Moshi. Licha ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuridhia kwa kishindo, kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee wa chama hicho kwa nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu, kuna makada wameonekana kutoridhika na uamuzi huo wa kidemokrasia.
Zipo taarifa kuwa baadhi ya makada wa CCM waliokuwa wakijipanga kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2030, hawakufurahia uamuzi huo wakiamini unawaweka kwenye mazingira magumu hapo baadaye.
Miongoni mwa makada wa CCM ambao wamekuwa na mtazamo tofauti na kupinga uamuzi huo wa Mkutano Mkuu, yumo Dk Godfrey Malisa ambaye yeye amejitokeza hadharani na kutangaza kupinga uamuzi huo mahakamani, akidai katiba ya CCM imekiukwa na kwamba Rais Samia alipaswa kushindanishwa
Rais Samia alipitishwa kuwania nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 ya kura za ndio katika Mkutano Mkuu uliofanyika Januari 19, 2025 jijini Dodoma, ambao pia ulibariki Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (SMZ), Dk Hussein Mwinyi kuwa mgombea urais wa Zanzibar.
Pia, kwenye mkutano huo Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi aliteuliwa kuwa mgombea mwenza, uamuzi ambao ulipokewa kwa furaha na wanachama kutokana na historia yake ndani ya chama hicho na Serikali.
Hatua ya kada huyo kupinga uamuzi huo wa mkutano mkuu, ukailazimu Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro kukutana kumjadili na kufikia uamuzi wa kumvua uanachama.
Kilichomkuta Malisa kinafanana na kile kilichowahi kutokea kwa makada wengine akiwemo marehemu Bernard Membe, ambaye alifukuzwa CCM baada ya kutaka kugombea urais dhidi ya Rais John Magufuli mwaka 2020.
Hali kama hiyo pia ilitokea kwa Bhoke Munanka mwaka 2000 na Dk Mohamed Gharib Bilal mwaka 2005; wote wakiwa na nia ya kugombea urais ndani ya CCM, huku marais waliokuwa madarakani wakiwa wameongoza kwa kipindi kimoja.
Kwa muda mrefu ndani ya CCM kumekuwepo na utamaduni wa rais aliyepo madarakani katika kipindi chake cha kwanza, kupewa nafasi ya kugombea muhula wa pili.
Hata hivyo, Dk Bilal na Munamka hawakufukuzwa ndani ya CCM kama ilivyokuwa kwa wengine baada ya kukataliwa azma yao hiyo.
Akitangaza uamuzi wa kikao cha Halmashauri Kuu ya chama Mkoa, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel, alisema kada huyo amefukuzwa uanachama kuanzia jana.
“Leo (jana) tulikuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro ambacho pamoja na mambo mengine kimemfukuza Dk Godfrey Malisa aliyekuwa mwanachama wa CCM.
“Malisa amefukuzwa kwenye chama kwa kukosa sifa za za kuendelea kuwa mwanachama wa CCM kutokana na kwamba, amekuwa mara kwa mara akibeza uamuzi halali uliofanywa na mkutano mkuu wa CCM wa Januari 19, 2025 jijini Dodoma,’’alisema na kuongeza:
“Baada ya mkutano ule Dk Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na katika nchi yetu.
“Malisa ameenda mbali na kusema mkutano ule mkuu umevunja katiba ya CCM. Kwa mujibu wa kanuni za maadili ya chama chetu kifungu cha 6 kifungu kidogo cha tatu (b) kinasema mwanachama atakayekataa maamuzi halali ya chama, atakuwa ametenda kosa la utovu wa nidhamu na ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni.
Akinukuu zaidi katiba hiyo, alisema: “Kifungu kidogo cha tatu (C) kinasema mwanachama yeyote atakayekataa kumuunga mkono mgombea wa CCM aliyeteuliwa na kikao halali cha chama na kuthubutu kufanya kampeni za siri au za wazi kumhujumu, atakuwa ametenda kosa la usaliti na atastahili adhabu ya kufukuzwa uanachama.’’
