Ateba afichua siri ya Che Malone Simba

MSHAMBULIAJI wa Simba, Lionel Ateba amemtaja beki wa timu hiyo, Che Fondoh Malone kama mtu aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuzoea haraka maisha ya ndani na nje ya uwanja baada ya kujiunga na klabu hiyo.

Ateba amejiunga na Simba katika dirisha kubwa la usajili akitokea USM Alger ambapo hadi sasa ameifungia timu hiyo mabao manane kwenye Ligi Kuu na pia amefumania nyavu mara tatu katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza na www.cafonline.com, Ateba amesema kuwa kuna mchango mkubwa wa Che Fondoh Malone katika mafanikio yake kwa miezi michache aliyoichezea Simba.

“Nadhani uwepo wake umenisaidia sana kuzoea kirahisi. Muda mfupi baada ya mimi kuwasili tulizungumza. Alijaribu kuzungumza na mimi na ikawa rahisi kwangu. Lakini pia mimi ni mchezaji wa kulipwa, natakiwa kuwa na uwezo wa kumudu kwa haraka kile kitakachokuja mbele yangu.

“Ni mtu anayejichanganya na wengine na tunafahamiana vizuri tangu zamani iwe nje au ndani ya eneo la kuchezea. Kule Cameroon tulicheza pamoja hivyo anajua ninacheza vipi. Anajua nakimbia vipi. Anajua muda gani wa kunitazama hivyo hili linakuwa rahisi kwa sababu tunafahamiana nje ndani ya kiwanja. Sio jambo jipya ni muwendelezo tu na unavyofahamiana na mchezaji mwenzako inakuwa rahisi,” amesema.

Ateba hakusita pia kuwataja kocha Fadlu Davids na wachezaji wa Simba kuwa wamechangia kumfanya amudu kwa haraka mazingira ya Tanzania na soka la hapa.

Mshambuliaji huyo amesema malengo yake ni kuhakikisha Simba inafanya vizuri hasa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Unajua mashindano kama Kombe la Shirikisho ni makubwa na unatakiwa utoe kila ulichonacho. Ni uzoefu mpya lakini ni muendelezo kwa vile nimeyajua kwingineko. Ni mara yangu ya nne kushiriki haya mashindano na nina furaha kuwa na uwezo wa kucheza katika klabu kubwa ambayo ni Simba.

“Mwaka uliopita nikiwa na USM Alger tulifika nusu fainali licha ya kwamba hatukucheza na RS Berkane. Kwangu mimi ni kama mwendelezo kwa sababu nilicheza vizuri nikiwa na ile timu ya Algeria na sasa naendelea kusaidia timu yangu,” amesema Ateba.

Related Posts