Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa Rais wa Namibia na wananchi wote kufuatia kifo cha Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Sam Nujoma.
Kupitia taarifa yake katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, Rais Samia ameandika: “Nimesikitishwa sana na kifo cha Rais, muasisi wa Taifa la Namibia, Dk Sam Nujoma.
“Mpigania uhuru, mwanamajumui na rafiki mpendwa wa Tanzania, ambako wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Namibia, Dk Nujoma aliishi maisha ya utumishi ambayo yalitengeneza siyo tu hatima ya nchi yake, bali pia yaliwahamasisha vizazi kusimama kwa ajili ya maadili ya uhuru, usawa na haki.”
Ameongeza kuwa: “Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kuwasilisha salamu zetu za rambirambi kwa Dk Nangolo Mbumba, Rais wa Jamhuri ya Namibia, wananchi wa Namibia, mke wa Rais Mwanzilishi wa Jamhuri ya Namibia, mheshimiwa Kovambo Nujoma, watoto wa Dk Nujoma, familia yake yote, marafiki na wanachama wa SWAPO.”