Matumaini mapya SGR ikitarajiwa kuanza usafirishaji wa mizigo

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) linatarajia kuanza usafirishaji wa mizigo kwa treni ya kisasa ya SGR Aprili 2025, baada ya kufanyika majaribio ya mfumo huo.

Hadi sasa, mabehewa 264 yaliyotengenezwa nchini China yamewasili katika Bandari ya Dar es Salaam tangu Desemba 24, 2024, yakisubiri kuanzishwa kwa usafiri wa treni ya umeme.

Kati ya mabehewa hayo, 200 yameundwa kwa ajili ya kubeba makontena, na 64 kubeba mizigo isiyofungwa (shehena kichele).

Akizungumza na Mwananchi leo, Februari 10, 2025, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa TRC, Fredy Mwanjala, amesema matarajio ya TRC ni kuanza rasmi usafirishaji wa mizigo baada ya miezi minne, akieleza kuwa majaribio ya treni hiyo yatafanyika kwanza ikiwa tupu, kisha ikiwa na mizigo.

“Matarajio yetu ni kuanza usafirishaji wa mizigo ndani ya miezi minne kuanzia Januari mwaka huu, baada ya mabehewa kupimwa na wataalamu pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra),” amesema.

Amesema usafirishaji utaanza mara baada ya majaribio, ambapo treni hiyo itatembea kwa kasi ya kilomita 120 kwa saa, mabehewa yakiwa tupu na kisha yakiwa yamebeba mizigo kabla ya kuanza rasmi shughuli ya usafirishaji.

“Kama nilivyosema, matarajio ya kuanza kuendesha usafiri huu ni ndani ya miezi minne. Matarajio haya ni kuanzia Januari mwaka huu,” amesema Mwanjala.

Amesema baada ya shughuli za majaribio, wataalamu wao pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) watajiridhisha kabla ya usafirishaji kuanza rasmi.

“Mabehewa hayo ni lazima yajaribiwe kwenye reli yenyewe kwanza. Wataalamu wakishajiridhisha kwamba yanaweza kutembea vizuri kwa kasi ya kilomita 120 kwa saa, ndipo yatapakizwa mizigo kwa majaribio zaidi.

Baada ya wataalamu kujiridhisha katika hatua hiyo, ndipo Latra watafanya kazi yao. Wakisharidhika, watatoa idhini ya kuanza rasmi usafirishaji wa mizigo. Michakato yote hii inakadiriwa kuchukua miezi minne,” amesema.

Matumaini ya Wafanyabiashara

Kuanza kwa usafiri huo kunatajwa na wafanyabiashara kuwa kutasaidia kupunguza muda na gharama kwa msafirishaji, mfanyabiashara hadi mlaji wa mwisho. Matamanio yao makubwa ni bei ya usafirishaji kuwa rafiki ili kuleta unafuu kwa mlaji wa mwisho.

Mbali na gharama, wameeleza kuwa usafiri huo utasaidia kupunguza muda wa usafirishaji na kusaidia barabara kudumu kwa kupunguza msongamano wa malori.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamis Livembe, amesema usafiri huo utawarahisishia kufikisha mizigo kwa muda mfupi, hasa kwa wafanyabiashara wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi.

“Ukianza, bidhaa zitapelekwa Dodoma badala ya Dar es Salaam, hivyo kupunguza muda wa kusafirisha mizigo,” amesema.

Amesema pamoja na kwamba gharama bado hazijajulikana, tumaini kubwa kwao ni lengo la kupunguza muda wa kusafirisha mizigo kutimia.

“Itasaidia pia kupunguza msongamano wa magari kwa kupunguza idadi ya malori barabarani,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Severine Mushi, amesema matumaini makubwa ni bei ya usafiri huo kuwa rafiki ikilinganishwa na bei za kusafirisha bidhaa kwa malori.

“Bei ikiwa rafiki, itawasaidia wafanyabiashara wengi kutumia usafiri huu ambao ni wa haraka zaidi, tofauti na lori ambako bidhaa zinaweza kuchukua siku nzima kuwasili na wakati mwingine hata siku inayofuata,” amesema.

“Kwenye SGR, bidhaa zinatumwa na kuletwa ndani ya saa chache. Mfano, oda ikishawekwa, bidhaa zinapakiwa, na zitaletwa kwa saa chache na kumfikia mtumiaji wa mwisho kwa muda mfupi,” amesema.

Mdau wa usafirishaji, Profesa Zacharia Mganilwa, hakutofautiana sana na watangulizi wake, akibainisha kuwa mbali na kupunguza gharama, muda na kumfikia mlaji wa mwisho kwa haraka, pia utasaidia barabara kudumu.

Profesa Mganilwa, aliyewahi kuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kabla ya kuhamishiwa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), amesema kuanza kwa usafiri huo kutafungua fursa za kiuchumi na kurahisisha maisha ya wananchi.

“Mfano ni saruji, Dar es Salaam inauzwa Sh 17,000, lakini saruji hiyo hiyo kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa ni Sh 23,000 hadi 25,000. Tukianza kusafirisha mizigo kwa SGR kwenye mikoa hiyo, bei itashuka,” amesema.

Amesema gharama ya usafirishaji ikiwa nafuu, hata mfanyabiashara akiuza kwa bei ya chini atapata faida yake, na mlaji ataipata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.

“Hata barabara zetu, ambazo zinajengwa kwa gharama kubwa, zitadumu muda mrefu kwa kupungua kwa idadi ya malori,” amesema.

Related Posts