Uwezo: Daraja sifuri lifutwe mitihani ya kitaifa

Dar es Salaam. Ikiwa zimepita takriban wiki mbili tangu kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2024, Shirika la Uwezo Tanzania limependekeza kufutwa kwa daraja sifuri, likisema uwepo wake unawaathiri kisaikolojia vijana.

Badala yake, wamependekeza daraja la nne kutanuliwa wigo na kuwekwa utaratibu maalumu utakaowafanya wanaopata daraja la nne na sifuri kuingizwa vyuo vya ufundi stadi (VETA) bila malipo au kupewa mitaji wanapomaliza.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Uwezo Tanzania, Baraka Mgohamwende, katika mahojiano na Mwananchi juzi Ijumaa, Februari 7, 2025 alipokuwa akichambua matokeo ya kidato cha nne mwaka 2024. Baraka amesema kama inawezekana, ni vyema kuanza kufikiria namna ya kufuta daraja sifuri katika mitihani ya kitaifa, kwa sababu inatengeneza unyanyapaa na inawafanya vijana wajione hawafai kwa jambo lolote.

Takwimu za matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji, Dk Said Mohamed, Januari 23, 2025, yanaonyesha wanafunzi 39,433 walipata daraja sifuri, idadi ambayo ni sawa na asilimia 7.63 ya watahiniwa wote.

“Kusema wamepata sifuri inawarudisha nyuma kisaikolojia. Tunaona ufaulu wa daraja la nne ungeongezwa ukomo kutoka ilipo sasa, au badala ya kuwa na daraja sifuri, ingekuwa na daraja la tano kwa ajili ya kuwapa nafasi ambao hawakuweza kufaulu katika kiwango cha daraja lingine,” amesema Baraka.

Amesema kuongezwa kwa daraja lingine kungewafanya kutambuliwa na kuchukuliwa katika maeneo mengine yenye fursa, ikiwemo biashara au ajira mbalimbali. “Lakini kwa sasa imekuwa ngumu kwa sababu tumeamua kuwapa sifuri kwa kuona kuwa hawawezi kufanya chochote,” amesema.

Amesema kadri idadi ya watu inavyoongezeka, ni ngumu kuwarudisha wanafunzi wote waliopata sifuri darasani kurudia mitihani, lakini wanaweza kupewa daraja maalumu litakalowafanya watumike katika maeneo mengine. Akizungumzia wingi wa wanafunzi wanaoangukia daraja la nne na sifuri, amesema ipo haja ya kuendeleza juhudi ili elimu iwasaidie vijana kujinufaisha wenyewe wanapomaliza masomo na kusaidia familia na jamii kwa ujumla.

Uchambuzi unanyesha katika matokeo yaliyotangazwa watahiniwa wa shule waliopata daraja la I-III walikuwa 221,953 sawa na asilimia 42.96, huku wanaobakia wakiangukia daraja la nne na sifuri.

Matokeo ya 2024 yanaonyesha ufaulu wa daraja sifuri na la nne ni zaidi ya asilimia 56. Asilimia 56 ni kubwa, na ukiangalia shule moja moja, basi za umma ndiyo hazifanyi vizuri sana, shule binafsi wanajitahidi lazima tuangalie kwanini,” amesema.

Alitumia nafasi hiyo kutaka shule za kata zilizofanya vizuri kupongezwa kutokana na changamoto walizonazo, ikiwemo upungufu wa walimu.

Mitazamo ya wadau Kufutwa kwa daraja sifuri kulipokewa kwa mitazamo tofauti, na waalimu wastaafu, ambapo Ndayanse Mashaka amesema inaweza kusaidia wanafunzi kujiamini na kutojisikia vibaya ndani ya jamii, lakini ndani yake inaweza kufanya wabweteke na kuona hawana cha kupoteza.

Kwa upande wake, Lissa Komba amesema uwepo wa daraja sifuri unawafanya wanafunzi kuweka bidii katika kusoma ili wasikose fursa mbalimbali baadaye. “Kuongeza daraja ni wazo zuri, lakini hili lifanyike kwa tahadhari tusije angusha zaidi elimu yetu, kwani tabia za wanafunzi shuleni tunazijua,” amesema Lissa.

Katika hilo, Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko, amesema kuondoa daraja sifuri ni hatua nzuri kuelekea katika ujenzi wa umahiri wa aina fulani ya ujuzi, kama inavyoakisiwa katika mabadiliko ya mitaala yanayoanza kutekelezwa, ingawa ina faida na hasara. Amesema hiyo inaweza kupunguza unyanyapaa na athari za kisaikolojia kwa wanafunzi darasani.

Akizungumza na Mwananchi, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Juma Kipanga, amesema mara zote mitihani hutumika kupima uelewa wa wanafunzi juu ya kile walichofundishwa. “Huu ni utaratibu wa duniani kote, suala la mitihani na kutoa madaraja ni suala la duniani kote, hivyo inatusaidia kujua kwa kiasi gani wanafunzi wanaelewa na tuko wapi.

“Lakini kwenye kufuta daraja sifuri, Waziri (Profesa Adolf Mkenda) anaweza kuwa na majibu mazuri zaidi kwa sababu yeye ndiye mzungumzaji wa wizara, hivyo ningeshauri umtafute,” amesema Kipanga.

Hata hivyo, Mwananchi ilishindwa kumfikia Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, ambaye kwa sasa yuko katika msiba wa mama yake mzazi.

