Matengenezo Barabara ya Seronera, uwanja wa ndege yaanza

Serengeti. Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limeanza matengenezo makubwa ya barabara muhimu inayotumiwa na watalii kuanzia Seronera hadi Robo.

Aidha imeanza kukarabati uwanja wa ndege wa Seronera unaopokea idadi kubwa ya ndege kwa viwanja vilivyopo ndani ya Hufadhi za Taifa, lengo la maboresho likiwa ni kuboresha miundombinu ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Akizungumza jana Jumapili, Februari 9, 2025 wakati wa ukaguzi wa maboresho hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi Bodi ya Tanapa, Hadija Ramadhan amesema ukarabati huo utagharimu zaidi ya Sh1 bilioni.

Amesema wameridhika na kazi ya uboreshaji wa miundombinu hiyo na kuagiza kazi hiyo imalizike kwa wakati ili miundombinu katika hifadhi hiyo iweze kupitika katika msimu wote wa mwaka.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, Stephano Msumi amesema katika ukarabati huo zaidi ya Sh508.7 milioni ni kwa ajili ya miundombinu ya barabara huku Sh670 milioni zikitarajiwa kutumika kwa ajili ya Kiwanja cha Ndege cha Seronera.

“Lengo la maboresho haya ni kurahisisha huduma kwa watalii wanaoenda katika hifadhi barabara bora zitarahisisha safari na uwanja wa ndege utasaidia pia kwa wale wanaotumia ndege kufika Serengeti, maboresho haya yatasaidia  kuondoa malalamiko hasa kwa madereva wa utalii ambao wamekuwa wakilalamikia miundombinu ya barabara mibovu,” amesema.

Mmoja wa madereva wa magari ya utalii, Hussein Madafa amesema wamekuwa wakikumbana na adha kubwa hasa kipindi cha mvua kutokana na barabara nyingi kuharibika.

Amesema kipindi cha mvua kutokana na barabara nyingi kuathiriwa na mvua wamekuwa wakiteseka kusafirisha watalii kutokana na ubovu wa barabara.

“Tunashukuru kwa maboresho haya na tunaamini itatusaidia kuondoa adha ya ubovu wa barabara hasa msimu wa mvua,” amesema.

Kuhusu suluhu ya kudumu ya changamoto hiyo awali Machi 10, 2024 kutokana na mvua kubwa ziliokuwa zikinyesha, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Tanapa ilisema inaandaa andiko la kuomba kukarabati barabara hizo kwa kiwango cha zege na lami.

Aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi aliwaeleza waandishi wa habari Dodoma wanaomba kibali hicho Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), kwani hifadi za Taifa katika nchi mbalimbali duniani huwa zinapata hadhi maalumu ya kuorodheshwa kwenye urithi wa dunia ambayo inasimamiwa na Unesco.

Alieleza kutokana na uharibifu uliotokea kwenye hifadhi hiyo uliosababishwa na mvua za El Nino zilizoanza Oktoba 2023, andiko hilo la kuomba ukarabati wa barabara hizo kwa kutumia tabaka gumu, ili zidumu kwa muda mrefu.

Alisema barabara zilizopo ndani ya hifadhi hiyo zilijengwa kwa kutumia udongo na changarawe na zimetumika kwa zaidi ya miaka 65 sasa, hivyo wanataka kukarabati kwa kutumia tabaka gumu la zege au lami.

Related Posts