Chirwa ashtua, Bwenzi aendeleza moto Ken Gold ikiilaza Fountain Gate

Achana na ushindi wa mabao 2-0 waliopata Ken Gold dhidi ya Fountain Gate, ishu ilikuwa ni staili ya ushangiliaji wa nyota wa timu hiyo, Obrey Chirwa ambayo imeamsha hisia tofauti kwa wadau na mashabiki wa soka.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa, Ken Gold ilionekana kuwa imara wakiwapa wakati mgumu wapinzani hao ambao mara nyingi walifanya kazi ya kuokoa hatari.

Sele Bwenzi ndiye alianza kuwanyanyua mashabiki wa Ken Gold kwa bao la kwanza kwa penalti katika dakika 33 ikiwa ni bao lake la pili katika mechi mbili baada ya lile shuti lake alilomtungua Kipa wa Yanga, Djigui Diara kutokea katikati ya uwanja wakati Ken Gold ilipolala 6-1 kwenye Uwanja wa KMC Dar es Salaam wiki iliyopita.

Chirwa aliyeingia kutokea benchini kuchukua nafasi ya Emmanuel Mpuka, alifunga bao la pili katika dakika ya 88, huku akienda kwenye kibendera na kutembea mithili ya kikongwe, ambayo imetafsiriwa kuwa anatuma ujumbe kwamba bado hajazeeka na anazidi kung’ara pengine kutokana na mijadala iliyodumu kwa muda mrefu kuwa KenGold licha ya kusajili wachezaji 24 wapya katika dirisha dogo lililomalizika mwezi uliopita, huenda wakaendelea kupata matokeo yasiyoridhisha kwa kuwa imesajili ‘wazee’.

Nyota huyo raia wa Zambia aliwahi kutesa na timu kadhaa ikiwa ni Yanga, Azam, Kagera Sugar na sasa anaitumikia Ken Gold inayopambana kukwepa kushuka daraja.

Fountain Gate iliyotoka kuwasimamisha Simba kwa sare ya bao 1-1 licha ya kuonyesha ushindani, imekubali kichapo hicho na kubaki katika nafasi ya saba kwa pointi 21.

Pamoja na ushindi wa Ken Gold ambao ni wa pili katika msimu huu, wanabaki mkiani kwa pointi tisa baada ya michezo 19 na sasa watasafiri kuwafuata Tabora United.

Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Robert Matano amesema wanakubali matokeo kutokana na kuzidiwa na wapinzani akikiri vijana wake walicheza chini ya kiwango na kwamba uwanja haukuwa rafiki sana kuwaruhusu kuonyesha soka lao.

“Siyo nguvu kubwa ya mechi dhidi ya Simba, japo uchovu nao umechangia ila wamecheza chini ya kiwango na tumepata nafasi tumeshindwa kuzitumia,” amesema Matano.

Kocha Msaidizi wa Ken Gold, Omary Kapilima amesema ushindi huo licha ya kuwabakiza mkiani lakini ndio mwanzo wa kufufuka kutafuta kupanda katika nafasi za juu akieleza kuwa kila mechi ni fainali ya pointi.

“Kwa sasa tunaanza upya Ligi, hatutaki kupoteza wala kupata sare, tutaendelea kuwaandaa wachezaji kiakili na kisaikolojia kuhakikisha tunabaki Ligi Kuu na uwezekano upo,” amesema Kapilima.

Related Posts