Kero ya wavuta skanka, bangi kwa wanafunzi shule za Geita

Geita. Baraza la Madiwani Manispaa ya Geita limekerwa na vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na vikundi vya vijana wahalifu kujificha eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji Kata ya Bombambili kuvuta bangi na skanka na kuhatarisha usalama wa wanafunzi wa shule zilizopo kwenye maeneo hayo.

Kutokana na hali hiyo, baraza hilo limeiomba kamati ya ulinzi na usalama Wilaya kuingilia kati na kuwakamata vijana hao, ili wachukuliwe hatua za kisheria kabla hawajasababisha madhara zaidi.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya madiwani wakati wa kikao cha Baraza hilo kilichofanyika leo Jumatatu, Februari 10, 2025.

Diwani wa Bombambili, Leornad Bugomola amesema vipo vikundi vya uhalifu vinavyojificha kwenye maeneo hayo wakivuta bangi na skanka na sasa wapo baadhi ya wanafunzi wanaotoroka na kwenda kujumuika nao.

“Mwenyekiti tufike mahali tukubaliane watoto wengi wanaotusumbua ni wale wanaotoka kwenye Kata ya Kalangalala, ni vizuri wanapopanga shule kwa kuwa kila kata ila shule,  basi wanafunzi wawe wanapangwa kwenye maeneo ya kata zao ili kuondoa usumbufu,” amesema Bugomola.

“Mfano huku Bombambili hata eneo ambalo wakazi wake hawana watoto lakini hawa wanaotoka Kalangalala ndio wanaleta madhara, tunapata shida sana tunashindwa kufanya shughuli tunalinda maeneo nyuma ya hoteli wanakaa wanavuta bangi na skanka tuone namna ya kukomesha hili,” amesema Bugomola.

Diwani wa viti maalumu kutoka Kata ya Kalangalala, Zaituni Fundikira amesema changamoto kubwa ni ongezeko la watoto wa mtaani ambao, kwani  licha ya kukamatwa mara kwa mara na kurudishwa kwao baada ya muda mfupi hurudi na kuendelea na maisha Geita.

“Mwenyekiti naomba kama inawezekana wajengewe kituo maalumu wapatiwe elimu maana hawa watoto wanaleta athari kwenye jamii. Kwa mfano, juzi wapo waliokamatwa na mlinzi lakini wenzao walikuja na kumshambulia mlinzi kwa mawe na chupa na kuwaokoa waliokamatwa hii ni hatari mwenyekiti,” amesema Fundikira.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita, Barnabas Mapande amesema hali ya usalama inatia shaka katika Wilaya hiyo ikiwemo eneo la Bugulula kwenda Geita Mjini ambapo vibaka wamekuwa wakiwakamata bodaboda na waendesha baiskeli na kuwapora,  lakini pia majira ya jioni huvamia kinamama wanaofanya biashara ya samaki na kuwapora.

Amesema changamoto nyingine ni wizi wa mifugo ambapo wezi wanaingia kwenye zizi na kwenda kuchinja na kuuza maeneo mengine,  ikiwemo kwenye mabucha na kulitaka baraza hilo kuangalia wizi huo hasa kwenye mifugo ambayo haichinjwi kwenye machinjio rasmi.

Baadhi ya madiwani wa Manispaa ya Geita wakiwa kwenye kikao cha baraza hilo cha robo ya pili ya mwaka kinachofanyika kwenye  ukumbi wa EPZ Geita.

“Lazima tuliangalie hili na kujiuliza hawa ng’ombe wanaochinjwa nyama inapelekwa wapi ni mabucha gani yanauza, hii mifugo inayoibiwa na kuchinjwa nje ya machinjio zetu inapelekwa wapi? Mkurugenzi sisi na vyombo vyetu na watu wetu wanaohakiki nyama fuatilieni hili tukifanikiwa hapa tutakuwa tumekomesha wizi wa mifugo”amesema

Mwakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Janeth Mobe amesema kumekuwa na matukio mengi ya uhalifu na wao wamekuwa wakifanya operesheni mara kwa mara kuhakikisha mji unakuwa salama.

“Ni kweli yapo matukio ya uhalifu na tunashirikiana na polisi kuhakikisha wahalifu wanakamatwa. Wilaya ni kubwa na changamoto iliyopo ni upungufu wa magari kwa jeshi letu, jambo hili limejadiliwa na tayari polisi wamepewa maelekezo na hili tunalichukua kwa dharura zaidi ili kudhibiti wanafunzi wetu wasiingie kwenye matendo haya maovu,” amesema Mobe.

Related Posts