Mbaroni akituhumiwa kuiba mtoto wa siku moja

Kahama. Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia mkazi wa Kata ya Mwakitolyo, Sai Charles (38) kwa tuhuma za kuiba mtoto wa siku moja.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 10, 2025 Kamanda wa Polisi mkoani humo, Janeth Magomi amesema mtoto huyo aliibiwa Februari 5, 2025 nyumbani wakati mama yake akiwa anaoga.

Magomi amesema mtuhumiwa alifanikiwa kumuiba mtoto huyo baada ya kujifanya ndugu wa karibu wa mama yake, Rachel Mathayo (19) kisha kufanya tukio hilo.

“Alijitokeza kwenye Zahanati ya Ngaya, Halmashauri ya Msalala, muda mfupi baada ya Rahel kujifungua akijifanya kuwa ni ndugu au rafiki wa karibu, Sai alijitolea kumsaidia Rahel na kujenga urafiki wa karibu na yeye.

“Baada ya Rahel kutoka hospitalini na kurudi nyumbani, mtuhumiwa alimsaidia na kumchukua mtoto na mama mzazi kumpeleka nyumbani kwao Bulige, saa 1:00 asubuhi Rahel alipokwenda kuoga bafuni aliporudi hakumuona mtoto na msaidizi hakuwepo ndipo alipogundua mtoto wake amepotea,” amesema Magomi.

Kamanda huyo ameeleza baada ya Rachel kugundua mtoto wake ameibwa, alipiga kelele na kuita msaada ambapo vijana wa bodaboda waliokuwa karibu walitoa taarifa kwa polisi, wakieleza mtuhumiwa alikuwa amepanda bodaboda akiwa na mtoto mdogo.

Amesema baada ya taarifa hiyo, jeshi hilo lilifanya msako wa haraka na kufanikiwa kumkamata Sai akiwa Kata ya Mwakitolyo na mtoto ambaye tayari amerudishwa kwa mama yake mzazi.

“Alikuwa na watoto wakubwa lakini alitaka kuwa na mtoto mwingine jambo ambalo haliwezekani ndiyo maana aliamua kumchukua mtoto wa mtu mwingine na kumfanya kuwa wake,” ameeleza Magomi.

Akiwashukuru waendesha bodaboda waliofanikisha mtoto huyo kupatikana, Kamanda Magomi amewataka wananchi hasa wanawake kuwa makini na watu wanaojitokeza kama ndugu au marafiki baada ya kujifungua.

“Wizi wa watoto siyo jambo dogo ni kosa kubwa la jinai tunawahimiza wananchi kuwa waangalifu na kuzingatia maadili ya kitanzania badala ya kutafuta watoto kwa njia zisizo halali,” amesema Magomi.

Related Posts