Dar es Salaam. Zaidi ya kampuni tano za kigeni kutoka Ufaransa na Misri, pamoja na wawekezaji wa ndani ya Tanzania, wameonyesha nia ya kuwekeza katika usafirishaji wa nyaya (cable).
Ili kufanikisha hilo sasa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) inakamilisha Kanuni za Usafiri wa Waya za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Mwaka, 2024 katika ngazi ya Serikali.
Kanuni zingine zinazoendelea zinazopendekezwa ni pamoja na Kanuni za Latra (Utoaji Leseni kwa Waendeshaji Reli) 2024 na Kanuni ya Utoaji Leseni ya Usafiri (Leseni ya Kipekee ya Usafiri wa Umma), 2024.
Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Mawasiliano wa Latra, Salum Pazzy ameiambia The Citizen kwamba kampuni mbili kutoka Ufaransa na moja kutoka Misri zimejitokeza zikisubiri idhini ya kuwekeza katika sekta hiyo.
Kampuni hizi zimewasilisha mapendekezo yao na yanasubiri kuidhinishwa kwa kanuni ili kujihakikishia mazingira mazuri kwani usafiri wa waya unaonekana kuwa fursa kubwa ya kiuwekezaji.
“Nia hii inayoongezeka inaangazia uwezo wa usafiri wa cable kama suluhisho la mageuzi la kukabiliana na changamoto za usafiri na kukuza ukuaji wa uchumi,” amesema Pazzy.
Kuhusu wawekezaji wa ndani, Pazzy amesema Latra tayari imetoa leseni za muda kwa baadhi ya kampuni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji wa waya na pindi ujenzi utakapokamilika mamlaka itatoa leseni za uendeshaji.
Hata hivyo, Pazzy hakutaja makampuni lakini alibainisha kuwa baadhi tayari yanaendesha mifumo hiyo huko Meru.
Amesema pindi tu kanuni hizo zitakapokamilika, wawekezaji watazipitia na kufanya maamuzi yao ya uwekezaji.
“Baadhi ya makampuni yatahusika katika ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa waya. Makampuni haya ya ujenzi yakishaingia, wawekezaji wengine, kama waendeshaji, wataiga mfano huo na kufanya uwekezaji wao,” amesema.
Kanuni zinazokuja zinatarajiwa kutoa mwelekeo wa wazi ambao utakuza mazingira mazuri ya uwekezaji na maendeleo endelevu ya njia hii ya ubunifu ya usafiri huku wadau mbalimbali ambao wameonyesha nia ya kuwekeza katika usafiri huo wakizisubiri kwa shauku.
Hii ni muhimu hasa kwa kuzingatia ongezeko la uhamasishaji na uvutiaji wa watalii uliofanyika kupitia filamu ya Royal Tour ambayo imekuza sekta ya utalii kwa kiasi kikubwa na sasa inavutia wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika usafiri wa cable.
Akizungumzia muda ambao utatumika katika maandalizi ya kanuni hizo, Pazzy amesema hazitachukua muda mrefu kukamilika kutokana na maslahi makubwa ya uwekezaji wakati ambao serikali inajitahidi kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji.
Hiyo inafanya sasa wizara kushinikiza kutekelezwa kwa kanuni za usafirishaji wa waya ambao zinatarajiwa kuwa tayari ndani ya miezi michache ijayo.
“Tunawahimiza wawekezaji wa ndani wajitokeze kwani hii ni sekta mpya yenye mchangi mkubwa kiuchumi katika sekta ya utalii. Aidha alieleza kuwa Latra iko tayari kutoa mwongozo, na endapo yeyote atakumbana na changamoto atatoa msaada,” amesema.