Dodoma. Bunge limebaini hasara ya miaka mitatu mfululizo kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwamba inasababishwa na utaratibu wa ukodishaji kutoka Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA).
Ni kutokana na utaratibu huo, Bunge limetoa Azimio kuwa, hadi ifikapo Juni mwaka huu, Serikali ikamilishe mchakato wa kuhamisha ndege kutoka TGFA kwenda ATCL.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Oran Njeza ameliambia Bunge leo Jumatatu Februari10, 2025 wakati akisoma taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli za Kamati.
Lengo la mpango huo ni kulipunguzia shirika gharama za uendeshaji na kuweza kujitanua katika masoko ikiwemo kufika katika nchi ambazo kwa sasa haiwezi kufika.
Njeza ametaja changamoto ya Mizania ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuwa hasara hii inatokana na kuwa na madeni makubwa yanayosababishwa na utaratibu wa ukodishaji wa ndege kutoka TGFA.
“Hasara inayopatikana inaathiri mizania ya shirika na kushusha sifa nzuri ya shirika (credibility).
Mtaalamu wa masuala ya uchumi Dk Abed Kinyondo amesema hakuna ubaya kwa kufanya hivyo kwani ATCL ilikuwa imeng’olewa meno licha ya kuwa taasisi zote ni mali ya Serikali.
Dk Abed amesema lengo la kuhamisha mzigo wa madeni kutoka sehemu moja kwenda nyingine huwa ni kufanya ulinzi madhubuti wa kampuni, lakini inapofika wakati mnaona linaweza kujitegemea basi hakuna ubaya kurudisha umiliki wa kila kitu ikiwemo suala la makusanyo.
“Awali lengo lilikuwa ni ‘kuprotex’ (kulinda) kampuni ili kwamba hata kama kuna mtu alitaka kutaifisha ndege kutokana na madeni asiweze,lakini nako kuna hasara zake, shirika haliwezi kukopesheka kwa namna yoyote maana limenyang’anywa uwezo wake,” amesema Dk Kinyondo.
Kamati ya Bunge imesema jambo hilo hilo linahitaji kupatiwa ufumbuzi ili mtaji wa umma unaotumika uwe na tija na ufanisi na mizania ya vitabu vya shirika ikae sawa.
“Imebainika kuwa ATCL inakabiliwa na changamoto kubwa ya mizania ya hesabu zake kuwa vibaya, hali inayotokana na kuendelea kukodi ndege kutoka TGFA na kubebeshwa mzigo wa malipo ya matengenezo na ukodishaji,” imeeleza Kamati ya Bunge.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati hiyo, hali hiyo imesababisha hali ya fedha ya shirika kutoakisi uhalisia na kuvuruga uwezo wa shirika kukopa kwa ajili ya kuendelea kibiashara.
Kamati ilipendekeza Serikali kufanya mchakato wa kufuta madeni ya TGFA kwa ATCL kwa lengo la kuweka sawa mizania ya vitabu vya shirika jambo ambalo lilikubarika na likapitisha.
Karika taarifa yake, Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) alisema Kampuni ya Ndege imeendelea kupata hasara kwa kipindi cha miaka sita mfululizo.
Katika Taarifa ya CAG ilionyesha mwaka wa fedha 2022/23 ATCL ilipata hasara ya Sh56.64 bilioni huku mwaka wa fedha 2023/24 ikipata hasara ya Sh53.23 bilioni.
Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imetaja kuwa kukosekana kwa Mawasilinao ya Barabara katika Stesheni za Mizigo kwenye Reli ya Kisasa (SGR) unapunguza tija na lengo lililokusudiwa la ujenzi wa reli hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Hole ametoa taarifa ya kamati hiyo mbele ya Bunge akisema mradi wa uwekezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa umekusudia kuchochea uchumi kwa kuharakisha huduma za usafirishaji hususani wa bidhaa ambapo reli hiyo inakusudia kuunganisha na kuongeza ufanisi na tija ya njia nyingine za usafirishaji, matharani njia ya barabara na maji.
