Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali imelipa takribani Sh254 bilioni ndani ya miezi miwili kwa wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya barabara na madaraja nchini.
Kufanyika kwa malipo hayo kwa mujibu wa Ulega ni utejkelezwaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka makandarasi wote wanaotekeleza kazi mbalimbali walipwe.
Hata hivyo, mapema baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Ulega aliahidi kuhakikisha kila mkandarasi anayeidai Serikali atalipwa fedha yake na wote wanaotekeleza kazi watalipwa kama walivyokubaliana.
Hayo yanakuja katika kipindi ambacho, kuliibuka malalamiko kwa makandarasi hasa wazawa kutolipwa fedha zao kwa wakati wanapotekeleza miradi mbalimbali, jambo linalodhoofisha ufanisi wao.
Ulega ameyasema hayo jijini Dodoma jana Jumapili, Februari 9, 2025, baada ya kukagua ujenzi wa Barabara ya Ntyuka hadi Kikombo yenye urefu wa kilomita 76 inayojengwa kwa awamu mbili na makandarasi wawili ambao ni CHICO pamoja na China First.

Amesema Rais Samia ametoa maelekezo ya kulipwa kwa wakandarasi hao, ili kuwajengea uwezo wa kukamilisha miradi yote ya sekta ya ujenzi kutekelezwa kama ilivyopangwa.
“Mmeona katika muda wa hii miezi mwili, Rais Samia tayari amelipa malipo ya wakandarasi ya takribani Sh254 bilioni, matumaini yetu tunataka kuona kazi zikiendelea,“ amesema Ulega.
Amesema mwishoni mwa Februari 2025, Serikali inatarajia kutoa fedha nyingine za kutekeleza miradi ya miundombinu katika sekta ya ujenzi.
Ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuipa kipaumbele barabara hiyo ili ianze kujengwa haraka.
Waziri wa Madini, ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde amesema Barabara ya Ntyuka – Mvumi- Kikombo ina historia ni vema ikamilishwe.
Amesema kujengwa kwa kiwango cha lami kwa barabara hiyo utakuwa ukombozi kwa kuwa inakwenda ilipo hospitali ya macho ya Mvumi.
Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohammed Besta amesema ujenzi wa barabara ya Ntyuka- Mvumi- Kikombo unatekelezwa kwa sehemu mbili.
Sehemu ya kwanza, amesema kutoka Ntyuka- Mvumi- Makulu na Kikombo-Chololo -Mapinduzi (Kilomita 25) inatekelezwa na Mkandarasi CHICO kwa Sh38.1 bilioni.
Kwa upande wa sehemu ya pili, amesema ni Ntyuka-Mvumi Hospitali – Kikombo (Kilomita 53) inatekelezwa na Mkandarasi China First kwa Sh98.4 bilioni.