Kitendawili cha elimu, malezi ndani ya zama za dijitali

Siha.Teknolojia imeleta mapinduzi makubwa katika maeneo mbalimbali, likiwamo eneo la  makuzi na malezi ya watoto.

Unapozungumzia makuzi na malezi ya watoto katika zama hizi za utandawazi, unabaki na maswali mengi kwa wazazi na walezi,  huku kila mmoja akitafakari ni namna gani anaweza kuushinda mtihani huo katikati ya mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia.

Mtihani huo ndio uliomsukuma Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Dk Haji Mnasi kuandika kitabu  akiangazia elimu na malezi kwa watoto katika zama za kidijitali.

Kitabu hicho kimesheheni mambo mbalimbali yanayolenga kuonyesha  namna ya kuandaa kizazi kipya kwa maisha ya kidijitali.

Akizungumza na Mwananchi,  Dk Mnasi amesema kitabu hicho kimebeba suluhisho la malezi bora na makuzi ya watoto kipindi hiki cha utandawazi.

 Kilichomsukuma kuandika kitabu hicho

Dk Mnasi ambaye kitaaluma ni mwalimu anaeleza kuwa changamoto zinazoikabili jamii kwa sasa katika malezi na makuzi ya watoto,  ni moja ya kichocheo kikubwa kilichomfanya aandike kitabu hicho.

Anasema akiwa mwalimu amepita ngazi mbalimbali za ufundishaji kuanzia awali na hata kuwa kiongozi katika idara ya elimu ikiwemo ofisa elimu wa wilaya, hivyo anazifahamu vyema changamoto wanazopitia wazazi na walezi kwenye malezi ya watoto.

“Nikiwa  mwalimu niliyepitia ngazi mbalimbali, kufundisha na hata kuwa  ofisa elimu wilaya, nilijifunza mambo mengi hasa suala nzima la ufundishaji na ujifunzaji  sambamba na malezi ya watoto,’’ anasema.

Anaeleza kuwa katika uzoefu wake huo kwenye malezi ya watoto,  akiwa  mwalimu na mzazi, amebaini uwepo wa changamoto kubwa kwenye malezi inayotokana na maendeleo makubwa ya teknolojia.

 ” Watoto kwa sasa siyo wageni tena kwenye kushika na kuitumia simu na vifaa vingine vya teknolojia kama vile tabiti,  vishkwambi, kompyuta na runinga, hivi vitu sasa vimekuwa ni vya kawaida sana kwa watoto wa mjini na hata vijijini”.

“Kwa hiyo changamoto hii kwa sasa ni kubwa hasa kwenye suala la malezi, tunajiuliza sasa hawa watoto inakuwaje, tamaduni za zamani na zile njia za kujifunza wakati ule hazipo, tupo   zama za teknolojia,’’ anaeleza na kuongeza:

“Ndipo nikaja na hiki kitabu ambacho kina suluhisho la namna ya kukabiliana na changamoto za malezi na makuzi ya watoto bila kuathiri utandawazi na tamaduni”.

Anasema kupitia kitabu hicho anahitaji watoto waweze kupata malezi na maarifa ambayo yatasaidia katika kuzienzi falsafa mbalimbali ikiwemo iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya 4R.

“Katika kipindi hiki cha teknolojia, watoto hawa wanawezaje kuzienzi, kuziishi na kuzitumia zile 4R. Lakini nikiwa  mwalimu na mzazi,  ninaona changamoto ya malezi inavyoitesa jamii kwa sasa nikaona nitumie muda mchache nilio nao, niandike kitabu hiki kuleta suluhisho ili na mimi nisaidie jamii  hasa kipindi hiki ambacho tumeona kuna uboreshaji na mabadiliko ya mitalaa mbalimbali ya elimu,’’ anabainisha.

Akizungumzia muda aliotumia kuandika kitabu hicho, Dk Mnasi anasema ilimchukua muda wa zaidi ya miezi sita kukiandika na kukikamilisha.

“Uandishi wa kitabu hiki ulikuwa mgumu sana kutokana na muda nilionao na majukumu yangu kama mkurugenzi wa halmashauri…’’ anasema.

Anasema kitabu hicho ni toleo la kwanza na kwamba ana matarajio ya kutoa toleo la pili na hata kuvitafsiri kwa lugha ya Kiingereza, lengo likiwa kupanua wigo na kuwezesha kuwafikia watu wengi zaidi.

Dk Mnasi anasema anatarajia kitabu hicho  kilete mabadiliko chanya kuanzia kwa wazazi, walezi na wanafunzi wenyewe,  na kuwezesha malezi bora na sahihi katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia.

“Ninatarajia pia kitabu hiki kitaimarisha malezi ili yaendane na zama hizi za utandawazi na teknolojia. Hiki kitabu kina majibu ya changamoto za malezi na makuzi, wazazi, walezi na wanafunzi hawapaswi kukikosa” anaeleza Dk Mnasi.

Anaongeza: “Kitabu hiki ni mchango wangu kwa jamii hivyo watu wanaokihitaji watachangia Sh10,000 lakini pia niko kwenye mpango wa kuona ni namna gani kinaweza kuwekwa kwenye mfumo wa dijitali, ili kuwezesha kuwafikia watu wengi zaidi na kufanikisha malengo ya  kuandaa kizazi kipya kwa maisha ya kidijitali”.

Dk Mnasi anasema katika kitabu hicho msomaji atakutana na maarifa mbalimbali ikiwemo nafasi ya wazazi katika malezi ya kidijitali na hilo amelichambua na kulielezea  kwa mapana.

Anasema pia amezungumzia udhibiti wa matumizi ya teknolojia, changamoto zinazotokana na teknolojia pamoja na  mwelekeo wa wazazi katika matumizi ya teknolojia na malezi ya watoto.

“Haya ndiyo baadhi ya mambo ambayo yamedadavuliwa kwenye kitabu hiki kwa kina,  yakilenga kuimarisha malezi na kuzalisha kizazi bora cha sasa na baadaye”.

“Nimshukuru Mungu kwa kunipa fursa na maono makubwa ya kuweza kukiandika kitabu hiki. Kwangu mimi naona ni wakati mwafaka kuwa na kitabu hiki,  kutokana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia hasa katika suala la elimu na malezi,”anaeleza.

Related Posts