Ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya dunia ya sasa, elimu ya amali inatajwa kama mojawapo ya nyenzo muhimu za kuwaandaa Watanzania kuhimili vishindo vya mabadiliko hayo.
Ndio sababu Serikali ikalazimika kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, msukumo ukiwa kuwa na wahitimu wenye ujuzi wa aina mbalimbali kupitia mabadiliko ya elimu hiyo.
Hata hivyo, kwa baadhi ya watu akiwamo mdau maarufu wa elimu nchini, Benjamin Nkonya, mabadiliko ya mtalaa unaopogia chapuo mafunzo ya ujuzi wa aina mbalimbali, umeyaweka kando baadhi ya mafunzo muhimu, ukiwamo udereva wa wa vyombo vya moto kama pikipiki anaosema ungeingizwa katika mtalaa wa elimu ya msingi.

Nkonya ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya ubunifu katika elimu Tanzania (EIT), amezungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu akitoa ushauri wa masuala mbalimbali unaolenga kuboresha sekta ya elimu nchini. Endelea…
Swali: Hivi karibuni, tumezindua sera ya elimu 2014 iliyofanyiwa mapitio 2023, unadhani sera hiyo inaweza kututoa tulipo na kwenda kwenye mafanikio zaidi ya kielimu?
Jibu: Jibu ni ndio. Katika sera hiyo mimi ni miongoni mwa tulioshiriki kuiboresha mwaka 2014 tukiwa na Dk Kisangi kwa kuzunguka nchi nzima kufanya upatikanaji wake.
Ile sera ilisema mwanafunzi anapomaliza elimu yake ya lazima yupo huru kwenda kwenye elimu ya mafunzo au kwenda kwenye elimu nyingine kama kidato cha tano.
Lakini haikutekelezwa mpaka baadaye mwaka 2021 ndio likatoka tena hilo wazo, nikachukuliwa tena kuwa miongoni mwa wataalamu wa kukusanya maoni na kuboresha sera hiyo kazi tuliyoifanya 2022 na 2023 na baadaye ikatangazwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Pamoja na kuwepo kwa elimu ya darasa la kwanza hadi chuo kikuu, elimu ya amali ni muhimu kwa sababu ndio maisha ya Watanzania wengi yako huko, yaani asilimia 85 ya watanzania wako katika sekta isiyo rasmi na asilimia 15 ndio wapo kwenye sekta rasmi.
Hivyo kama kuna mtu anajua ufundi wa kuchomelea ataendelea huko, kama anajua kuendesha chombo cha moto ataenda huko.
Lakini licha nia nzuri hiyo ya Serikali kuja na sera iliyoboreshwa, tatizo naliona lipo kwenye utekelezaji na kubwa ni pale tunapokuwa na aina 27 za mafunzo ya amali ambazo ndio zimeingizwa kwenye ufundishaji kwa shule za kawaida. Kuna nyingine ni muhimu lakini zimeachwa.
Swali: Tupe mifano ya mafunzo unayodhani ni muhimu lakini yameachwa?
Jibu: Nikupe mifano. Mkoa wa Dar es Salaam umezungukwa na maji, vilevile Mkoa wa Mwanza ambao una visiwa na kwa ujumla Tanzania nzima imezungukwa na maziwa kwa hiyo kuna samaki wengi wanaochagiza shughuli nyingi za uchumi wa bluu lakini ajabu mafunzo ya uvuvi hayapo katika orodha ya masomo 27 ya elimu ya amali.
Pia kuna mafunzo kama ya udereva. Mtu ukimwambia udereva, anadhani ni kuendesha gari tu. Inatakiwa mtoto kwa mfano watoto wafundishwe kuendesha bodaboda ambayo ni ajira kubwa kwa vijana sasa.
Leo mtu anamaliza kidato cha nne, anamaliza kidato cha sita, chuo kikuu, hajui kuendesha chombo chochote cha moto.Baadaye mtu huyohuyo anapomaliza shule anaingia kwenye bodaboda na kusababisha ajali wakati angefundishwa haya akiwa shuleni, angeheshimu kazi hiyo na pia kuchukua tahadhari zote za usalama barabarani.
Swali:Kwa mtazamo wako nini kinakwamisha maendeleo ya sekta ya elimu kwa jumla?
Jibu:Sekta ya elimu inakwamishwa na mambo mawili, la kwanza mfumo wa ugharamiaji elimu.Hapa tuige nchi kama Colombia, Uholanzi na Sri lanka ambazo wao wanachofanya bajeti ya serikali inatengenezwa kwa ujumla wake halafu wanagawa kwa idadi ya wanafunzi halafu mzazi anapewa vocha ya kumpeleka mtoto wake shule yoyote anayoona inafaa.
