Ushindi mechi nne mfululizo wamkosha Mourinho

KOCHA wa Yanga Princess, Edna Lema ‘Mourinho’ amesema ushindi wa mechi nne mfululizo kwenye ligi zinachangiwa na juhudi za wachezaji wake waliopambana hasa duru la pili.

Kwenye mechi 11 za ligi Yanga Princess imepata ushindi mechi sita, sare tatu na kupoteza mechi mbili ikisalia nafasi ya tatu na pointi 24.

Mourinho alisema mzunguko wa kwanza wa ligi haukuwa mzuri kwa upande wao wakitoa sare mbili mfululizo akiamini timu yake imebadilika kiasi hasa eneo la kushambulia ikifunga mabao mengi.

“Nimefurahi mechi tulizocheza mfululizo zote raundi ya kwanza tulitoka sare sio kitu rahisi tumetoka kwenye matokeo mabaya mfululizo ya sare lakini sasa naona kuna mabadiliko ingawa bado,” alisema Mourinho.

Akiongelea kuhusu ongezeko la wachezaji wapya kwenye kikosi chake dirisha dogo akiwemo Lydia Akoth, Aregash Kalsa na Jeaninne Mukandasyenga alisema;

“Wachezaji wapya wamekuwa na mchango mkubwa uwanjani, eneo la kiungo mshambuliaji lilikuwa changamoto kwetu, nafikiri wamekuja kusaidia kwa kiasi fulani, hatuwezi kusema moja kwa moja kwani bado tunaendelea kujenga timu.”

Kwenye sare ilizotoka Yanga duru na kwanza dhidi ya Bunda Queens, Alliance Girls na Mashujaa Queens 1-1, mzunguko wa pili Yanga imeshinda mechi zote dhidi ya Alliance 4-1, Bunda 3-0 na Mashujaa 2-1.

Related Posts