Bodi ya mikopo yatoa Sh8.2 trilioni

Dodoma. Jumla ya Sh8.2 trilioni zimeshatolewa mkopo kwa zaidi ya wanufaika 830,000 wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Takwimu hizo zimetolewa jijini Dodoma leo Jumatatu Februari 10, 2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Ndombo wakati akifungua Maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Profesa Ndombo amesema kiasi hicho kimekwenda kwa wanufaika zaidi ya 830,000 ambao walionekana kuwa sifa za kukopeshwa lakini akasisitiza suala la urejeshaji kwa walionufaika hata kupitia kwa waajiri wao.

Maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu pia yataendelea katika mikoa ya  Mwanza na Dar es Salaam na yatahitimishwa na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa Februari 17, 2025.

Profesa Ndombo amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu juu bila ubaguzi kwa namna yoyote.

“Kikubwa tunasisitiza kwa wanufaika kuendelea kurejesha madeni ya mikopo yenu na kwa wenye uwezo wanaruhusiwa kulipa hata kwa mkupuo, waajiri tunaomba mtusaidie katika hili,” amesema Profesa Ndombo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo, Profesa Hamisi Dihenga amesema kwa sasa wamejidhatiti katika kuwahudumia wahitaji na kurahisisha upatikanaji wa mikopo kuliko ilivyokuwa awali.

Profesa Dihenga amewaomba Watanzania kujenga imani kwa Bodi ya Mikopo kutokana na mabadiriko makubwa yaliyofanywa ikiwemo matumizi ya mifumo ya TEHAMA.

Tangu kuundwa kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Profesa Dihenga ni Mwenyekiti wa nne huku Mwenyekiti wa kwanza akiwa ni Hayati Nimrod Mkono.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Alhaj Jabil Shekimweri amesema kuwa utoaji wa mikopo kwa sasa umeipunguzia Serikali malalamiko yaliyokuwepo awali ambapo baadhi ya wanafunzi walikuwa wakibaguliwa kwa kigezo cha kusoma shule za binafsi.

Kwa mujibu wa Alhaj Shekimweri, hivi sasa kila mmoja anapata mikopo ilimradi akiwa na sifa za kukopesheka bila kujali shule aliyosoma hata kama ilikuwa ni ya kulipiwa jambo lililopunguza malalamiko na manung’uniko kwa wananchi.

Related Posts