Samatta atupia mawili Paok ikishinda tano

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars, Mbwana Samatta jana aliisaidia timu yake ya Paok kupata pointi tatu muhimu baada ya kuifungia mabao mawili kwenye mchezo wa Ligi Kuu nchini Ugiriki dhidi ya OFI Crete.

Katika mchezo huo Paok ndiyo walikuwa wageni wa OFI Crete kwenye Dimba la Thódoros Vardinoyánnis ambapo staa wa Tanzania, Mbwana Samatta aliweka historia ya kufunga mabao mawili.

Samatta alikuwa wa kwanza kufumania nyavu za OFI Crete katika dakika ya pili ya mchezo akimalizia kwa kichwa mpira uliotemwa na kipa, Nikolaos Christogeorgos baada ya kupigiwa shuti kali na Giannis Michailidis ambaye alifunga bao la nne.
Dakika ya 67, Samatta alifunga bao la tano kwa Paok huku likiwa la pili kwake baada ya kumalizia kwa kichwa krosi iliopigwa na Dimitris Pelkas ambaye alifunga bao la pili dakika ya nane huku bao lingine likifungwa na nahodha, Stefan Schwab kwa mkwaju wa penalti baada ya mchezaji wa OFI Crete kushika mpira ndani ya eneo la hatari.
Samatta ambaye mwanzoni mwa msimu aliwekwa nje ya kikosi na kutokana na kile kilichodaiwa kuwa hayupo kwenye malengo ya timu hiyo mpaka sasa amecheza mechi sita za Ligi Kuu akiwa amefunga mabao mawili.

Baada ya ushindi wa jana, Paok imesogea mpaka nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Ugiriki maarufu kama ‘Super League’ ikifikisha jumla ya pointi 40 ikiwa nyuma kwa pointi saba dhidi ya vinara wa ligi hiyo Olympiacos yenye pointi 47.

Paok ambao ndiyo Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu wamecheza michezo 22 ambapo wameshinda mechi 12, wamepata sare mechi nne na kupoteza mechi sita wakiwa wamefunga mabao 40 na kuruhusu mabao 22.

Related Posts