Miloud Hamdi aanzia jeshini | Mwanaspoti

MASHABIKI wa Yanga wanataka kuona mavitu ya kocha mpya wa timu hiyo, Miloud Hamdi wakati atakapokiongoza kikosi hicho katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania, utakaopigwa saa 10:15 jioni Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Kocha huyo aliyetua nchini kwa mara ya kwanza Desemba 30, mwaka jana kuinoa Singida Black Stars, alitambulishwa rasmi na Yanga Februari 4, mwaka huu kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Sead Ramovic aliyejiunga na CR Belouizdad ya Algeria.

Hamdi mwenye uraia pacha wa Ufaransa na Algeria alikishuhudia tu kikosi hicho jukwaani wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao Yanga ilishinda mabao 6-1, dhidi ya KenGold, Februari 5, hivyo kusubiriwa kile atakachoanza kukionyesha kikosini.

YN 01

Wakati Yanga ikiingia na mzuka baada ya kushinda michezo saba mfululizo ya Ligi Kuu Bara, kwa upande wa JKT Tanzania, haijashinda mchezo wowote kati ya sita iliyopita, huku pia mechi ya mwisho ikichapwa mabao 2-1, dhidi ya Coastal Union.

Katika michezo hiyo sita iliyopita, JKT imechapwa mitatu mfululizo na mingine ikiisha kwa sare, huku mara ya mwisho pia kushinda ilikuwa ni ushindi ugenini wa bao 1-0, dhidi ya Fountain Gate, mechi iliyopigwa Manyara Novemba 29, mwaka jana.

JKT inayoshika nafasi ya tisa na pointi 19, imekuwa haina safu bora ya ushambuliaji kwani katika michezo 17 iliyocheza, imefunga mabao 11 tu sawa na KMC, ikiwa ni timu ya tatu iliyofunga mabao machache baada ya Pamba (8) na TZ Prisons (9).

Moja ya ubora wa JKT Tanzania ni timu ambayo haijapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara ikiwa Uwanja wa Meja Isamuhyo Mbweni, kwani kati ya 17 iliyocheza, saba ni ya nyumbani na imeshinda mitatu, huku minne iliyobaki ikiisha kwa sare. 

YN 02

Mabao 11, ya JKT yamefunga na nyota mbalimbali na anayeongoza ni John Bocco na Said Ndemla wenye mawili kila mmoja, huku Edward Songo, Hassan Dilunga, Wilson Nangu, Shiza Kichuya, Hassan Kapalata na Najim Magulu wakifunga pia moja moja.

Licha ya ubora huo, ila inakutana na Yanga ambayo haijapoteza michezo saba mfululizo ya Ligi Kuu Bara ikifunga pia jumla ya mabao 28, ikiwa na wastani wa kufunga manne kwenye kila mchezo, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu tu.

Miongoni mwa nyota hatari katika kikosi cha Yanga katika mabao hayo ni Clement Mzize aliyefunga saba sawa na Prince Dube ingawa kwa Mzize amefunga tisa, wakifuatiwa na kiungo mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Pacome Zouzoua aliyefunga matano.

Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally alisema wachezaji wote wako katika morali nzuri ya mchezo huo isipokuwa nyota mshambuliaji wa kikosi hicho, John Bocco ambaye alipata changamoto ya hali ya hewa wakiwa jijini Arusha.

YN 03

“Tunaiheshimu Yanga kwa sababu ya ubora iliokuwa nao hadi sasa, lakini sisi kama benchi la ufundi tumejipanga kwa ajili ya kuhakikisha tunatumia mianya ya kuwazuia wasitushambulie, huku tukiandaa pia mikakati mizuri ya kutumia udhaifu wao.”

Kwa upande wa Kocha Hamdi anayefundisha soka la kushambulia kwa kasi kama ilivyokuwa kwa Ramovic, alisema licha ya ugeni wake ila amefuatilia maendeleo ya kila mchezaji mmoja mmoja ndani ya kikosi hicho, huku akiweka wazi mashabiki wasitarajie pia kufanya mabadiliko ya haraka kikosini humo.

“Wanasema timu ya ushindi huwa haibadilishwi, wachezaji wote wako tayari na kikubwa ambacho nitakifanya ni kuendelea tu pale tulipoishia, labda kuanzia mchezo wetu wa nne au zaidi ndiyo unaoweza kuona mabadiliko ya kiuchezaji yakitokea pia.”

YN 04

Mchezo mwingine ambao utapigwa sambamba na huo wa Yanga utakuwa kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge ambao wenyeji KMC iliyochapwa na Azam FC mabao 2-0, itacheza na Singida Black Stars iliyotoka sare ya 2-2 na Kagera Sugar mechi ya mwisho.

