Dodoma. Bunge la Tanzania limeazimia Serikali ihakikishe mifuko ya hifadhi ya jamii isimamiwe ipasavyo katika kuhakikisha uwekezaji unaofanywa ni wa tija na unaendana na michango.
Bunge limeazimia baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti taarifa ya shughuli zake wa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025 iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu, Febrauri 10, 2025.
Akiwasilisha ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2020/21, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere alisema amebaini mifuko ya hifadhi ya jamii iko hatarini kupata hasara ya mabilioni ya shilingi kutokana na utekelezaji duni wa miradi yake ya ubia na kampuni mbalimbali.
Leo Jumatatu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Oran Njeza amesema mifuko ya hifadhi ya Jamii imekuwa inafanya uwekezaji usio na tija ambapo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22, 2022/23, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma, (PSSSF), umelipa mafao ya wastaafu yenye thamani ya Sh4.34 trilioni na kupata faida (Return) ya Sh1.8 trilioni.
Amesema takwimu hizo zinaonyesha kiasi kilicholipwa ni kikubwa ukilinganisha na faida inayotokana na uwekezaji wake.
Amesema pia kiwango cha uhimilivu cha mfuko ni asilimia 36.4 ikilinganishwa na kiwango kinachokubalika cha asilimia 60 na lengo la chini la uhimilivu la asilimia 40.
Njeza amesema usimamizi wa mifuko ya hifadhi ya jamii hufanywa na Benki Kuu (BoT) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
“Kwa hiyo basi Bunge linaazimia kwamba Serikali ihakikishe kuwa mifuko hiyo inasimamiwa ipasavyo katika kuhakikisha kuwa uwekezaji unaofanywa ni wa tija na unaendana na michango,”amesema.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza vihatarishi na kuwezesha mifuko kulipa mafao ya wastaafu kwa wakati.
‘Tathimini ya madeni’
Pia, Bunge limeazimia, Serikali kufanya tathmini ya kina ya madeni yote ya wazabuni, wakandarasi na watoa huduma kuanzia Februari 2024 hadi 30 Aprili, 2025 ili kubaini ni kiasi gani Serikali inadaiwa.
Njeza amesema wanakubaliana na mapendekezo na kama Serikali wanakubaliana nayo yale yote yanahusiana na hatua za kikodi ikiwemo refernd za mambo ya kikodi.
Njeza amesema changamoto ya ulipaji wa madeni ya wazabuni, wakandarasi na watoa huduma imekuwa ni jambo la muda mrefu na limekuwa likiathiri utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa miaka tano mfululizo.
Amesema tangu mwaka 2022 ilipofanyika tathmini ya kina na kubaini Serikali inadaidwa Sh3.2 trilioni na tangu kipindi hicho haijafanyika tathmini ya kina kama hiyo.
“Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia, Serikali kufanya tathmini ya kina ya madeni yote ya wazabuni, wakandarasi na watoa huduma kuanzia Februari hadi 30 Aprili, 2025 ili kubaini ni kiasi gani Serikali inadaiwa,” amesema.
Amesema Serikali iweke ukomo wa siku 90 wa uhakiki wa madeni kwa kufanya mabadiliko kwenye Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma Sura ya 348 ili kuondoa kisingizio cha kuchelewa kulipa kwa sababu ya kufanya uhakiki.
“Serikali kuwasilisha taarifa ya tathmini kwenye kamati ya bajeti sanjari na hatua za kulipa madeni hayo,” amesema.
Njeza amesema kwa hatua hizo zikifanyika zitaondoa madhira ambayo sekta binafsi nchini inapitia ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu kufilisika kutokana na Serikali kutolipa kwa wakati.
TRA ipewe mamlaka ya kiuchunguzi
Njeza amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia Kamishna Mkuu ipewe uwezo wa kufanya uchunguzi wa kodi (Tax Investigation).
Amesema TRA, imekuwa ikifanya uchunguzi wa masuala ya kodi, ili kubaini ubadhirifu unaofanywa na Kampuni au wafanyabiashara wasio waaminifu na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za kodi pale inapobainika mfanyabiashara au Kampuni ina makosa.
Amesema katika kufanya chunguzi hizo huwa wanatumia askari polisi ambao hawana utaaalamu kuhusu masuala ya kodi na wakati huo huo ndio wanatakiwa kuchukua maelezo ya mtuhumiwa.
Amesema hatua, hiyo imekuwa inafanya mamlaka ya mapato kupoteza kodi ambayo inatakiwa kukusanywa pindi shitaka linapofika mahakamani.
“Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na Wizara ya Fedha kufanya kikao cha pamoja kabla ya vikao vya kamati vya Machi, 2025 ili kubainisha utaratibu utakaotumika kuondokana na changamoto hii,”amesema.
Njeza amesema endapo itaonekana kuna ulazima wa kufanya mabadiliko yafanyike kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2025 na kuwa taarifa ya kikao hicho na maamuzi yake yawasilishwe kwenye kamati.
Akichangia, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema wanakubaliana na mapendekezo ambayo kamati imeyapeleka bungeni.
“Yale ambayo moja kwa kwa moja yanahusiana na hatua za kikodi ikiwemo refund za masuala ya kodi kwa kuwa tuko katika mchakato wa mambo mawili, tuna jambo kubwa ambalo serikali tunafanya la kurekebisha mifumo kutoka katika masuala ya kianalogia,” amesema.
Amesema wameshafanya hatua kubwa katika kodi za ndani na kwamba suala hilo ndio lilikuwa linasababisha utaratibu wa rejesho la fedha (refund), tathimini na makusanyo ya kodi za miaka ya nyuma kuchukua muda mrefu.
“Sasa tutakapokuwa tumekamilisha masuala haya ya kimfumo tutaweza kutaja rasmi nilini tunaweza tukatekeleza yale ya muda wa refund (rejesho la fedha),” amesema.
Dk Mwigulu alipongeza wabunge kwa mjadala wa taarifa ya kamati hiyo na kuwa wameendelea kuthibitisha kuwa ni bunge lenye watu makini.