Timu ya Dodoma Jiji yapata ajali Nangurukuru

KIKOSI cha Dodoma Jiji kimepata ajali ya basi kikitokea Ruangwa mkoani Lindi kuja jijini Dar es Salaam, baada ya jana tu kumaliza mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao Namungo FC, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu, Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson amesema ni kweli ajali hiyo imetokea katikati ya Nangurukuru na Somanga, huku akiweka wazi majeruhi ni wengi ila hakuna taarifa yoyote ya kifo hadi sasa.

“Basi lilipinduka mara mbili kwenye mto na wachezaji waliopata majeraha ya ajali ni wengi, tunashukuru tumepata msaada wa haraka sana wa kijiji na Serikali ya Mkoa wa Lindi ambao hadi muda huu tunapoongea wanaendelea kuwaokoa,” amesema.

Fortunatus amesema kwa sasa ni mapema kuzungumza kile kinachoendelea ingawa baada ya muda watatoa taarifa kamili kwa kushirikiana na madaktari wa mkoa, hivyo mashabiki, wapenzi na wadau wa soka nchini waendelee kuwaombea majeruhi wote.

Dodoma Jiji ilikuwa safarini kuja Dar es Salaam kisha kwenda jijini Mbeya kwa ajili ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara na maafande wa Tanzania Prisons uliopangwa kuchezwa Februari 14 kwenye Uwanja wa Sokoine, ingawa huenda mechi hiyo isichezwe.

Related Posts