Musoma. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa anayewakilisha mkoa wa Mara, Christopher Gachuma pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kemirembe Lwota wamepata ajali ya gari jana Februari 9, 2025 wakiwa njiani kwenda kumpokea Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira.
Akizungumza leo Jumatatu Februari 10, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amesema Lwota na Gachuma ambao walipata majeraha katika ajali hiyo walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa ajili ya matibabu.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi (aliyekaa kitandani) akimjulia hali, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa anayewakilisha mkoa wa Mara, Chrisopher Gachuma ambaye amelazwa katika hospitali ya Rufaa ya kanda Bugando baada ya kupata ajali wilayani Serengeti.
“Kwenye gari kulikuwa na watu watatu, Christopher Gachuma, Kemirembe Lwota pamoja na dereva wakitokea Mugumu kwenda Tarime kumpokea Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, wote walikimbizwa Bugando kwa usafiri wa ndege kutoka Fort Ikoma,” amesema.
Kamanda Lutumo amesema chanzo cha ajali hiyo ni gari aina ya Toyota Landcruiser V8 kuacha njia na kupinduka na kusababisha watatu ho kupata majeraha sehemu mbalimbali ya miili yao.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amesema majeruhi wote wanaendelea vizuri ingawa Mkuu wa Wilaya anasafirishwa usiku huu kwenda jijijni Dar es salam kwa matibabu zaidi, huku Gachuma akiruhusiwa.

“DC ataondoka usiku huu kwenda Dar es Salaam kwa matibabu zaidi ingawa kwa sasa hali yake sio mbaya,” amesema Mtambi
Wasira alikuwa na ziara katika wilaya sita za mkoa Mara ya ambapo pamoja na mambo mengine alifanya vikao na wanachama wa CCM katika wilaya hizo kabla ya kuendelea na ziara yake mkoani Simiyu.
Endelea kufuatilia Mwananchi.