WALIPAKODI KATAVI WAKOSHWA NA UTENDAJI WA TRA WAMZAWADIA CG MWENDA

 

Walipakodi wa mkoa wa Katavi wameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kukusanya Kodi bila kutumia nguvu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda pamoja na uongozi wa TRA mkoani Katavi tarehe 07.02.2025 wamesema katika siku za karibuni kumekuwa na ukaribu baina yao na TRA hali ambayo imewafanya wajisikie furaha kulipa Kodi.

Kudhihirisha ukaribu huo baina yao na TRA Walipakodi hao wamemkabidhi zawadi na kumshukuru kwa kuwatembelea Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda na kumtaka aendelee kusimamia nidhamu ndani ya Mamlaka hiyo.

Abdi Kasembo na  Daniel Tarimo ni miongoni mwa Wafanyabiashara hao ambao wameeleza kuwa katika kipindi hiki kumekuwa na fursa ya kufanya majadiliano na TRA kuhusu makadirio na kuruhusiwa kulipa kwa awamu.

“Kamishna Mwenda kazi unahoifanya Mungu anaiona, Sasa hivi hatuna hofu na tumekuwa marafiki na TRA kupitia uongozi wako, tunashukuru sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kukuteua na kukuamini” wamesema Wafanyabiashara hao wa mkoa wa Katavi.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda akizungumza na Wafanyabiashara hao mkoani Katavi amesema jukumu la TRA ni kukuza biashara na kusimamia ustawi wa Wafanyabiashara nchini.

Bw. Mwenda amesema katika kipindi hiki TRA imejipanga kuboresha huduma kwa Mlipakodi na kuleta usawa katika kukusanya Kodi kwa kuhakikisha kila anayestahili kulipa Kodi analipa.

BW. Mwenda amesema ili kuleta usawa kila mmoja anao wajibu wa kuwafichua watu wanao kwepa kodi kwa kutokusajili biashara au kwa kutumia risiti bandia.

Bw. Mwenda amesema TRA imewekeza katika kutoa Elimu kwa Mlipakodi ili kuhakikisha mazingira ya Wafanyabiashara nchini yanaimarika na kuhakikisha kuwa hakuna biashara yoyote nchini inayoweza kufa ndiyo maana TRA imewekeza katika kutoa Elimu kwa Mlipakodi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mhe. Majid Mwanga alipokutana na CG Mwenda amesema uongozi wa wilaya yake umekuwa ukishirikiana na TRA kutoa Elimu kwa Mlipakodi huku akiahidi kuendelea kutoa Elimu kwa Mlipakodi ili kuongeza wigo wa ulipaji Kodi nchini. 

Mwisho

Related Posts