Abiria waliokuwa wakisafiri na ndege ya Shirika la EasyJet kutoka Misri kuelekea Manchester walijikuta katika kizaazaa kikubwa baada ya rubani wa ndege hiyo kuzimia ghafla wakati ndege ikiwa angani, tukio lililotokea jana, Jumamosi.
Kufuatia dharura hiyo, ilibidi msaidizi wa rubani, au First Officer kama anavyoitwa kitaalamu, aishushe ndege hiyo kwa dharura na hatimaye kufanikiwa kutua salama katika Uwanja wa Ndege wa Athens, ambako vikosi vya zimamoto, vikosi vya usalama, huduma ya kwanza, na Msalaba Mwekundu vilikuwa ‘standby’ endapo lolote lingetokea wakati wa kutua.
Abiria mmoja amenukuliwa na mtandao wa The Mirror akieleza kwamba hekaheka zilianzia ndani ya ndege baada ya abiria kushtukia wahudumu wa ndege wakikimbilia upande wa mbele aliko rubani.
“Tukiwa tumeshaanza kupanic, ndipo tulipotaarifiwa kwamba rubani alikuwa na dharura ya kiafya, wakauliza kama kuna madaktari miongoni mwetu abiria, watu kadhaa waliosomea udaktari wakasimama na kuelekea kwa rubani,” alisimulia abiria huyo.
Shirika la Ndege la EasyJet lilitoa ufafanuzi kuwa rubani wake alipata dharura ya kiafya akiwa angani, na hivyo msaidizi wake alibeba jukumu la kuishusha ndege hiyo kwa dharura, huku wakitoa radhi kwa abiria kwa usumbufu.
Baada ya kutua Athens, abiria walitafutiwa sehemu za kulala na chakula hadi leo, Jumapili, ambapo safari imeendelea.