Mwendokasi yashusha mabasi 100 yanayotumia gesi, full AC

Dar es Salaam. Kilio cha muda mrefu cha usafiri wa mabasi yaendayo haraka kinatarajia kumalizika baada ya Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) kushusha mabasi ya kisasa 100.

Awamu ya kwanza ya mradi inajumuisha barabara za Morogoro kutoka Kimara hadi Kivukoni-Kimara Gerezani na Kimara Morocco, ambayo ilianza kutoa huduma mwaka 2016 baada ya kuzinduliwa na Rais wa wakati huo, John Magufuli.

Katika miezi ya karibuni, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa abiria wanaotumia usafiri huu hususan nyakati za asubuhi na jioni baada ya magari yanayotua huduma kuwa machache.

Malalamiko kutoka kwa wakazi wa maeneo hayo ni kuwa wanalazimika kuyasubiri mabasi hayo muda mrefu vituoni, hivyo kuchelewa shughuli zao za kila siku, huku yale yanayofanya safari zake Mbezi kwenda Kivukoni na Mbezi kwenda Gerezani ndio yameonekana kuwa na changamoto zaidi hasa asubuhi na jioni.

Katika kukabiliana na adha hiyo, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Mei 2024 ilitangaza kuruhusu kurejeshwa kwa daladala 20, ambazo kila moja ilipaswa kuwa na uwezo wa kubeba abiria 40, hivyo kuwezesha wakazi wa Mbezi na maeneo ya jirani kupata usafiri kwa urahisi.

Matarajio ya mradi ilikuwa wananchi kukaa vituoni dakika chache, lakini imekuwa tofauti, kwani abiria husubiri mabasi kwa nusu saa au zaidi.

Viongozi wa Serikali wamekuwa wakifanya ziara na kutoa matamko ya kuboresha ufanisi.

Watumiaji wa usafiri huo wanakwenda mbali zaidi na kueleza kama awamu ya kwanza inasuasua, vipi awamu nyingine zitakuwaje, ikiwa ni pamoja na barabara za Kilwa kutoka katikati ya Jiji hadi Mbagala, katikati ya Jiji kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hadi Gongo la Mboto, Tegeta, na maeneo mengine.

Awamu ya tano inajumuisha barabara za Nelson Mandela, Mbagala, Tabata, Segerea, Kigogo, na awamu ya sita itahusisha barabara za Mwai Kibaki, na barabara nyongeza za awamu ya kwanza kutoka Kimara Mwisho hadi Kibaha.

Katikati ya vilio hivyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) wamezungumzia kinachoendelea ili kuufanya kuwa rafiki wa mfano kama ilivyotarajiwa.

Leo Jumatatu, Februari 10, 2025 bungeni jijini Dodoma, suala hilo limejadiliwa baada ya PIC kuwasilisha taarifa yake ya shughuli kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025.

Mwenyekiti wa PIC, Augustine Hole, amesema nia njema ya Serikali kutekeleza mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam inafifishwa na uendeshaji wa miradi hii, ambapo miundombinu yake inatumika kwa kiwango kidogo, jambo linaloshusha tija ya uwekezaji huu mkubwa.

“Ni vema taasisi husika zikaharakisha michakato ya kupata watoa huduma ili waweze kuendesha awamu zote za zilizokamilika kwa ufanisi na tija ya mtaji wa umma uliowekezwa iweze kupatikana,” amesema.

Hole amesema mradi huu unakabiliwa na changamoto, ikiwa ni pamoja na upungufu wa mabasi kwa awamu ya kwanza (Kimara – Kivukoni), ambapo mabasi 100 yanayofanya kazi badala ya 305; kuchelewa kukamilika kwa mchakato wa kumpata mwendeshaji katika awamu ya pili (Mbagala – Katikati ya Jiji).

Amesema changamoto hizi zisipotatuliwa, mtaji mkubwa wa umma uliotumika katika ujenzi wa miundombinu utakuwa umepotea.

Amesema kamati haioni jitihada za makusudi za kutumia au kuendesha mradi huu wa mwendo haraka kwa ukamilifu wake, licha ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa ambapo sehemu ya fedha inayotumika ikiwa ni fedha ya mkopo.

