Dodoma. Wabunge wanne wa Tanzania wameliamsha tena bungeni wakitaka Serikali iangalie upya kikokotoo cha mafao ya kustaafu kwa kuwa bado kuna malalamiko huku wengine wakisema kiwango cha pensheni cha kila mwezi hakilingani na gharama za maisha.
Kilio cha kikotoo kimekuwa kisikika kwa nyakati tofauti bungeni tangu Julai 1, 2022, Serikali ilivyotangaza matumizi ya kanuni mpya za kikotoo cha mafao ya mkupuo kwa wastaafu kuwa ni asilimia 33 kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii.
Hata hivyo, baada ya malalamiko hayo yalikuwa yakisikika nje ya Bunge pia, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akisoma bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25, alitangaza ongezeko hilo kutoka asilimia 33 hadi 40 kwa wale waliokuwa wakilipwa asilimia 50.
Katika ongezeko hilo pia Serikali ilitangaza watumishi waliostaafu kuanzia Julai 2022 ambao ni 17,068 watalipwa mapunjo ya mafao ya mkupuo kulingana na kikokotoo kilichotangazwa Juni 13, 2024.
Hata hivyo, leo Jumatatu, Februari 10, 2025 suala hilo limeibuka kwa mara nyingine wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni.
Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi amesema wanatambua kumekuwa na ongezeko la pensheni kwa wastaafu.
Amehoji iwapo Serikali iko tayari kufanya tathimini ya kina kwa kuangalia uhimilivu wa mifuko na kuangalia na hali ya maisha ili kuona kuwaongozea kwa sababu Sh150,000 bado ni kiwango kidogo.
“Lakini kumekuwa Serikali kufanya ufuatiliaji wa watumishi wastaafu kwa kuangalia kama wako hai ama wamefariki dunia lakini kwa bahati mbaya sana wastaafu wengi ni wagonjwa,” amesema.
“Mara nyingi zoezi hilo linafanyika katika ngazi ya mkoa hamuoni kwadhulumu hawa wafanyakazi ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu na haioni kuna haja ya kuwafuata waliko kufanya tathimini,” amehoji.
Akijibu maswali hayo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ameahidi kuwa Serikali wanaendelea kufanya tathimini lakini kigezo kikubwa ni ustahimilivu wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Utaratibu wa sasa ni utaratibu ambao unashirikisha hadi ngazi ya chini, kupitia ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya tumeweka utaratibu ambao tarifa za mstaafu mmoja mmoja katika eneo analoishi tunazipata na tunazifanyia kazi,” amesema.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Christina Mzava amesema kuna baadhi ya wastaafu walilipwa kwa kiwango cha zamani cha mafao ya mkupuo na wengine bado hawajalipwa fidia (ongezeko) na kuhoji kauli ya Serikali kuhusiana na suala hilo.
Akijibu swali hilo, Kikwete ameomba watu wenye madai kutokana na kikokotoo, wawasilishe katika ofisi yao ili wafanyie kazi na kwamba ongezeko hilo linaonyesha uchumi wa nchi unakwenda vizuri.
“Kitendo hicho kinaonyesha mheshimiwa Rais yuko tayari kusaidia wale wote wenye mahitaji na wana matatizo katika maeneo hayo. Kama kuna watu wenye malalamiko yoyote basi ofisi yangu iko tayari kupokea malalamiko hayo na kuyafanyia kazi,”amesema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda amesema ni kweli kiwango cha Sh150,000 cha pensheni lakini gharama za maisha zimeongezeka, hivyo kiwango hicho hakiwezi kumtosha.
“Serikali haioni kuna haja ya kuongeza fedha ili hata ifike Sh600,000 ili kumsaidia mzee huyu aliyeitumikia Taifa kwa muda mrefu,” amehoji.
Akijibu swali hilo, Ridhiwan amesema malipo ya kikokotoo yanategemea vigezo vingi ikiwemo hali ya kiuchumu, ustahimilivu wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Tunatamani sana kama na uwezo huo mkubwa tuweze hata kulipa Sh1 milioni lakini hapa tulipo ya Sh100,000 hadi Sh150,000 ni sehemu ya hayo makubwa yanayofanyika akiwemo na mambo mengine yanayoambatana na hayo,” amesema.
Katika swali la msingi la Mbunge wa Mbogwe (CCM), Nicodemas Maganga amehoji ni lini Serikali itafanya mabadiliko kwenye kikokotoo cha watumishi nchini kwa kuwa malalamiko yamekuwa mengi.
Akijibu swali hilo, Ridhiwan amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/23 Serikali ilifanya mabadiliko ya Kikokotoo kwa watumishi nchini na mwaka 2024/25 imefanya maboresho zaidi kwenye kikokotoo hicho baada ya mjadala ndani ya Bunge.
Ameyataja maboresho hayo ni kuboresha malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40 kwa waliokuwa wanalipwa asilimia 50, na kutoka asilimia 33 hadi 35.
“Januari 2025, Serikali imeongeza kima cha chini cha pensheni kutoka Sh100,000 hadi Sh150,000 kwa mwezi. Vilevile, Serikali imehuisha (indexation) pensheni ya kila mwezi kwa kiwango cha asilimia mbili kwa kuzingatia sheria na Kanuni zilizopo,” amesema.
Amesema pamoja na hilo, Ridhiwan amesema Serikali itaendelea kufanya tathimini ya kupima uhimilivu wa Mifuko kila baada ya miaka mitatu kama inavyoelekezwa kisheria ili kuangalia uwezo wa kuboresha mafao bila kuathiri uendelevu wake.