“Mheshimiwa mwenyekiti, uchambuzi wa Kamati umeabini, kuwa baadhi ya maeneo yaliyosanifiwa na kujengwa stesheni za mizigo yanakabiliwa na ukosefu wa barabara zinazounganisha stesheni hizo na barabara kuu hali inayoweza kuathiri usafirishaji wa bidhaa,” amesema Hole.
Amesema kutokana na mtaji mkubwa uliowekezwa katika SGR linategemea takribani asilimia 90 kutokana na usafirishaji wa mizigo na kwamba usafirishaji huo unategemea muunganiko wa reli na barabara.
Katika Azimio la Bunge, wabunge kwa kauli moja waliazimia kwamba, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) iweke miundombinu wezeshi kwa maeneo yote yenye stesheni za mizigo kwa ajili ya kufanikisha mawasiliano ya stesheni hizo na Barabara za kusafirisha mizigo pindi inapofika.
Akizungumzia suala la utalii, amesema kuwa imekuwa ikifanya vizuri kwa upate wa mapato yatokanayo na shughuli za utalii ambayo yamepelekea kuimarika kwa urari wa kibiashara na huduma za nje.
Kamati imetaja kuwa, taasisi za uhifadhi wa wanyamapori zinajiendesha kwa misingi ya kibiashara lakini utaratibu wa utolewaji wa fedha kama ilivyo kwa Wizara au Idara za Serikali umekuwa ukiathiri utendaji kazi wake.
“Kwa hiyo basi, Kamati inaazimia kwamba Serikali kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2025 kufanya mabadiliko ya kurejesha utaratibu wa Taasisi hizi kukusanya na kutumia mapato yake kulingana na bajeti zilizoidhinishwa.
Wabunge wametaja vifungu vinavyotakiwa kufanyiwa mabadiliko ni Kifungu cha 9 cha Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura ya 282, Kifungu cha 12(2) cha Sheria ya Mamlaka ya
Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro Sura ya 284 pamoja na Jedwali la kwanza la Sheria ya Mamlaka ya Mapato Sura ya 399.
Wamesema marekebisho hayo yaende sambamba na kuondoa Sheria hizo kwenye jedwali la kwanza la Sheria ya Mamlaka ya Mapato Sura ya 399 kwa madai kuwa,hatua hiyo itasaidia Taasisi na Mamlaka hizo
kutumia mapato yake ikiwemo kuimarisha miundombinu ya msingi katika hifadhi ili kuvutia watalii wengi zaidi.
Mbunge Shamsi Vuai Nahodha ameliambia kuwa, njia nzuri ya kufanikisha mipango yote siyo kulegeza masharti kwenye makusanyo bali ni kuweka utaratibu wa makusanyo kuwa katika mfuko mmoja.
Nahodha amesema ziko kelele kuwa Tanzania imekuwa na utitiri wa kodi wakati siyo kweli isipokuwa utaratibu wa ukusanyaji ndiyo unakuwa na malalamiko.
Mbunge wa Vunjo, Charles Kimei amesema kuwa riba za mikopo zinapaswa kuangaliwa upya ili ziweze kuendana na halihalisi ya sasa na usimamizi madhubuti wa makusanyo uendane na elimu nzuri kwa watu.
Kwenye mchango wake, Joseph Kandege amesema kuna haja ya kuangalia sheria zinazohusiana na makusanyo ya kodi ziangaliwe ili ziwe rafiki na kwamba zisipoangaliwa kwa ujumla wake, wananchi watalilalamikia bunge.
Hata hivyo mbunge huyo amezungumzia kauli za Serikali kwa wabunge wanapotoa maoni yao lakini wanaambiwa kuwa wakitoa maoni kwenye eneo moja la kuondoa kifungu, basi wapeleke mapendekezo kwamba kodi hiyo itapatikana kwa mlango upi jambo alilosema siyo sahihi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Dk Joseph Mhagama amewahoji wabunge kuhusu Taarifa hizo na mapendekezo ya Kamati na wabunge walipitisha kuwa Maazimio ya Bunge.