Moshi. Mwanasiasa mkongwe nchini, Nicodemus Banduka(80) amefariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mloganzila iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Banduka ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikalini, amefariki dunia Ijumaa Februari 7, 2025.
Akizungumza na Mwananchi digital leo Jumapili Februari 9, 2025, mmoja wa ndugu wa familia hiyo, Salehe Mkwizu amesema; “Mzee wetu ni kweli amefariki na alikuwa anatibiwa Dar es Salaam katika Hospitali ya Mloganzila.”
Hata hivyo, amesema taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko zitatolewa na familia baada ya kukamilika kwa taratibu mbalimbali za mazishi.
Akizungumzia kifo cha mwanasiasa huyo, Mbunge wa Mwanga (CCM), Joseph Tadayo amesema Banduka alikuwa mmoja wa wanasiasa wakongwe kutoka Wilaya ya Mwanga na atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa serikalini na kwenye chama.
“Ni kweli mzee Banduka amefariki usiku wa kuamkia jana Jumamosi, Msiba kwa sasa upo Kibaha, lakini kijijini kwake ni Mruma kata ya Msangeni Wilaya ya Mwanga, alikuwa mwanasiasa mkongwe na mbobevu,”amesema Tadayo.
Mbunge huyo amesema Banduka atakumbukwa kama kada mbobezi na mtiifu wa CCM aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kuzielewa na kuzinadi sera za chama chake.
“Aliaminika sana na Baba wa Taifa kama Kada wa CCM na alikuwa na kipawa kikubwa cha kuhimiza maendeleo na amekuwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali na mwaka 2005, alijitokeza kuomba uteuzi kwa nafasi ya ubunge wa Jimbo la Mwanga, lakini kura hazikutosha,” amesema Tadayo.
Mzee Banduka enzi za ujana wake anatajwa kuipenda siasa na kujishughulisha na mambo ya siasa tangu akiwa shule n ahata alipoendelea na masomo yake ya chuo kikuu.
Banduka ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Mruma, Ugweno, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM ikiwamo ya Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa Mkoa wa Kilimanjaro, Mjumbe wa kamati kuu Taifa, Katibu wa CCM Mkoa na baadaye kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa huku akihudumu kwa nafasi hiyo katika mikoa mbalimbali hadi alipostaafu.