Khan (AKFED), mfuko huo ulichochea maendeleo endelevu huku ukitumia kauli yake: “AKFED hailengi kutengeneza faida, bali ni mpango wa maendeleo ya kesho.”
Pia, ni mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) ambao umeleta tija maeneo mbalimbali hususan katika sekta ya afya, elimu na utamaduni, hususan uwezeshaji kiuchumi maeneo ya vijijini nchini Tanzania na Kenya.
Uwepo wa Aga Khan nchini Tanzania unaonekana kupitia uanzishwaji wa kampuni mbalimbali, ikiwemo Mwananchi Communications Limited (MCL), Hospitali za Aga Khan, na miradi mbalimbali katika sekta ya afya na elimu.