Undani wa barabara Dar kuitwa Sam Nujoma

Dar es Salaam. Barabara ya Sam Nujoma, jijini Dar es Salaam ilipewa jina hilo la Rais wa kwanza na Baba wa Taifa la Namibia, Samuel Daniel Shafiishuna Nujoma miaka 1980, lengo likiwa kuenzi harakati za mpigania uhuru huyo.

Nujoma kama alivyopenda kuitwa amefariki dunia leo Jumapili Februari 9, 2025, akiwa na miaka 95 akiacha alama nchini kwake Namibia, Afrika na duniani.

Moja ya alama kubwa ni kupigania uhuru wa Namibia na kufanikiwa kumuondoa mkoloni madarakani na kuwa Rais wa kwanza na Baba wa Taifa wa Taifa hilo mwaka 1990 hadi 2005.

Kabla ya kuwa Rais wa Taifa hilo, nchini Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alienzi harakati zake na kwa heshima, aliipa moja ya barabara za jijini  Dar es Salaam jina la mwanamema huyo mashuhuri wa Afrika, ambaye leo amelala usingizi wa umauti.

Barabara hiyo ni ile inayotoka Mwenge kuanzia kwenye makutano na Barabara ya Bagamoyo hadi Ubungo maarufu Barabara ya Sam Nujoma ikiwa ni ufupisho wa jina lake la Samuel na la baba yake, Nujoma.

Mmoja wa watu wanayoilewa vema historia ya Jiji la Dar es Salaam, Sheikh Khamis Mataka anasema awali barabara hiyo ilikuwa ikiitwa barabara ya Mlimani kabla ya kubadilishwa kuwa Sam Nujoma.

“Eneo lile kwa kuwa lilikuwa la Chuo Kikuu cha Mlimani, hata ile barabara tulikuwa tukiita barabara ya Mlimani.

“Miaka ya 1980, ndipo iliitwa jina la Sam Nujoma, lengo la Mwalimu (Nyerere) lilikuwa ni kumheshimu kiongozi huyo mkuu wa chama cha Ukombozi Namibia (Chama cha Swapo),” amesema.

Amesema kabla ya kupewa heshima hiyo, Nujoma alikuja Tanzania wakati huo bado hajawa rais, akiwa yupo kwenye harakati za kudai uhuru, ndipo Mwalimu Nyerere akampa heshima hiyo.

“Mwalimu alikuwa akiwaenzi wapigania uhuru wa Afrika akiwamo Nujoma, wakati ule Tanzania ndiyo ilikuwa mwenyekiti wa nchi tano za kupigania uhuru, ikiwamo nchi za Zambia na Msumbiji.

“Kwa heshima ya Nujoma, ndipo Serikali ya Tanzania ikaipa jina lake hiyo barabara,” amesema Sheikh Mataka.

Katika harakati za kudai uhuru wa Namibia, inaelezwa, Nujoma alifanikiwa kuonana na Mwenyekiti wa Tanu wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere aliyemsaidia kupata hati ya kusafiria ili iwe rahisi kwake kufanya harakati za ukombozi.

Kiongozi huyo alizaliwa katika mji wa Etunda, Kijiji cha Ongandjera Mei 12, 1929. Mama yake alijulikana kwa jina la Helvi Mpingana Kondombolo aliyefariki dunia mwaka 2008 na baba yake alijulikana kwa jina la Daniel Uutoni Nujoma.

Nujoma alijitumbukiza kwenye siasa mwanzoni mwa miaka ya 1950 kupitia vyama vya wafanyakazi, Novemba 1989, Namibia ilipata wabunge kufuatia uchaguzi ambao pia ulimtangaza yeye kama rais wa kwanza, Aliapishwa Machi 21, 1990.

Related Posts