Mwinyi: Maboresho ya mahakama yaendane na marekebisho ya sheria zilizopotwa na wakati

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema maboresho ya mahakama ya kiutendaji na mifumo lazima viende sambamba na upitiaji wa sheria ambazo zimepitwa na wakati na zile ambazo ni kikwazo katika kufikia upatikanaji wa haki.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Februari 10, 2025 katika kilele cha Wiki ya Sheria mjini Unguja, kwamba maboresha pekee ya mahakama hayatakuwa na maana iwapo zitaendelea kuwapo sheria ambazo zimepitwa na wakati.

Amesema mafanikio katika utekelezaji wa mipango ya Serikali ya kuimarisha ustawi wa jamii, lazima yaendane na mchango wa sekta ya sheria ikiwemo mahakama.

“Nimefurahi kusikia kazi kubwa ya maboresho ya kiutendaji na mifumo inayoendelea, lakini hatuna budi kuhakikisha kwamba tunachukua hatua za kurekebisha sheria zilizopitwa na wakati na zile zinazokwaza upatikanaji wa haki.

Ametolea mfano wa sheria ya Mwenendo wa Madai ya Zanzibar ya mwaka 1917 sura ya nane akisema ni ya zamani imeshapitwa na wakati kwani ina zaidi ya miaka 100.

“Maendeleo mbalimbali yaliyotokea kwa miaka yote hiyo yakiwemo ya teknolojia na matakwa ya sheria za uwekezaji ni  sababu ya  kuwa na sheria mpya,” amesema 

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa nchi, sheria na mifumo bora ya kusimamia mashauri katika vyombo vya kutafuta haki vina mchango mkubwa katika kuwavutia wawekezaji kuja  kuwekeza nchini.

Ametumia fursa hiyo kuikumbusha mahakama na wadau wake wote kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili katika utoaji wa haki na kwamba Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa maadili  kwa watumishi wa umma, na kwa upande wa mahakama suala la maadili lina uzito wa aina yake.

“Tunapaswa tutambuwe kuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala wa sheria ni kuwepo kwa vitendo vya rushwa, uzembe, kukosa uwajibikaji na ukiukwaji kwa maadili,” amesema na kuongeza

“Naamini kuwa wengi wenu mnajitahidi kulizingatia suala hili, lakini kutokana na umuhimu wake, nimeona ni vyema  kutumia hadhara hii kwa lengo la kuzidi kusisitiza na kukumbushana,”

Amesema Serikali inaelewa  kwamba, utekelezaji wa sheria kwa uadilifu na kuwepo kwa mifumo imara  ya upatikanaji haki  ni msingi umuhimu katika kujenga na kukuza imani ya wananchi kwa Serikali yao, kuleta  amani na utulivu katika nchi pamoja na kuchochea mafanikio ya kiuchumi na kijamii.

“Ni dhahiri kuwa ustawi bora wa jamii, kwa kiasi kikubwa kutategemea kuwepo kwa misingi imara ya kuheshimu haki za binadamu, utawala wa sheria, uhuru wa mahakama na uwepo wa sheria na mifumo madhubuti inayorahisisha upatikanaji wa haki hizo kwa usawa na kwa wakati,” amesema.

Katika kuliendea hilo, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa muhimili huu wa mahakama na wadau wake ili kuhakikisha utawala bora na haki za wananchi katika nyanja zote zinazopatikana.

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla amesema mwaka 2024 jumla ya mashauri mapya 7,912 yalifunguliwa kuanzia Januari hadi Desemba kwa mahakama zote za Zanzibar. Miongoini mwa mashauri hayo ya jinai ni 4,319, madai 3593.

“Katika kipindi hiki mashauri 5,348 yaliamualiwa sawa na asilimia 78 na mashauri yanayoendelea mahakamani ni 2,564 sawa na asilimia 22,” amesema.

Amesema katika mahakama maalumu za udhalilishaji mwaka 2024 mashauri mapya ni 292 huku kwa upande wa mahakama maalumu za makosa ya dawa za kulevya mwaka 2024 alisema jumla ya mashauri mapya 104  yalifunguliwa.

Hata hivyo, amesema kwa mwaka 2025 mahakama imeweka malengo mbalimbali ikiwemo kuimarisha na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa kuhakikisha ubunifu na usanifu wa mifumo ya kielektroniki ya usikilizaji wa mashauri inakamilika ndani ya mwaka huu.

“Vile vile kuharahisha usikilizaji wa mashauri kwa kuzingatia sheria na kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani,” amesema.

Jaji Khamis amesema wanaendelea kufanya tathmini ili kujua kwa namba gani watumiaji wa mahakama wanaridhika na huduma zinazotolewa katika mahakama.

Related Posts