“Kwa utaratibu huu, mzazi atampeleka mtoto shule yenye ufaulu mzuri, matokeo yake watoa huduma ya elimu watashindana katika gharama na ubora wa elimu na kwa kufanya hivyo kunapunguza kazi ya kuweka wadhibiti ubora kwa kuwa mzazi mwenyewe anasimamia ubora wa elimu anayopewa mtoto wake kupitia vocha anayopewa.
Sio hapa kwetu mzazi unaambiwa tu umpeleke mtoto wako shule kwani hakuna ada, lakini mzazi huyo hawezi kufanya ufuatiliaji kama mwalimu amefundisha au la.
Changamoto ya pili ni dhana iliyopo kuwa maisha ni elimu na kutaka kuwafanya wanafunzi wote waende kwenye maisha ya kusoma.
Matokeo ya haya ni kwamba unakuta shule haina maabara, haina walimu wala miundombinu. Darasani wanakaa watoto hadi 200, ilimradi tu waonekane wameenda shule.
Nashauri turudi enzi za Mwalimu Nyerere miaka ya 1970 hadi 19810, shule zilikuwa shule na vitu vyote ambavyo vimetajwa na sheria ya elimu.
Swali: Unadhani ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kwenye elimu ni imara na pande zote zinafurahia ushirikiano huo?
Jibu: Naona bado upo hafifu kwani hata sheria ya elimu inavyoelekeza haitekelezwi. Kwa mfano, Sheria ya Elimu kifungu cha pili kinazungumzia katibu mkuu wa elimu ambaye anateuliwa na waziri, kazi yake ni kusimamia au kuratibu shuguli zote ambazo zinatokea kwenye shule ambazo sio za Serikali.
Maana yake ni kwamba sekta binafsi inatakiwa iratibiwe na katibu mkuu aliyeteuliwa na waziri.
Ushirikiano huo ungekuwa unapatikana haya yanayoonekana leo yasingekuwepo kwani tumegeuka washindani kwa Serikali yaani utadhani ni mtu na mke mwenza.
Pia kifungu cha sita na cha saba cha sheria ya elimu, kimesema kuwepo na baraza la ushauri la elimu, baraza ambalo liliwepo wakati wa Joseph Mungai akiwa Waziri wa Elimu, na kanuni zilitungwa na tukawa tunaenda kwenye vikao.
Hata hivyo, miaka ya 2000 hadi 2003 baraza hilo likafutwa, hivyo unakuta sekta binafasi kupeleka hoja zake wizarani inakuwa ni kazi ngumu mpaka umbembeleze waziri, ajisikie ndio aje kutusikiliza.
Pia kwa bahati mbaya sekta hiyo binafsi imeshachukuliwa kama ni shamba la bibi, kila mtu anaona ni sehemu ya kuchuma.
Unakuta mabango tu mtu anakutoza kodi, mtu wa Tanroad anakutoza kodi kwenye mabango hayohayo ya shule, anakuja TRA anakutoza kodi, bado halmashauri. Haishii tu kwenye mabango bali na katika leseni za biashara na kujikuta asilimia 30 ya mapato yote ya shule unalipa kodi.
Lakini ikifika mahali ukipandisha ada kutokana na gharama unazozipata katika kuendesha shule, wazazi nao wanahamisha watoto na kuwapeleka shule za Serikali.
Kwa kifupi hali hiyo isipotafutiwa ufumbuzi, kuna athari ya watoto kuja kuwa wa mtaani, wavuta bangi kwa kuwa shule binafsi zimekuwa na mchango mkubwa katika elimu. Pia ni katika ubia huo, nashauri ili kupunguza wingi wa wanafunzi katika shule za Serikali, wengine wangepunguzwa na kupelekwa shule za binafsi.
Nasema hivi kwa kuwa utafiti unaonyesha asilimia 30 ya madarasa katika shule binafsi hayana wanafunzi kwa sasa, hivyo Serikali ingeweza kuingia ushirikiano na shule hizo wanafunzi wakasomea huko, huku yenyewe ikilipa mishahara walimu badala ya hivi sasa inavyowalundika wanafunzi wengi darasa moja na kugeuka kuwa mzigo kwake.
Swali: Unaweza kueleza kwa kina hoja yako ya wanafunzi kuhamishiwa shule binafsi?
Jibu: Sheria ya Elimu inataka watoto 45 wafundishwe na mwalimu mmoja, hivyo shule binafsi kukiwa na watoto 15 watakaolipiwa ada na wazazi wao, tuchanganye na watoto 30 kutoka serikalini hapo watakuwa jumla 45 darasani.
