SERIKALI YASHAURIWA KUSIMAMIA WAKANDARASI UJENZI UWANJA WA NDEGE MSALATO, BARABARA ZA MZUNGUKO

Na Janeth Raphae,Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeshauri Serikali kusimamia vema Mkandarasi anayejenga uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma ili akamilishe ujenzi wa uwanja huo kwa wakati kulingana na muda mkataba.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo walipotembelea uwanja huo pamoja na ujenzi wa barabara za mzunguko, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Selemani Kakoso amesema ni vema mkandarasi akaharakisha ujenzi wa uwanja huo ili kwenda na mkataba wa ujenzi.

Amefafanua kumekuwa na tabia kwa baadhi ya Wakandarasi kuomba kuongezewa muda wa ziada wanapopewa kazi bila kujua muda utakapoongezwa na gharama nazo zinaongezeka.Hivyo wao kama Kamati wanashauri Serikali kwanza ni kumsimamia mkandarasi akamilishe ujenzi kwa wakati.

“Kumekuwa na tabia ya Wakandarasi wetu wanapopewa kazi wanaongeza muda wa ziada ambao hautakiwi uingezwa mara kwa mara, Hivyo tunaomba eneo hili Serikali isimamie kwani anapoongezewa muda na gharama zinazidi zaidi za ule mkataba uliokuwa umesainiwa”.

Pia Kakoso amesema kuwa Kamati hiyo imeridhishwa na mwenendo wa ujenzi unavyokwenda na kuipongeza Serikali kwa kutoa fedha kwa asilimia kubwa ambazo zinafanyakazi zinazoonekana.

“Kamati ya Bunge imeridhishwa na mwenendo wa ujenzi unavyokwendwa,lakini tunaipongeza Serikali kwa kutoa fedha kwa asilimia kubwa sana ambayo inaonesha fedha zinazotolewa zinafanyakazi maana inaonekana kabisa kuwa uwanja huu utakuwa mzuru na wa kisasa utakapo kamilika”.

Kakoso amesisitiza katika maeneo ya uwanja huo kuwe na uwekezaji kwenye maeneo ambayo yatasaidia usafirishaji wa mazao ambayo yatahitajika huko Duniani.

“Tuendelee kusisitiza kwenye maeneo ya uwanja ndege huu kuwe na uwekezaji kwenye maeneo ambayo yatasaidia usafirshaji wa mazao ambayo yanahitajika huko duniani, kama vile mboga mboga ambazo zitasaidia Watanzania kuwa na usafirishaji na uingizaji wa fedha kuwaongeza kiuchumi”.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe Godfrey Kasekenya amesema Wizara pamoja na Taasisi ya Wakala wa ujenzi wa Barabara (TANROADS)watayafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo.

Pia amesema kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Serikali watahakikisha uwanja huo unakamilika kwa wakati na kujengwa kama ulivyosanifiwa ili uwe bora na wa kisasa kuliko viwanja vyote Tanzania kutokana na Teknolojia inayotumika katika ujenzi huo.

“Sisi Wizara pamoja na wenzetu wa Tanloads maelekezo yote mliyoyatoa tutayafanyia kazi na kwaniaba Waziri wa Ujenzi na Serikali niahidi kwamba tuhahakisha uwanja huu unakamilikwa kwa wakati,tunamsimamia mkandarasi muda wote na kuhakikisha anajenga uwanja kama ulivyosanifiwa”.

“Mwenyekiti uwanja wa Msalato utakapokamilika utakuwa bora na wa kisasa kuliko viwanja vyote Tanzania kwasababu tunatumia teknolojia ya kisasa na utakuwa na uwezo wa kupokea ndege ya aina yeyote kutoka sehemu yeyote ambayo itapokelewa Dodoma ambayo ndio makao makuu ya nchi yetu.”

Awali akitoa maelezo kuhusu baadhi ya meneo katika uwanja huo ikiwemo maingilio ya ndege yani lami,sehemu za kupaki ndege na sehemu ya kupumzika abiria wanaotoka na kuingia uwanjani Mohamed Besta ambaye ni Mtendaji Mkuu TANROADS amesema jengo la abiria linalojengwa ni la ghorofa tatu na lina uwezo wa kuchukua watu 1100 kwa wakati mmoja.

Ameongeza eneo la maegesho ya ndege lenye upana wa mita 150 hadi 260 lina uwezo kupaki ndege 13 hadi 17 kutokana na ukubwa wa ndege na eneo la kurukia ndege lina upana wa mita 60 na urefu wa mita 3600 ambayo ipo kwenye hatua za juu kabisa kwa asilimia 90 ya utekelezaji wa ujenzi huo.

Kamati hiyo pamoja na mambo mengine imefanya ziara ya kuangalia maendeleo ya miradi ya mikubwa na ya kimkakati inayotekelezwa jijini Dodoma.








Related Posts