“Jambo hili linafifisha juhudi kubwa inayofanywa na Serikali, ni rai ya kamati kuwa Dart (Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka) iharakishe kupata watoa huduma kwa awamu zote tatu ili mradi huu uweze kuendeshwa kwa ukamilifu wake (full capacity) ili tija ya uwekezaji wa mtaji wa umma iweze kupatikana,” amesema Hole.

Wakati Bunge likiazimia hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Udart, Waziri Kindamba, hivi karibuni akiwa na ujumbe wa Tanzania walikwenda nchini China na kukutana na Kampuni ya Golden Dragon ambayo inatarajia kuleta mabasi 100.

Sehemu ya video aliyoiweka katika ukurasa wake wa kijamii wa Instagram, Kindamba amesema kuna Mapinduzi makubwa ya usafiri jijini Dar es Salaam yanakuja kwa mabasi yanayotumia gesi ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuongeza matumizi ya nishati safi.

“Mapinduzi makubwa ya usafiri jijini DSM yanakuja, tunaongeza idadi kubwa ya mabasi ya kisasa yanayotumia teknolojia ya gesi (CNG) kuendana na maelekezo ya Mh. Rais SSH kutumia nishati safi na kuepuka gesi ya ukaa,” amesema Kindamba.

Mwananchi lilipomtafuta Kindamba kufafanua zaidi, alielekeza kutafutwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Udart, Gabriel Katanga, ambaye alipotafutwa amesema mabasi hayo 100 kutoka China yanakuja kuongeza ufanisi katika mradi wa kwanza ambao ulianza mwaka 2016 Kimara-Gerezani-Kivukoni na Morocco.

“Tunatarajia mwanzoni au mwishoni mwa mwezi ujao (Machi) basi moja la majaribio litakuja nchini na mabasi mengine 100 tunatarajia hadi Mei yawe yamefika,” amesema Katanga akisema basi moja litakuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 150.

Alipoulizwa mabasi haya yana tofauti gani na yaliyopo sasa, amesema: “Haya ya sasa yanatumia mfumo wa gesi, yatakuwa na AC (viyoyozi), wameangalia hali ya hewa tuliyonayo hapa, kwa kifupi ni mabasi ya ‘class’ ya juu.”

Amesema kwa sasa wana mabasi 208, lakini yanayotoa huduma ni 130, huku mengine yakifanyiwa marekebisho na kurudi barabarani kuendelea kutoa huduma.

Mkazi wa Kimara, Mariam Juma, akizungumza na Mwananchi amesema: “Sisi wananchi kwa kweli tumechoka na ahadi za kila uchwao, tunachokitaka ni kuona magari, kama kweli yanakuja yatasaidia kutupunguzia adha ya usafiri.”

“Nakumbuka tuliambiwa unakaa kituoni dakika tano tu gari imefika, lakini kwa sasa unaweza kukaa kituoni hata saa nzima, sasa hakuna maana tena ya mwendokasi,” amesema Mariam.

Mkazi wa Mbezi, Christina Mollel, hana matumaini kuhusu ujio wa mabasi hayo kutokana na kile alichoeleza, ahadi nyingi zilishatolewa lakini mabasi hayakuonekana.

Ingawa amekosa matumaini, amesema iwapo yataletwa yatasaidia kupunguza msongamano vituoni na mrundikano ndani ya mabasi unaosababishwa na uhaba wa vyombo vya usafiri.

“Kituoni unakaa nusu saa hadi saa kusubiri basi na linapita likiwa limejaa kiasi cha kukosa pa kuingia, mabasi machache abiria wengi, angalau yakiongezeka yatakidhi mahitaji,” amesema.

Mussa Salum anayeishi Ubungo, amesema angalau mabasi hayo yatapunguza adha ya usafiri kwa watumiaji wa barabara ya Morogoro.

“Tulidhani mabasi yaendayo haraka yangetuepusha na msongamano wa magari na kuchelewa kazini, lakini hali iliyopo sasa yamekuwa chanzo cha kuchelewa kazini kwa sababu hayapiti vituoni kwa wakati na hata yanayopita huwa yamejaa,” amesema.

Kwa mujibu wa Mussa, ndani ya basi moja huwa na abiria zaidi ya 200 na wakati mwingine inakosekana hewa.

“Kuna mama aliwahi kuzirai ndani ya basi kwa sababu amekosa hewa, watu tunabanana huna pa kupumulia,” amesema.

Related Posts