Chama cha Malema chamcharukia Musk, chaitaja Starlink

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita saa chache tangu Mmiliki wa mtandao wa X na Mkurugenzi wa Idara ya Ufanisi wa Serikali ya Marekani, Elon Musk amuite kiongozi wa chama cha EFF cha Afrika kusini, Julius Malema kuwa mhalifu wa kimataifa, chama hicho kimemjibu.

Chanzo cha Musk kumuita jina hilo Malema ni mabishano yaliyoendelea katika mtandao wa X baada ya video ya Malema ya mwaka 2018 iliyochapishwa tena jana Februari 9, 2025. Malema alisema, “Tutakata koo la watu weupe,” akimaanisha kumuondoa aliyekuwa meya (mzungu) wa Nelson Mandela Bay, Athol Trollip.

Baada ya Musk kuandika hivyo, Malema amemjibu kuwa hataacha kupigania haki za watu weusi na kutaka usawa, huku akimtuhumu Musk kunufaika na unyonyaji unaofanywa na watu weupe.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Februari 9, 2025 na chama cha EFF imesema haijashtushwa na tamko hilo, kwa sababu Malema ni mwanaharakati anayetetea thamani ya mwafrika, hivyo mabeberu hawawezi kumpenda.

“Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa EFF (Malema), amekuwa mstari wa mbele katika mapambano barani Afrika, na diaspora tangu harakati zake za ukombozi akiwa kijana, ameziendeleza harakati hizo za ukombozi wa Afrika Kusini. Muhimu wa mtazamo wake sio tu kuhusu uhuru wa kiuchumi na ukombozi wa watu wa Afrika, huo umekuwa upinzani mkali dhidi ya ubeberu wa magharibi.

“Kwa hiyo haishangazi kuona Julius Malema anatangazwa kuwa adui na mfumo wa kibepari wa kimataifa, ajenda iliyoendelezwa na watu kama vile Elon Musk,” imesema taarifa hiyo.

Imesema dhana potofu na tabia mbaya ya Rais wa EFF kama mauaji ya halaiki ni onyesho la kando ambalo linalenga kudhoofisha mawazo ambayo anawakilisha.

Wagusia Elon Musk kuingiza Starlink Afrika Kusini

Mbali na suala la Malema, EFF pia imesema chama hicho kitahakikisha huduma ya intaneti ya satelaiti ya Starlink inayomilikiwa na bilione huyo wa Marekani haitafanya kazi nchini Afrika Kusini kama haitatimiza vigezo vya asilimia 30 ya umiliki wa ndani.

Kampuni ya Starlink ilianza mazungumzo na serikali ya Afrika Kusini kuhusu kuingiza huduma hiyo Septemba 2024.

“Zaidi ya hayo, EFF inatoa ahadi thabiti kwamba Starlink ya Elon Musk haitawahi kufanya kazi nchini Afrika Kusini, bila kuzingatia sheria za ndani zinazotaka lazima kuwe na umiliki wa ndani wa asilimia 30,”imeeleza taarifa hiyo.

Chama hicho chenye viti 39 katika Bunge la Taifa la Afrika Kusini lenye jumla ya viti 400 kimeendelea kushikilia msimamo kuwa ardhi irejeshwe kwa Wafrika.

“Kanuni inabakia kuwa usawa nchini Afrika Kusini unatokana na kurejesha ardhi kwa watu wa Afrika, na hili litafikiwa kwa kunyang’anywa watu weupe bila kulipwa fidia.

“Kosa ambalo Musk amefanya dhidi ya kiongozi wa EFF ni kuingilia mambo yetu ya ndani ambayo hatuyachukulii kirahisi, na lazima aonekane kama ubeberu anayetaka kudhoofisha uhuru wa kiuchumi na kisiasa wa Afrika Kusini kupitia vikwazo, na ni sehemu ya majaribio mabaya ya uhusiano mbaya kati ya Afrika Kusini na Marekani,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo yenye kurasa mbili.

Aidha taarifa hiyo imedai kuwa Elon Musk kutokana na nafasi aliyopewa na Marekani chini ya Rais Donald Trump atasababisha taifa hilo kuanguka.

“EFF ilimtangaza Elon Musk kama adui wa Afrika Kusini, na mtekaji wa utawala nchini Marekani ambaye atasababisha mataifa hayo kuanguka. Mataifa yote yanayoendelea, pamoja na Urusi, China, India, na mataifa yote ya Afrika yanapaswa kutenga na kukataa biashara zote zinazofanywa na Elon Musk katika mataifa yao,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia imesema chama hicho hakitatishika ama kurudi nyuma katika kukabiliana na ubeberu.

Related Posts