Sugu awataka wanachadema kumaliza tofauti zao wakati wa uchaguzi

Mbeya. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amewataka wanachama na wafuasi wa chama hicho kuondoa tofauti zilizokuwepo wakati wa uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti Taifa badala yake waungane kufikia malengo.

Uchaguzi wa chama hicho katika nafasi mbalimbali ngazi ya Taifa ulifanyika Januari 21, 2025, ambapo Tundu Lissu aliibuka mshindi dhidi ya Freeman Mbowe aliyekuwa akitetea nafasi hiyo.

Akizungumza leo Jumatatu, Februari 10, 2025, katika Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha), Sugu amesema uchaguzi umeisha na kinachohitajika ni kuungana kwa pamoja na kuondoa tofauti zilizokuwapo wakati wa uchaguzi.

Amesema ili kufikia malengo ya kuking’oa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wanahitaji nguvu ya umma, hivyo bila umoja hawataweza.

“Uchaguzi umeisha ngazi zote, tulianza mkoa, kanda na hatimaye Taifa, tuwe wamoja kwa sasa, tofauti zetu ziishe, bila umoja hatutafanikiwa kufikia malengo.

“CCM inategemea nguvu ya dola, sisi tunategemea nguvu ya umma. Tushirikiane na viongozi wote waliochaguliwa, Elizabeth Mwakimomo (Makamu Mwenyekiti Bawacha), waunganishe wanawake kwani wanayo nguvu sana ya maamuzi katika nchi hii,” amesema Sugu.

Ameongeza kuwa anaamini hakuna utofauti mkubwa kwani wote wamekutana katika chama hicho wakiwa wakubwa na kuunganishwa na Chadema, hivyo matarajio yake ni kuonesha mfano wa mageuzi kwenye kanda hiyo.

Baadhi ya wanawake wa Bawacha wakiwa katika mkutano wa Chadema uliofanyika jijini Mbeya.

Amesema kuwa kwa sasa wanachosubiri ni kauli ya Mwenyekiti wao mpya wa Taifa, Lissu, kutoa mwelekeo wa chama kwenda mbele, akieleza kuwa waliotarajia Chadema kupasuka baada ya uchaguzi wanapoteza muda kwani ni chama kinachotegemewa na Watanzania.

“Ajenda tunazo, Chadema ndiyo chama tegemeo kwa wananchi na hakiwezi kupasuka kwa uchaguzi. Tuna umoja wetu na tunasubiri kauli ya mwenyekiti mpya atupe mwelekeo,” amesema mbunge huyo wa zamani wa Mbeya Mjini.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Elizabeth, ametumia fursa hiyo kuwashukuru wapigakura kwa kumpitisha kushika nafasi hiyo, akieleza kuwa yuko tayari kupokea ushauri na kuelekezwa katika kuongoza nafasi hiyo.

“Ninawaahidi kile nilichoeleza kwenye sera yangu nitatekeleza. Niko tayari kushirikiana na kushauriana na wenzangu kukiongoza chama chetu. Kupitia wanawake, nataka kupata usawa na ushirikishwaji.”

“Hata zile nafasi za kitaifa tunahitaji wanawake zaidi kwani tuna uwezo na nia ili wawepo katika kurugenzi zilizobaki kitaifa. Chadema si ya mchezo mchezo na wanawake wanajiweza,” amesema Elizabeth

Mwenyekiti wa Chadema mkoani Mbeya, Masaga Kaloli, amesema imekuwa bahati kubwa mkoa huo kupata viongozi wakubwa ngazi ya Taifa, akiwaomba kutumia fursa hiyo kushirikiana vyema kutengeneza chama hicho.

“Mkitumia hii fursa kuwaunganisha kina mama, kanda hii itakuwa bora katika uchaguzi. Binafsi nilikuwa namuunga mkono Mbowe, lakini tulitarajia kwamba lazima mshindi atapatikana, hivyo tutaenda naye Lissu na tutashirikiana naye kuiondoa CCM madarakani,” amesema Kaloli.

Kaloli amesema Bawacha imepata viongozi imara, akieleza kuwa waliotarajia mkwamo katika nafasi hiyo wanajidanganya na kwamba kupitia Elizabeth, wanawake wengine watahamasika zaidi kuwania nafasi nyingine za juu.

Naye Makamu wa Baraza la Wazee wa chama hicho (Bazecha), Hamid Mfalingundi, amesema matarajio yao ni kuona matokeo chanya hasa inapoelekea uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais.

“Tunaenda kwenye uchaguzi, tunaomba kuwapo haki sawa kwa upande wa wanawake. Sisi Bazecha tunaamini kutakuwapo matokeo mazuri huko tunakoelekea, tutawapa ushirikiano wowote,” amesema Mfalingundi.

Related Posts