Siri mizizi ya rushwa kwenye chaguzi hii hapa

Dar es Salaam. Kuimarishwa mifumo ya uteuzi wa wagombea ndani ya vyama, kufutwa mtazamo wa mavuno nyakati za uchaguzi na umakini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), yametajwa kuwa mambo muhimu yanayopaswa kufanywa ili kukabili vitendo vya rushwa katika uchaguzi.

Kwa mujibu wa wadau wa siasa, vitendo vya rushwa nyakati za uchaguzi vinachochewa na mianya iliyopo inayosababishwa na kukosekana kwa umakini wa kuvidhibiti vitendo hivyo.

Wapo wanaodai mfumo wenyewe wa uchaguzi umewekwa katika mazingira yanayochochea rushwa, ndio maana hata wananchi wanajiweka tayari kuvuna fedha unapofika wakati wa uchaguzi.

Wadau hao wamedai kuwa, kuna haja kwa vyama vya siasa kuwa na kamati za wasomi wachache kwa ajili ya kupima na kuteua wagombea, badala ya kutumia wajumbe ambao aghalabu hawana uwezo wa kutambua haiba ya kiongozi.

Mitazamo ya wadau hao inakuja kipindi ambacho, vitendo vya rushwa vimekuwa vikitajwa kufanyika kwenye chaguzi za ndani ya vyama vya siasa na hata chaguzi za kitaifa.

Pia, hoja za wadau hao zinapigia msumari kilichowahi kuelezwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba kuwa, vitendo vya rushwa vinafanyika sio katika uchaguzi mkuu pekee, hata chaguzi za ndani ya vyama, jambo alilodai ni hatari kwa Taifa.

Mathalani, katika uchaguzi wa ndani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kulikuwa na hali ya kutuhumiana rushwa miongoni mwa makada na wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho.

Sio Chadema pekee, malalamiko kama hayo yameshuhudiwa katika vyama vingi vya siasa, lakini haikuwahi kutokea mtuhumiwa yeyote kuchukuliwa hatua.

Akizungumzia mzizi wa rushwa, Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema tatizo linaanzia kwenye mifumo ya uchaguzi iliyowekwa katika mazingira ya rushwa.

Kutokana na uhalisia huo, Olengurumwa amesema Watanzania wamegeuza michakato ya uchaguzi kuwa nyakati za mavuno na kuneemeka.

“Mwananchi kipindi hiki anajiandaa kuvuna fedha, katika kipindi hiki wanajiandaa kutumia fedha nyingi kupata mamlaka hiyo, imekuwa picha kuanzia ndani ya vyama vya siasa, kuja kwenye kuteua majina ya wagombea ili kwenda kushindana,” amesema.

Katika kutafuta namna ya kudhibiti hali hiyo, amesema mwaka jana kulikuwa na pendekezo la kuandaliwa mfumo wa kuwa na watu wengi wanaohusisha kupitisha wagombea ndani ya vyama ili kuepusha wasinunulike na  chama tawala kimefanyia kazi mwaka huu.

“Wajumbe wanaopiga kura kwenye wilaya,  lazima waongezwe wawe wengi badala ya kukaa na wawakilishi 600 kwenye chama, ilikuwa inasababisha mtu anaandaa fedha kuwanunua wajumbe wote,” amesema.

Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema: “Mwaka 2020 CCM uongozi wake ulianzisha vuguvugu la kukataa rushwa ndani ya chama na walitoa vitisho vingi na kufanya waliotaka kugombea wakati ule, waone watachaguliwa kwa uwezo na si una nini mfukoni.”

Dhana ya mwaka wa uchaguzi kuonekana wa neema kwa wananchi, imerudiwa na Dk Mbunda katika hoja yake kuhusu mizizi ya rushwa.

Amesema hilo limekuwepo tangu mwaka 1995 ulipoanzishwa mfumo wa siasa za vyama vingi.

“Nimeshafanya tafiti zao katika chaguzi kadhaa nikiwa kama mtazamaji na kuna wanaojifanyia tathimini binafsi kwamba katika uchaguzi huu nimekula fedha kiasi fulani na nilipewa na mtu fulani na wamekuwa wakifanya ujasiriamali,” amesema.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere (MNF), Joseph Butiku amesema tatizo la rushwa, vijana wanapaswa kujiuliza kwa sababu wanatoa na kupokea.

“Wengine ikiwamo mimi nimetoka serikalini muda mrefu, hili ni tatizo hasa kwa vijana, wanapokea na kutoa rushwa, wanapaswa kuzungumza wafanye nini kwa sababu ni tatizo lao,” amesema Butiku.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga amesema ugumu wa kudhibiti rushwa unasababishwa na mzizi wake kuanzia kwa wanasiasa.

“Tumeona chaguzi za ndani ya vyama zenyewe zimekuwa na rushwa, kwa hiyo tutegemee rushwa kuendelea hata kwenye uchaguzi mkuu. Takukuru wana nafasi kubwa ya kuzuia rushwa kama wataamua kufanya kweli kazi yao bila kuegemea upande wowote,”amesema Henga.