Hili tulishalipendekeza pia kama Tamongsco (Chama cha Wamiliki na Mameneja wa Shule Binafsi) mwaka 2003 kwa kuandika barua kwa Katibu Mkuu, tukaambiwa tusubiri sera mpya ipite. Na hata katibu mkuu wa sasa tulimwandikia barua, na akatujibu tusubiri waijadili.
Swali: Unaonaje uamuzi wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kusitisha utangazaji wa shule na wanafunzi bora?
Jibu: Kuacha kutangaza kumefanya watu kuanza kubweteka lakini kubwa nachokiona ni Serikali kuogopa kuhojiwa kwa nini shule zake zinafanya vibaya.
Ieleweke kuwa kwenye elimu unapoficha taarifa kama hizo, watu wenye maslahi yao wanakuja kutengeneza orodha zao za kughushi na baadhi ya wazazi kujikuta wakiingia katika mkenge wa kuwapeleka watoto kwenye shule mbovu.
Utaratibu wa zamani urudishwe kwani utafanya watu kuwajibika kwa shule zao kutofanya vizuri na hapa Serikali iache kuingiza siasa katika hili, kama shule binafsi zinafanya vizuri, iende ikajifunze huko.
Pia kama inawezekana bodi za shule za Serikali zihusishe walimu waliotoka shule binafsi zinazofanya vizuri, ili wawasaidie kimawazo nini wanafanya kupata mafanikio katika ufaulu, badala ya shule binafsi kuonekana maadui katika utoaji elimu.
Mamlaka zinapaswa kujua kwamba sekta ya elimu ni yetu sote, kwa sababu tunapotengeneza daktari au mhandisi mbovu atakayekuja kutengeneza barabara mbovu kesho, sote tutalaumiwa, lakini tukifanya haya mambo kwa kushirikiana, hakika tutalifikisha Taifa letu mbali.
Swali: Unautazamaje mfumo wa utahini nchini ambao unakosolewa kwa kuweka msukumo zaidi kwenye mitihani ya mwisho ya taifa?
Jibu.Huu ni mfumo mbovu wa elimu, kwani kuna watu wengi wamefaulu mitihani ya chuo kikuu lakini wakienda kwenye zabuni mbalimbali wanashindwa.
Wapo wanaosingizia kutokuwa na mitaji au rushwa katika kuomba zabuni, lakini ukweli ni kwamba elimu yao ni ndogo katika uandikaji wa kuomba zabuni na kufikiri kuna rushwa katika zabuni za Serikali wakati zabuni hizo zipo mtandaoni.
Nashauri watoto kuanzia shule za msingi wafundishwe kinadharia na kivitendo. Kwa mfano, kama mwalimu wa hisabati anafundisha mada ya maumbo, aende kwa fundi wa makochi aone namna anavyobuni umbo la kochi pamoja na vipimo vyake.
Pia mwanafunzi apimwe katika kazi alizofanya za vitendo kwa sababu mwishowe binadamu hupimwa kwa vitendo vyake.Pia, ufundishaji wa somo la sayansi ufundishwe katika lugha nyepesi ambayo mtoto atailewa kulingana na mazingira anayoishi.
Swali: Una maoni gani kuhusu utaratibu wa sasa wa lugha mbili kutumika kama lugha za kufundishia katika ngazi tofauti, nini faida na hasara ya utaratibu huo?
Jibu: Siridhiki na lugha ya Kiingereza kufundishia; duniani kote hawafanyi hivyo. Wajapani, Wakorea, Waarabu na Warusi wengi hawajui Kiingereza na ndio mataifa makubwa tunayofanya nayo biashara.
Kinachotakiwa hapa sio lugha, bali kile ulichomfundisha hata kama ni kwa lugha yako, ameelewa kwa kiasi gani? Kwa kuwa watoto wengi wa Kitanzania hadi wanafikisha miaka mitatu wanakijua Kiswahili, ni vema wakafundishwa kwa lugha hiyo hadi chuo.
Matumizi hayo ya lugha mbili, ndio maana asilimia 70 ya wanafunzi wanaofeli kidato cha pili wanatoka shule za Serikali, kwa sababu tu walibadilishiwa lugha ya kufundishia baada ya kuingia sekondari.
Swali: Ungepewa nafasi ya kuongoza sekta ya elimu, ungeleta mabadiliko gani kwa Watanzania?
Jibu: Ningefanya mambo makuu manne ikiwamo kufuta Kiingereza kuwa lugha ya kufundisha. Pia Serikali ningehakikisha Serikali inagharamia elimu kwa wananfunzi wote, kuweka mkazo katika mafunzo ya amali na elimu ya nadharia inayofundishwa darasani kwenda sambamba na vitendo.