Oktoba mwaka 2013, Serikali iliwahi kutangaza kufuta daraja sifuri katika matokeo ya elimu ya sekondari nchini na kuongeza daraja la tano. Pia matokeo ya kidato cha nne kwa watahiniwa wanaorudia mitihani yatahusisha matokeo yao ya awali wakati wakiwa shuleni ili kuwarahisishia kupata alama nzuri.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa wakati huo, Profesa Sifuni Mchome, alisema pamoja na marekebisho hayo, pia wameongeza daraja B la juu (B+) kwa alama za ufaulu, ambapo daraja A kiwango cha ufaulu ni kati ya alama 75 na 100, daraja B la juu (B+) ni kati ya alama 60 na 74, daraja B la kati (B) ni 50 na 59.

Kwa wale wa daraja C kati ya 40 na 49, daraja D kati ya 30 na 39, daraja E kati ya 20 na 29, na daraja F ni kati ya alama 0 na 19.

Hata hivyo, suala hili halikudumu na baadaye upangaji wa madaraja ulirudi kama ilivyokuwa awali.

Wakati kundi kubwa la wanafunzi waliomaliza wakipata daraja la nne na sifuri, Uwezo inapendekeza kuwepo kwa utaratibu maalumu utakaowawezesha kujiunga vyuo vya ufundi ili wajifunze kazi za mikono au vya kati.

“Swali la kujiuliza, je, mfumo wetu umejiandaaje kupokea asilimia 56 katika vyuo vya kati au ufundi? Ingekuwa wamemaliza katika mtaala wa ujuzi uliozinduliwa, tungekuwa tumetengeneza mazingira mazuri ya kupokea wanafunzi wa kidato cha nne, lakini bahati mbaya mazingira hayajaandaliwa kutosheleza kupokea idadi kubwa ya watoto hao,” amesema.

Amesema umefika wakati sasa wadau na Serikali iangalie namna ya kuwatafutia fursa ili kuwaondoa mitaani, jambo linaloweza kuwavuta katika tabia ovu.

“Ipo haja ya serikali kuandaa utaratibu wa wanaopata daraja la nne wasajiliwe katika vyuo vya ufundi ili wasibaki bila ujuzi, na ikiwezekana elimu ya ufundi itolewe bure au kwa mikopo, kwa sababu wakimaliza wanakwenda moja kwa moja kutumika katika jamii kwa kutumia kile alichosoma,” amesema Baraka.

Tofauti na hilo amependekeza kutolewa kwa mitaji kama kianzio wanapomaliza vyuo ili kuwafanya vijana wengi waweze kujiunga katika masomo ya ufundi.

Wakati akitangaza matokeo haya, Katibu Mtendaji wa Necta alisema somo la hisabati lina ufaulu ulio chini ya wastani, ambao ni asilimia 25.35, ikiwa ni pungufu kidogo kutoka asilimia 25.42 mwaka 2023. Hilo, Uwezo inasema watoto wote wanaweza kufahamu hesabu kama ilivyo Kiswahili, lakini mbinu zinazotumika si rafiki. Hiyo ni kwa sababu watoto wangependa wawe kwenye darasa lenye furaha bila kiboko.

Katika hilo, Uwezo imesema imekuja na mwongozo wa kusaidia walimu wa madarasa ya awali ili kuhakikisha wanafunzi wao wanaweza kumudu kusoma na kuhesabu hadi wanapofika darasa la pili, kwani asipofanya vizuri katika ngazi hiyo, ni ngumu kufanya vizuri katika masomo mengine kama ya sayansi, kwa sababu hajui kusoma.

“Hata kungekuwa na walimu wachache lakini wenye mbinu ambao kuwafanya watoto wafurahie darasa, wangefaulu. Darasa la uwezo la ‘ujifunze’ hakuna kiboko, mwalimu anaimba na kucheza na watoto kama sehemu ya kujifunza,” amesema.

Akieleza namna darasa hilo linavyofanya kazi, amesema wakiwa darasani wanavua viatu, darasa ni tupu, halina madawati wala ubao, wanatumia nyenzo mbadala, ambalo linatengenezwa kutokana na mazingira yao, kama ni mawe ili wajifunze.

Amesema jambo hilo limefanya watoto waliokimbia shule warudi, kwa sababu mazingira ni rafiki, hivyo mbinu za ufundishaji ni muhimu zaidi na vifaa kwa masomo ya sayansi ni jambo ambalo linapaswa kuangaliwa zaidi.

Ufaulu hafifu masomo ya sayansi

Matokeo ya kidato cha nne 2024 yananyesha kuwapo kwa idadi ndogo ya wanafunzi waliopata daraja A hadi C katika mitihani ya fizikia na baiolojia, hali ambayo inatafsiriwa kuwa si ishara nzuri. Hiyo ni kutokana na taifa kuwa katika hatari ya kukosa vijana watakaomudu kutatua changamoto za karne ya 21.

Matokeo haya yanaonyesha kuwa wanafunzi waliopata daraja A hadi C katika somo la fizikia walikuwa asilimia 32.59, huku Baiolojia wakiwa asilimia 40.04, huku kemia ikifanya vizuri kwa kuwa na asilimia 74.95. “Kinachotakiwa ni kuweka mazingira rafiki na sahihi ya ujifunzaji. Uwekezaji katika vifaa vya kujifunzia ni mdogo sana.

“Shule nyingi hazina maabara, hivyo tunapaswa kuongeza vifaa na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata stadi ya sayansi inavyotakiwa,” amesema Nkoronko.

Related Posts