Dar es Salaam. Mshtakiwa Peter Gasaya (33) ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya JATU PLC, anayekabiliwa na kesi uhujumu uchumi, amemuomba hakimu anayesikiliza kesi yake, asisaini hati yake ya kumtoa gerezani na kumpeleka mahakamani mpaka hapo upelelezi wa kesi yake utakapokamilika.
Gasaya anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Ametoa ombi hilo leo Jumatatu, Februari 10, 2025, muda mfupi baada ya upande wa mashtaka kudai upelelezi wake bado unaendelea.
Amedai haoni sababu ya yeye kupelekwa mahakamani wakati kila tarehe anayopangiwa, upande wa mashtaka wanaieleza Mahakaka hiyo kuwa upelelezi wake bado unaendelea.
“Mheshimiwa hakimu, naomba hati ya kunitoa garezani kuletewa mahakamani hapa usiisaini mpaka pale upande wa mashtaka watakapokamilisha upelelezi wa kesi hii, ndio niletwe Mahakama hapa,” alidai Gasaya.
Gasaya alipoulizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi anayesikiliza kesi hiyo, Godfrey Mhini sababu za kutoa ombi hilo, alijibu kuwa haoni sababu ya kupelekwa Mahakamani hapo kwa madai kuwa kila akipelekwa anaambia upelekezi haujakamilika.
“Mheshimiwa hakimu, kesi yangu ni ya muda mrefu na upelelezi wake mpaka sasa bado haujakamilika, hivyo naomba tarehe ijayo nisiletwe Mahakama kwa sababu naletwa Mahakamani kwako, nikifika naambiwa upelelezi bado narudishwa, hivyo ni bora tu nikae mahabusu mpaka upande wa mashtaka utakapokamilisha upelelezi, ndio niletwe” alidai mshtakiwa.
Hata hivyo, Hakimu Mhini, alimwambia mshtakiwa huyo atakuwa anapelekwa mahakama hapo kila baada ya siku 14.
Mhini baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 20, 2024 kwa kutajwa.
Awali, wakili wa Serikali Eva kassa akishirikiana na Roida Mwakamele alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili kutakwa.
Kwa mara ya kwanza Gasaya alifikishwa katika Mahakamani hapo, Desemba 29, 2022 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili ambayo ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh 5,139,865,733 kutoka Saccos ya Jatu.
Mshtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.
Shtaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es salaam.
Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu Saccos, alijihusisha na muamala wa Sh 5.13 bilioni kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos iliyopo benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC liyopo katika benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.