Nyota saba washonwa ajali ya Dodoma Jiji

WACHEZAJI saba kati ya 37 waliopata majeraha katika ajali ya gari la timu ya Dodoma Jiji FC bado wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Kinyonga kutokana na kuumia kwa kukatwa na vioo wakati gari hilo lilipoanguka kwenye Mto Matandu katika barabara ya Kibiti-Lindi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo alisema ajali hiyo imetokea saa 3 asubuhi wakati kikosi hicho kikitokea Ruangwa, Lindi ilikocheza dhidi ya Namungo katika pambano la Ligi Kuu Bara lililoisha kwa sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja Majaliwa, Lindi.

Dodoma ilikuwa inawahi kwenda Dodoma ili kuanza maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Simba utakaopigwa Februari 15 kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.

Nyundo alisema katika ajali hiyo wachezaji saba bado wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga na wengine wamepumzika hotelini ili kusubiri wenzao wanaopatiwa matibabu, endapo hali zao zitakuwa zinaendelea vizuri watajumuika nao ili kuanza safari kwa kutumia usafiri mwingine.

“Dereva wa Dodoma Jiji alikuwa katika mwendo wa kasi, na pale walipopata ajali ni sehemu ambayo njia iliharibiwa na mvua za kimbunga Hidaya, sasa dereva alikuwa hajaangalia vizuri na kusababisha gari kuingia kwenye korongo la mto na kuleta madhara ya kuumia kwa wachezaji pamoja na kuharibu gari,” alisema Nyundo.

DC Nyundo aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Yassin Mgaza, Allan Ngereka, Disan Gariwango, Omary Shomary Rajabu, Francis Mkanula, Juma Kiswagala na Obata Paul na majeruhi wengine waliruhusiwa.

Shuhuda, aliyekuwapo eneo la tukio, Jafari Said alisema kuwa eneo ambalo wamepata ajali Dodoma Jiji ni sehemu ambayo ina mteremko na dereva alikuwa hajaangalia vizuri wakati wanashuka na kusababisha kuingia mtoni.

“Madereva wanatakiwa kuwa makini pindi wanapokuwa barabarani ili kuepusha ajali kama hizi,” alisema Said.

Hii ni ajali ya pili kwa msimu huu kwa timu za Ligi Kuu baada ya awali JKT Tanzania kupata ajali Oktoba 26 mwaka jana wakitokea Dodoma kurudi Dar es Salaam na kusababisha wachezaji kadhaa kuumia akiwamo John Bocco, Said Ndemla na wenzao walipatiwa matibabu.

Julai 9, 2021 timu ya Polisi Tanzania ilipata ajali ikitoka mazoezini CCP Moshi na kusababisha nyota wa timu hiyo Gerald Mdamu kuvunjika mguu mara mbili na kumsababishia kushindwa kuendelea kucheza soka kama ambavyo Mwanaspoti ilishawahi kuripoti madhila yake ikiwamo kuteseka kwa miaka mitatu akiuguza majeraha na imemsababishia ulemavu wa kudumu wa mguu wake ambao kisigino hakifiki kukanyaga chini.

Related Posts