Minziro aona mwanga Pamba Jiji

BAADA ya Pamba Jiji kuvuna pointi sita katika mechi mbili mfululizo mara ya kwanza msimu huu katika Ligi Kuu Bara, kocha wa timu hiyo Fred Felix ‘Minziro’ amewataka wachezaji kuendelea kujitoa ili kuwa mbali na janga la kushuka daraja.

Pamba Jiji ilivuna pointi hizo kwa kuzifunga Dodoma Jiji na Azam FC bao 1-0 kila moja jambo ambalo limeifanya kukamata nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 18.

Akizungumza na Mwanaspoti, Minziro alisema: “Tunatakiwa kuendelea kuwa kwenye mwelekeo wa ushindi. Kiukweli nawapongeza wachezaji wangu kwa kazi nzuri ambayo wamefanya lakini matokeo hayo yanatakiwa kuwa chachu ya kuendelea kujitoa na kufanya vizuri zaidi katika michezo ijayo.”

Kwa mujibu wa ratiba mchezo unaofuata Pamba Jiji itakuwa nyumbani, Oktoba 15 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kucheza dhidi ya Coastal Union na baada ya hapo itacheza mechi mbili ugenini dhidi ya Mashujaa na Singida Black Stars kabla ya kuivaa Yanga.

Kocha huyo ambaye ameiongoza Pamba Jiji katika michezo 11 ya ligi tangu arithi mikoba ya Goran Kopunovic, Oktoba 17, mwaka jana, aliongeza kuwa, “bado tunapambana na safu yetu ya ushambuliaji, tumekuwa na changamoto ya umaliziaji wa nafasi naamini washambuliaji wangu wataendelea kuimarika na kuonyesha makali yao.”

Katika michezo 11 ambayo Minziro ameiongoza Pamba Jiji imeshinda mara nne mbali na Dodoma Jiji pamoja na Azam, Pia dhidi ya KenGold kwa bao 1-0 na Fountain Gate ambapo kwa mabao 3-1.

Timu hiyo imetoka sare mbili dhidi ya Kagera Sugar na JKT Tanzania, hivyo chini ya kocha huyo mzawa imevuna pointi 14.  Kwa kuzingatia ubora wa timu kwa sasa ndani ya michezo mitano iliyopita, Pamba Jiji ya Minziro inashika nafasi ya nane kwa kushinda mechi mbili sare moja na kupoteza mbili, kabla ya mechi ya jana, Yanga ndio timu hatari zaidi kwa sasa imeshinda zote tano.

Related Posts