Diwani wa Wazo (CCM), Leonard Manyama amesema rushwa kwenye michakato ya chaguzi ni jambo lililo wazi na hasa hushamiri kwenye kura za maoni.

“Uchaguzi katika uzoefu wangu, rushwa si kubwa sana, ila kupata wagombea ndani ya vyama. Nje wagombea wanashindwa kutoa rushwa kwa wananchi kwa sababu ni wengi,” amesema Manyama.

Amesema wagombea wanatoa fedha nyingi kwa wajumbe na wanaopewa fedha hawamchagui mtu kwa kuangalia uwezo wake,  bali kiwango alichotoa ndicho kinachoamua.

 “Tatizo hili ni kubwa ndiyo sababu wabunge na madiwani wakichaguliwa wanakimbia maeneo yao kwa muda kwa sababu wanakuwa wameingia kwa kutumia fedha, hawa wajumbe wanaopiga kura hawana kazi maalumu wote ni watu wa vijiweni,” amedai Manyama. 

Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Crispin Chalamila ambaye amesema anafahamu vitendo vya rushwa mara nyingi huibuka zaidi nyakati za uchaguzi.

Chalamila amewataka wananchi kutoa taarifa Takukuru pindi wakivibaini vitendo hivyo ili kuvikomesha.

“Kwa desturi, vitendo vya rushwa mara nyingi vinaibuka kipindi cha uchaguzi, tunaomba wananchi watupe taarifa tuweze kudhibiti ili waweze kupata viongozi bora.

“Tanzania inaongozwa kidiplomasia, tutumie nafasi hii kupata viongozi bora wasiojihusisha na vitendo vya rushwa, lakini na wananchi wasiombe rushwa kwa wagombea na wagombea nao wasitoe rushwa,”amesema Chalamila.

Amesema wamejipanga kuzuia  rushwa kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara yake huku akieleza wanatarajiwa kukutana na wanasiasa na kujadili suala hilo.

“Tutaenda hadi bungeni kutoa semina, kwa kuwa tunajua wataenda majimboni kugombea, tunajua utu wa binadamu hauwezi kupimwa kwa dhamani ya fedha,” amesema Chalamila.

Katika maelezo yake,  Olengurumwa amesema lazima jamii iondokane na dhana ya kipindi hicho kugeuzwa cha mavuno.

Amesema badala yake wanapaswa kuchukulia uchaguzi ni jambo la msingi katika mustakabali wa maisha yao.

“Vyombo vinavyohusika na kukabiliana na rushwa vinatakiwa kuwa na macho zaidi kwenye nyakati za uchaguzi, kwa sababu kuna rushwa zinazoonekana wazi wazi lakini kuna wakati fulani watu wanatajwa, mwisho wa siku hatusikii watu wakichukuliwa hatua,”amesema Olengurumwa.

Manyama amesema ili kuliokoa taifa ni lazima kuanzishwe mifumo ya watu wasomi wachache wanampima mgombea kwa uwezo, itakuwa jambo nzuri kwakuwa watakuwa na uchungu tofauti na ilivyo sasa.

“Taifa la China linapiga hatua kwa sababu ya mifumo yao, mtu anachaguliwa kwa uwezo, mtu akitumia fedha unadhani akienda huo ataenda kupigania masilahi yake binafsi au ya umma ni lazima tubadilike,”amesema Manyama.

Amesema mamlaka zinazohusika lazima ziwe makini lakini changamoto iliyopo vyombo husika havionyeshi umuhimu wake kwa kuwa rushwa ziko wazi na zinajulikana.

“Siku hizi kuna teknolojia kuna wanaotumia simu, kalamu lakini hakuna umakini katika kufuatilia jambo hili na viongozi wengi wanaloongea ni tofauti na lililoko moyoni mwao,” amesema Manyama.

Februari 4, mwaka huu Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira aliwatahadharisha wanachama wa chama hicho kuchagua watu wanaokubalika, lakini wasiwe wapenda rushwa.

Kilichoelezwa na Wasira si kauli ya kwanza, iliwahi kusemwa na mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu, Dk Emmanuel Nchimbi katika nyakati tofauti wakikemea rushwa.

Hata hivyo, Wasira alisema mikusanyiko na mikutano inayoendelea ya chama hicho, siyo kuanza kwa kampeni bali wanafanya alichokiita ku-test mitambo.

Alisema kwa kuwa yeye ni mwenyekiti wa kamati ndogo ya maadili kwa muundo wa Katiba ya CCM, hivyo watu wanaokiuka maadili watakutana naye.

“Tunataka watu wachaguliwe ambao wanakubalika, na ninyi mkaangalie hilo siyo kuchagua watu wanaodhani uongozi ni kununua, tambueni siyo kila kitu kinanunuliwa, hata mapenzi hayanunuliwi ndiyo maana dereva wa bodaboda anaweza kumnyang’anya tajiri mke,” alisema Wasira.

Related Posts