Balaa la Waarabu! Kumng’oa Ngoma Msimbazi

KLABU kutoka ukanda wa Afrika Kaskazini, maarufu kama Waarabu wameendelea kuvuna watu kutoka katika Ligi Kuu Bara baada ya safari hii kuivamia Simba na kumwekea mezani kiungo Fabrice Ngoma kitita cha pesa.

Taarifa ya kutakiwa kwa Ngoma zimekuja huku tayari Waarabu wakiwa wameshamvuta aliyekuwa kocha wa Yanga, Sead Ramovic na mshambuliaji wa Singida BS aliyekuwa akicheza kwa mkopo Fountain Gate, Seleman Mwalimu na ikielezwa pia inamnyemelea kocha wa Simba, Fadlu Davids.

Kwa ishu ya kocha Fadlu, Simba ni kama imepona kwa sasa baada ya kocha huyo kuwagomea Wamorocco akiwaambia ana jambo lake Kombe la Shirikisho Afrika na pia kwenye Ligi Kuu Bara, lakini sasa presha mpya imebuka Msimbzi baada ya Walibya kutua kwa Ngoma na kutaka kumng’oa ikiwa ni siku chache tangu walipomkosa Clement Mzize na Stephane Aziz Ki wa Yanga.

Ipo hivi. Klabu ya Al- Ittihad inatingisha soka la Afrika ikiwa na akili ya kusuka kikosi upya, imemwekea Ngoma mezani dau la Dola 500,000 (zaidi ya Sh1 bilioni) ili kumng’oa Msimbazi. ili kununua mkataba wake na Simba.

Presha ya Ngoma imekuja kufuatia Al-Ittihad kumpa ajira kocha mmoja mkubwa, Mhispaniola Juan Carlos Garrido ambaye ndiye aliyetaka Ngoma achukuliwe haraka.

Garrido aliwahi pia kufanya kazi na Ngoma mwaka wa mwisho alipokuwa kocha wa Raja Athletic ya Morocco mwaka 2019, lakini hakufanya naye kazi sana kabla ya kocha huyo mwenye misimamo kuamua kutimka.

Walibya hao wameshakubaliana kila kitu na Ngoma na sasa imebaki hatua ya Simba kumalizana nao tu ambapo mabosi wa Wekundu hao wanasita kutopokea fedha hiyo ndefu kufuatia Mkongomani huyo kubakiza miezi mitano kwenye mkataba wake.

Simba ilikuwa mezani na Ngoma ikibakiza hatua ya kumsainisha tu mkataba mpya hatua ambayo kwa sasa imemfanya Mkongomani kuyo kuwa mzito kuweka wino akiwaambia mabosi hao wasubiri kwanza.

Simba inataka kufanya biashara hiyo sasa ili ivune fedha kwenye usajili huo kuliko Ngoma kuondoka bure mwisho wa msimu.

Simba iliona mabadiliko makubwa ya Ngoma akikiwasha vikali kiasi cha kubariki uamuzi wa kocha Fadlu Davids aliyempa ukubwa wa kuwa nahodha msaidizi wa kikosi hicho.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, muda wowote kiungo huyo anaweza kusepa kwani mabosi wa Msimbazi wamevutiwa na kiasi hicho na uamuzi wa kiungo huyo kuwagomea mkataba mpya ili wasipate hasara.

Jeuri ya kutaka kumruhusu Ngoma kuondoka, inatokana na ukweli katika kikosi cha sasa kuna wachezaji wanaomudu kucheza nafasi anayocheza Mkongoman huyo akiwamo Debora Mavambo, Mzamir Yassin, Augustine Okejepha na Yusuf Kagoma ambaye kwa sasa amekuwa akitengeneza pacha na kiungo huyo anayetakiwa Libya.

Kocha wa Simba, Fadlu amewagomea FAR Rabat ya Morocco juu ya dili la kutaka kumng’oa Msimbazi, akiwaambia hataki kuifanyia ‘ubaya ubwela’ Simba inayopigania mataji muhimu hivyo kama wanamhitaji siriazi basi wasubiri msimu umalizike.

Jibu hilo la Fadlu likawafanya FAR Rabat kufanya uamuzi wa haraka kumchukua chaguo lao la pili Mreno Alexander Santos, ambaye ni kocha wa zamani wa CS Sfaxien na Petro Luanda ya Angola.

Hadi jana Santos alibakiza mambo machache kutambulishwa kuwa kocha mpya wa timu hiyo ya Jeshi la Mfalme wa Morocco ambayo msimu uliopita ikiwa chini ya Nasreddine Nabi aliyepo Kaizer Chiefs ya Sauzi, iliukosa ubingwa wa Botola Pro mbele ya Raja Casablanca aliyekuwapo Fadlu kama kocha msaidizi.

Related Posts