KMC inayoongozwa na Kocha, Kally Ongala inashika nafasi ya 11 na pointi 19, ambapo imekuwa na safu butu ya ushambuliaji na ulinzi kwani hadi sasa imefunga mabao 11, katika michezo 17, iliyocheza, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 23.

Ongala alitangazwa na KMC Novemba 14, mwaka jana akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Abdihamid Moallin, aliyejiuzulu mwenyewe kisha kujiunga na Yanga, baada ya kuiongoza KMC msimu huu katika ya michezo 11, ya Ligi Kuu Bara.

YN 05

Kocha huyo ameiongoza KMC katika michezo sita ya Ligi Kuu Bara na kati ya hiyo ameshinda mmoja tu, sare miwili na kuchapwa mitatu, jambo linalosubiriwa kuona ni kwa jinsi gani ataingia kwenye mchezo huo muhimu kwao wakiwa nyumbani.

Kwa upande wa Singida iliyopo nafasi ya nne na pointi 34, inaingia katika mchezo huo ukiwa wa pili kwa Kaimu Kocha Mkuu, David Ouma aliyetangazwa Februari 5, mwaka huu, baada ya kuondoka kwa Miloud Hamdi aliyejiunga na Yanga Februari 4.

Ouma alianza kuiongoza Singida ikitoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Kagera Sugar, huku ikishuhudia nyota mpya wa kikosi hicho raia wa Ghana, Jonathan Sowah akifunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya.

Mbali na matumaini ya Ouma kwa Sowah, ila nyota mwingine wa kuchungwa ni Mkenya Elvis Rupia aliyefunga mabao manane ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu, akipitwa bao moja tu na mshambuliaji, Clement Mzize wa Yanga aliyetupia kambani mabao tisa.

YN 06

Nyota pekee wa KMC waliobeba matumaini katika safu ya ushambuliaji ni Daruweshi Saliboko na Redemtus Mussa wenye mabao mawili kila mmoja wao, ingawa ongezeko la mshambuliaji mzoefu, Shaaban Idd Chilunda linaongeza morali ya kikosi hicho.

Mchezo wa raundi ya kwanza baina yao uliopigwa Septemba 12, mwaka jana, Singida ilishinda kwa mabao 2-1, yaliyofungwa na Elvis Rupia na Josaphat Arthur Bada, huku lile la kufutia machozi kwa upande wa KMC FC likifungwa na Redemtus Mussa.

Akizungumzia mchezo huo, Kally alisema wanatarajia mchezo mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao, ingawa wamejipanga kuwazuia ili wabaki na pointi tatu nyumbani, huku Ouma wa Singida akiweka wazi wanaiheshimu KMC FC ila watapambana nao.

Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana, utapigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo KenGold iliyotoka kuchapwa mabao 6-1, mechi ya mwisho na Yanga, itacheza na Fountain Gate ambayo iliibania Simba baada ya kuilazimisha sare ya bao 1-1.

KenGold iliyopo mkiani na pointi sita baada ya kucheza michezo 17, licha ya kusheheni mastaa waliotamba na timu za Yanga na Simba wakiwemo, Kelvin Yondani, Bernard Morrison, Zawadi Mauya na Obrey Chirwa, ila wana kazi kubwa ya kukinasua.

Timu hiyo iliyoshinda mchezo mmoja tu, sare mitatu na kupoteza 13, haijashinda michezo 10, mfululizo ya Ligi Kuu, baada ya kuchapwa minane na kutoka sare miwili, huku mara ya mwisho kushinda ilikuwa bao 1-0, na JKT Tanzania, Oktoba 4, mwaka jana.

Kwa upande wa Fountain Gate iliyopo nafasi ya saba na pointi 21, baada ya kushinda michezo sita, sare mitatu na kupoteza minane, haijashinda michezo minne mfululizo tangu mara ya mwisho ilipoichapa Coastal Union mabao 3-2, Desemba 13, mwaka jana.

Mchezo wa kwanza zilipokutana KenGold ilichapwa ugenini mabao 2-1, Septemba 11, mwaka jana, hivyo utakuwa ni wa kisasi kwao ili kuweka matumaini hai ya kusalia Ligi Kuu Bara, ingawa hata ikishinda itaendelea kusalia kuburuza huko mkiani.

Kocha msaidizi wa KenGold, Omary Kapilima alisema kutakuwa na mabadiliko ya wachezaji ambao hawakucheza mchezo wa mwisho na Yanga jambo linalowapa matumaini makubwa, licha ya kueleza wana kazi kubwa ya kufanya ili kujinasua kutoka mkiani.

Kwa upande wa Kocha wa Fountain Gate, Mkenya Roberto Matano anayekiongoza kikosi hicho katika mchezo wake wa pili baada ya sare ya bao 1-1, dhidi ya Simba, alisema licha tu ya ugeni wake ila kuna maendeleo mazuri ya mchezaji mmoja mmoja.

Related Posts