Kiongozi wa kidini wa Jumuiya ya Waislamu wa Kishia Waismaili, Aga Khan IV, alizikwa jana Jumapili, Februari 9, mjini Aswan, Misri na maziko yake yalihudhuriwa na familia pamoja na watu wachache wa karibu.
Kifo cha Prince Karim -Imamu wa 49 wa Waislamu wa Kishia Waismaili- kilitangazwa Jumanne, Februari 4, 2025, na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (Aga Khan Development Network), pamoja na jamii ya kidini ya Waismaili.

Mwanawe mwenye umri wa miaka 53, Rahim Al-Hussaini, ametangazwa kuwa Aga Khan V, kiongozi wa kiroho wa mamilioni ya Waismaili duniani, kwa mujibu wa wosia wa baba yake.
Jumamosi, ibada ya mazishi ya faragha ilifanyika katika kituo cha jamii ya Waismaili mjini Lisbon, ikihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, Mfalme wa zamani wa Hispania, Juan Carlos, na Rais wa Ureno, Marcelo Rebelo de Sousa.
Kwa wafuasi wake, Aga Khan anachukuliwa kuwa mzawa wa moja kwa moja wa Mtume Muhammad (S.A.W) na anaheshimiwa kama kiongozi wa hadhi ya kitaifa.
Gavana wa Aswan aliikaribisha familia ya Prince Karim katika uwanja wa ndege wa jimbo hilo kusini mwa Misri siku ya Jumamosi.
“Wakati wosia wake ulipofunguliwa, ilibainika kuwa alikuwa ameomba azikwe Aswan karibu na babu yake, Sultan Muhammad Shah, na bibi yake, Om Habiba,” alisema Meja Jenerali Ismail Kamal.

Waombolezaji wa Kishia Waismaili walitembea kwa heshima huku kengele zikilia wakati wa ibada ya mazishi katika jimbo la Aswan.
Mwili wa Prince Karim ulisafirishwa kwa gari kabla ya kubebwa na waombolezaji walioufunika kwa sanda nyeupe na kuupeleka kwenye boti katika Mto Nile kuelekea katika mazishi yake.