Handeni. Serikali ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga imekabidhi kamera kwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa ajili ya kuzifunga barabarani kuanzia eneo la Mkata mpaka Segera ili kudhibiti matukio ya ajali za mara kwa mara.
Ndani ya siku 45 kati ya Desemba 2024 mpaka Januari 2025, watu zaidi ya 20 wamefariki dunia kwa ajali mbalimbali wilayani Handeni huku wengine wakijeruhiwa na kuachwa bila viungo sababu ya ajali ambapo nyingine zikidaiwa ni uzembe wa madereva.
Akizungumza wakati kukabidhi kamera hizo, Februari 9, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema jumla ya kamera 10, zitafungwa kwenye maeneo mbalimbali kwa nia ya kuthibiti ajali, kuzuia uhalifu na utoroshwaji mapato.
Amesema kwa hatua za awali zimepatikana kamera tatu na zitafungwa kuanzia eneo Tengwe, Kwekwale na Segera Chang’ombe, sehemu ambazo ndio hutokea ajali mara nyingi, hivyo polisi na kamati ya ulinzi na usalama wataweza kufuatilia matukio.
Lakini pia Msando amesema kamera nyingine zitafungwa kwenye vituo vya mabasi, minada na sehemu nyingine zenye mikusanyiko ili kudhibiti vurugu ambazo hutokea baina ya mawakala wa kampuni ya mabasi na wezi.
“Kamera hizi Jeshi la Polisi watazifunga maeneo mbalimbali kwenye wilaya yetu ya Handeni, maeneo haya ni Tengwe, Kwekwale, Kwangahu, Kwedikwazu na Segera Chang’ombe, Haya ni maeneo ambayo mara kwa mara zimekuwa zikitokea ajali,” amesema DC Msando.
Amesema vyanzo vya ajali mara nyingi huwa ni tofauti tofauti lakini vipo ambavyo kwa asilimia 70 mpaka 80 vinatokana na uzembe wa madereva, hivyo watafunga kamera hizo za kawaida na zile za siri ambazo zitaweza kuona mienendo ya watumiaji wote wa barabara ya kutoka Manga, Mkata na maeneo yote hadi kufika Segera.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Polisi Wilaya ya Handeni, George Elihaki amesema kamera hizo zitaweza kuwasaidia kufuatilia matukio yanayofanyika barabarani kwa ukaribu, pia kuweka ushahidi kwa wale madereva wanaovunja sheria.
Amesema kamera zitawasaidia kuwaona wanaovunja sheria za barabarani kwa makusudi, kwani mfumo uliopo unawawezesha kufuatilia kupitia simu za mkononi shughuli zote za barabarani kwa saa 24.
Mkuu wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, Willy Mwamasika, hivi karibuni, alisema licha ya juhudi hizo za wadau, wanaendelea na mchakato wa kuwapima kilevi madereva wanaopita barabara za Tanga, nia ikiwa ni kudhibiti ajali.
Ameiambia Mwananchi kwamba kwa Desemba, zaidi ya madereva 100 walikamatwa kwa makosa ya usalama barabarani na wapo waliofutiwa leseni, kutozwa faini na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.