Tabora. Zaidi ya Sh15 bilioni zimetengwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa mizani wa kupima uzito wa magari utakaowabana madereva wanaopitisha kinyemela mizigo mikubwa katika eneo la Kizengi lililopo Wilaya ya Uyui mkoani Tabora.
Akizungumza Februari 9, 2025 wakati akikagua ujenzi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) Mkoa wa Tabora, Raphael Mlimani amesema baadhi ya madereva wasio waaminifu wamekuwa wakipitisha mizigo mikubwa kwa kuwa eneo hilo halina mizani kwa muda mrefu na kuharibu miundombinu ya barabara.
Mlimaji amesema licha ya kufanyika kwa operesheni mbalimbali ili kudhibiti hali hiyo, hazikufanikiwa na kusababisha ujenzi wa mara kwa mara katika barabara.
“Kuzidisha mizigo kunasababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na hivyo kusababisha matengenezo ya mara kwa mara,” ameeleza.
Amesema mradi huo uliofika asilimia 30 ya ujenzi, unajengwa na kampuni ya WU YI ya nchini China chini ya mkandarasi Wang Wei ikiwa na mkataba wa miezi 16 ambapo ujenzi ulianza Februari 19, 2024 na utakamilika Juni 19, 2025.
Mmoja wa madereva wa gari la mizigo aliyekutwa eneo hilo, Japhet Mwanzo amesema baadhi yao wamekuwa na tabia ya kubeba mzigo mkubwa maeneo yasiyo na mizani na kuipunguza kwenye bajaji za mizigo wanapofika kwenye mizani kisha kuirudisha baada ya kuruhusiwa kupita.
“Ujenzi ukikamilika nadhani hata barabara hazitoharibika na kutusababishia adha sisi madereva tunaofuta sheria,” amesema.
Naye Shabani Kasim, kijana aliyepata fursa ya ajira kwenye mradi huo, amesema licha ya kupata ajira inayomtimizia mahitaji yake, pia ananufaika na ujuzi anaoupata kwenye kutekeleza mradi huo.
Mkoa wa Tabora una mtandao wa barabara wa kilomita 2188.09, kati ya hizo kilometa 967 ni barabara kuu zinazounganisha mkoa huo na mikoa mingine nchini.