Ni kwa sababu hiyo alisema kwa mujibu wa katiba ya CCM ambayo ndiyo sheria mama ya chama, ibara ya 89 kifungu kidogo cha nne kinaelekeza waziwazi kuwa amekosa sifa za uanachama.
Alisema kutokana na hali hiyo, kikao hicho kimetimiza matakwa ya katiba ya kumfukuza kama msaliti, ambaye amekuwa akipingana na maamuzi halali ya kikao kikubwa kuliko vyote ndani ya chama.
“Malisa anajiita ni mwanachama mwandamizi wa CCM, sasa halmashauri kuu inasema siyo kweli kwani alijiunga na CCM mwaka 2020 na muda wote tulikuwa tunamlea, lakini amekuwa akikiuka kanuni na taratibu za chama,” alisema.
Dk Malisa alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema hawezi kusema chochote kwa kuwa hajapata taarifa za kufukuzwa kwake.
“Siwezi kuzungumza wala kutoa maoni yoyote kuhusiana na hilo kwa sababu sijaambiwa rasmi. Hakuna mtu yeyote aliyefanya mawasiliano na mimi kutoka kwenye chama, hivyo siwezi kusema lolote, hayo nachukulia kama maneno ya mtaani.
“Sijaambiwa nimefukuzwa hivyo siwezi kusema chochote, na siwezi kujibu maswali kuhusu hili kwa sababu hiyo iliyo dhahiri, na wakati mwafaka ukifika nitawaambia tulizungumze,” alisema Dk Malisa.
Dk Malisa alijitokeza kwenye siasa kwa mara ya kwanza mwaka 2010 alipogombea ubunge Moshi Mjini kupitia chama cha Tanzania Labour Party (TLP), mwaka 2015, aligombea urais kupitia Chama cha Kijamii (CCK) na baadaye aligombea Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCK.
Mwaka 2018, Dk Malisa aligombea ubunge wa jimbo la Kinondoni kupitia TLP na mwaka 2020 aligombea ubunge Moshi Mjini kupitia NCCR-Mageuzi na baada ya uchaguzi huo akajiunga na CCM.
Mwaka 2022 Malisa alijitosa kuchukua fomu na kuwa miongoni mwa makada tisa waliochukua fomu kugombea uenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Matukio ya aina hiyo siku za nyuma
Bhoke Munanka, aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais akishughulika usalama, mwaka 2000 alitangaza kuchukua fomu ndani ya CCM kuomba kuteuliwa kugombea urais, lakini alikataliwa kwa kuwa Rais aliyekuwa madarakani Benjamin Mkapa alikuwa anagombea muhula wake wa pili.
Munanka, ambaye historia yake ni mfanyabishara mkubwa Kanda ya Ziwa, mwaka 1956 alianzisha Kampuni iitwayo Lake Province African General Trading Company (LAPACO).
Kisiasa Munamka alikuwa mwenyekiti wa TANU, ambaye pamoja na kushiriki kupigania uhuru pia alikuwa rafiki wa karibu wa hayati Mwalimu Julius Nyerere. Mbali na uwaziri pia aliwahi kuwa balozi wa Tanzania katika mataifa kadhaa yakiwamo Ethiopia na China.
Dk Mohamed Gharib Bilal, ambaye mwaka 2000 aligombea urais wa Zanzibar, jina lake lilikatwa lakini akaomba tena mwaka 2005, wakati rais aliyekuwa madarakani Amani Abeid Karume akiwa anagombea muhula wake wa pili.
Uamuzi huo wa Dk Bilal ulionekana ni kama kukiuka utaratibu unaotambulika ndani ya CCM wa kumwachia rais aliyepo madarakani kumaliza kipindi chake cha pili cha miaka mitano.
Kamati Kuu ya CCM Zanzibar ilimuomba Dk Bilal aliondoshe jina lake ili kumpa heshima rais aliyepo madarakani amalize ngwe yake.
Dk Bilal alikataa na kusema kuwa uamuzi wa kuondoshwa jina lake ni vema ukafanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na ndipo majina mawili; lake na la Rais Karume yalipelekwa Dodoma.
Huko nako Dk Bilal alishauriwa ajitoe kwa kuheshimu utaratibu wa chama na hatimaye akakubali.