KOCHA wa African Sports ‘Wanakimanumanu’, Kessy Abdallah amesema angalau kwa sasa timu hiyo inaendelea kuimarika tofauti na mwanzoni na sababu kuu ni mbili, kuchezea nyumbani na wachezaji kufuata maelekezo yake kwa ufasaha.
Timu hiyo imeshinda michezo miwili mfululizo kwa mara ya kwanza msimu huu, tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 2-0 na Transit Camp Januari 12, mwaka huu, baada ya kuzifunga Cosmopolitan na Green Warriors kila mmoja wao mabao 2-1.
“Wachezaji wanafuata vyema maelekezo na hata ukiangalia michezo tunayopoteza tulikuwa tunakosa pia bahati tu, nashukuru tunaendelea kuimarika kadri siku zinavyokwenda, hii inaturejeshea morali yetu ya kupambana zaidi mzunguko huu wa pili.”
Kessy aliongeza sababu nyingine inayochangia ni sapoti kubwa wanayoipata kutoka kwa mashabiki zao hasa baada ya kuchezea mechi zao za nyumbani Uwanja wa kituo cha TFF Mnyanjani mjini Tanga, tofauti na mwanzoni walipokuwa Jamhuri Morogoro.
Timu hiyo ambayo ni mabingwa wa Kombe la Muungano mwaka 1988, imepanda Ligi ya Championship msimu huu baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023 iliposhika nafasi ya 14 na pointi 23, huku msimu uliopita ikiwa ndio mabingwa wa First League.