Ukweli kuhusu Watanzania wanaougua kifafa

Dar es Salaam. Matokeo ya sasa ya utafiti yanaonesha kupungua kwa idadi ya wanaoathirika na ugonjwa wa kifafa, kutoka zaidi ya 70 mpaka 20 hadi 15 kwa kila watu 1000.

Utafiti huo uliofanywa na Chama cha Wataalamu wa Kifafa Tanzania (TEA) umeonesha pia kupungua kwa waathirika wapya, kutoka zaidi ya 73 hadi kufikia 50 kwa kila watu 100,000 kwa mwaka.

Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Patience Njenje alipofanya mahojiano kuelekea siku ya Kimataifa ya Kifafa ambayo inaadhimishwa leo Jumatatu, Februari 10, 2025.

“Tanzania ni moja ya nchi zenye baadhi ya vijiji vyenye idadi kubwa ya walioathirika, hadi kufikia watu 37.5 kwa kila watu 1000 ikiwa na watu 73-111 kwa kila wagonjwa 100,000 wapya wanaoongezeka kila mwaka,” amesema Dk Njenje.

Amesema wakilinganisha kwa umri, wagonjwa wenye kifafa wana kiwango kikubwa cha kufa mara sita kuliko watu wote.

Amesema zaidi ya asilimia 60 ya vifo hutokana na athari za ugonjwa huo, za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja.

“Kwa sasa kiwango cha kufa kwa wagonjwa kimebakia juu mara nne kuliko watu wote. Wagonjwa wenye kifafa ni watu wenye umri mdogo wakiwa na wastani wa miaka 15.4 ambayo imebakia sawia na matokeo ya miaka 60 na 32 iliyopita,” amesema.

Hata hivyo, utafiti wa Wizara ya Afya, unaonesha takribani watu milioni moja wanaishi na kifafa nchini.

Kifafa ni ugonjwa sugu usioambukiza wa ubongo, unaoathiri takriban watu milioni 50 duniani.

Kwa mujibu Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa Februari 2025, idadi hiyo ya watu ni jambo linaloufanya kuwa miongoni mwa magonjwa ya kawaida ya neva duniani, huku karibu asilimia 80 yao wakiishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

Inakadiriwa kuwa hadi asilimia 70 ya watu wanaoishi na kifafa, wanaweza kuishi bila mshtuko wa kifafa ikiwa watagunduliwa na kutibiwa ipasavyo.

Robo tatu ya watu wenye kifafa wanaoishi katika nchi za kipato cha chini hawapati matibabu wanayohitaji. Katika sehemu nyingi za dunia, watu wenye kifafa na familia zao wanakabiliwa na unyanyapaa na ubaguzi.

Mshtuko wa kifafa husababishwa na utoaji wa umeme kupita kiasi kwenye kundi la seli za ubongo. Sehemu mbalimbali za ubongo zinaweza kuwa chanzo cha utoaji huu wa umeme.

Mshtuko mmoja wa kifafa hauashirii kifafa. Takribani asilimia 10 ya watu duniani hupata mshtuko mmoja wa kifafa katika maisha yao.

Hofu, kutoeleweka, ubaguzi na unyanyapaa wa kijamii vimezunguka kifafa kwa karne nyingi. Hali hii inaendelea katika nchi nyingi hadi leo na inaweza kuathiri ubora wa maisha ya watu wenye ugonjwa huu na familia zao.

Tabia za mshtuko wa kifafa hutofautiana na hutegemea sehemu ya ubongo ambapo msukumo wa umeme umeanza na jinsi unavyosambaa.

Dalili za muda mfupi zinaweza kutokea, kama vile kupoteza fahamu au umakini na usumbufu wa harakati, hisia pamoja na kuona, kusikia na ladha, hali ya moyo au kazi nyingine za utambuzi.

Watu wenye kifafa huwa na matatizo mengi ya kimwili, kama vile kuvunjika mifupa na michubuko kutokana na majeraha yanayohusiana na mshtuko wa kifafa, pamoja na viwango vya juu vya matatizo ya kisaikolojia, ikiwa ni pamoja na wasiwasi na mfadhaiko.

Sehemu kubwa ya vifo vinavyohusiana na kifafa, hasa katika nchi za kipato cha chini na cha kati, vinaweza kuzuilika, kama vile kuanguka, kuzama majini, kuungua moto na mshtuko wa kifafa wa muda mrefu.

Kifafa kinachangia sehemu kubwa ya mzigo wa magonjwa duniani. Inakadiriwa kuwa kati ya watu wanne mpaka 10 kwa kila watu 1000 wana kifafa hai kwa wakati fulani.

Duniani kote, inakadiriwa kuwa watu milioni 5 hugunduliwa na kifafa kila mwaka. Katika nchi za kipato cha juu, inakadiriwa kuwa watu 49 kwa kila 100,000 hugunduliwa na kifafa kila mwaka.

Katika nchi za kipato cha chini na cha kati, idadi hii inaweza kuwa juu hadi 139 kwa kila 100,000.

Mshtuko wa kifafa unaweza kudhibitiwa. Hadi asilimia 70 ya watu wanaoishi na kifafa wanaweza kuacha kupata mshtuko wa kifafa kwa kutumia dawa za kupambana na kifafa ipasavyo.

Katika nchi za kipato cha chini, takriban robo tatu ya watu wenye kifafa hawapati matibabu wanayohitaji hali inayotafsiriwa kama pengo la matibabu.

Upatikanaji wa dawa za kifafa katika nchi za kipato cha chini na cha kati ni wa chini. Utafiti wa hivi karibuni ulibaini kuwa upatikanaji wa wastani wa dawa za kawaida za kifafa katika sekta ya umma ya nchi hizi ulikuwa chini ya asilimia 50.

Hata hivyo upasuaji unaweza kuwa na manufaa kwa wagonjwa wasiopata nafuu pindi watumiapo dawa.

Inakadiriwa kuwa asilimia 25 ya ugonjwa wa kifafa unaweza kuzuilika. Kuzuia majeraha ya kichwa, kwa mfano kwa kupunguza ajali za barabarani na michezoni ni njia bora ya kuzuia kifafa cha baada ya ajali.

Huduma bora wakati wa ujauzito inaweza kupunguza matokeo ya kifafa kinachosababishwa na majeraha ya kuzaliwa.

Kuzuia magonjwa ya kuambukiza kwenye mfumo wa neva, hasa katika maeneo ya tropiki, kunaweza kusaidia kupunguza kifafa duniani kote.

Athari za kijamii na kiuchumi, kifafa kinachangia zaidi ya asilimia 0.5 ya mzigo wa magonjwa duniani, kikihusisha mahitaji ya huduma za afya, vifo vya mapema na upotevu wa tija kazini.

Gharama kubwa za matibabu na upotevu wa mapato unaweza kuwa mzigo mkubwa kwa kaya. Unyanyapaa na ubaguzi unaohusiana na kifafa mara nyingi ni magumu zaidi kushinda kuliko mshtuko wa kifafa wenyewe.

Hata hivyo, watu wenye kifafa wanakabiliwa na vikwazo katika elimu, ajira na huduma za afya. Sheria zinazotokana na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu zinaweza kusaidia kupunguza ubaguzi na kuboresha maisha ya watu wenye kifafa.

Related Posts