Wanajeshi 75 wa DRC mbaroni, wadaiwa kuwakimbia waasi vitani

Mwanza. Mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) limewakamata na kuwashtaki wanajeshi 75 wa jeshi la nchi hiyo (FARDC), kwa kosa la kuwakimbia waasi kwenye uwanja wa vita.

Shirika la Habari la Reuters limeripoti jana Jumapili Februari 9, 2025, kuwa wanajeshi hao walikacha mapigano dhidi ya wapiganaji wa kundi la M23, walipokuwa wakienda kuiteka miji iliyoko Jimbo la Kivu Kaskazini, Mashariki mwa DRC.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Jeshi la FARDC, wanajeshi hao pia wanashtakiwa kwa makosa ya kufanya uporaji na uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo kuwaua raia katika maeneo hayo.

Taarifa hiyo imetoka wakati ambao Umoja wa Mataifa (UN) ulitoa taarifa ya utekelezwaji wa matukio ya uhalifu dhidi ya binadamu mashariki mwa DRC huku ukituhumu M23 na Jeshi la FARDC kutekeleza unyama huo.

Miongoni mwa matukio yanayodaiwa kutekelezwa na pande hizo kwa mujibu wa UN ni pamoja na mauaji, ubakaji wa makundi na utumwa wa kingono uliokuwa ukifanywa dhidi ya wakazi wa maeneo yenye na mapigano hayo.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN, katika ripoti yake ilidai kuwa matukio mengi yanayoshabihiana na ukatili huo yalitekelezwa wakati wa mapigano kati ya FARDC dhidi ya M23, yaliyosababisha waasi kuutwaa Mji wa Goma nchini humo.

Miongoni mwa visa vya kushtua vilivyoripotiwa ni pamoja na mauaji ya watu zaidi ya 3,000 mashariki wa DRC ikiwemo wafungwa 150 waliobakwa kisha kuuawa na makundi hayo.

Mamlaka nchini DRC hazijatolea ufafanuzi wowote kuhusiana na tuhuma hizo zikiitaka UN kuendelea kufanya uchunguzi wa uwepo wa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu mashariki mwa nchi hiyo hususan yanayotekelezwa na M23.

Rwanda, imekuwa ikishutumiwa kuifadhili M23, madai ambayo Rais Paul Kagame aliyakanusha kupitia mahojiano aliyofanya na CNN huku akisema hafahamu iwapo kuna wanajeshi wa RDF wanaopigana upande wa waasi nchini DRC.

Pamoja na kutangaza kusitisha mapigano, M23 ilishtukiza wiki iliyopita na kuuteka Mji wa Nyabibwe uliopo Jimbo la Kivu Kusini nchini humo, huku taarifa zikidai kuwa wanaendelea kujitanua kuelekea Mji wa Mkuu wa Kivu Kusini wa Bukavu.

Tayari FARDC imethibitisha kuwakamata wanajeshi wake 75 wakiishtakiwa kwa kuwakimbia waasi wakati wanaukamata Mji wa Nyabibwe na Goma. Wanatuhumiwa kwa ubakaji, mauaji, uporaji na kufanya mapinduzi dhidi ya Serikali.

Ofisi hiyo pia imesema huenda namba ikaongezeka kwa kile ambacho imedai ukamataji bado unaendelea. Taasisi ya Kibinadamu mjini Kavumu ulioko takriban kilometa 35 kutoka Bukavu iliripoti kuwa wanajeshi hao waliwaua watu 10 wakiwemo saba waliokuwa wamekaa baa.

“Vitendo vya uhalifu ikiwemo uporaji vimekuwa vikitekelezwa na wanajeshi wa FARDC wakiwemo wanaokimbia mapigano dhidi ya waasi na bado yanaendelea,” alisema Leonidas Tabaro ambaye ni kiongozi wa Taasisi ya kibinadamu iliyopo Bukavu nchini humo.

Endapo wakikutwa na hatia kwenye Mahakama ya Kijeshi nchini humo, wanajeshi hao huenda wakakutana na rungu la adhabu ya kifo ama kifungo cha maisha jela.

Msemaji wa Jimbo la Kivu Kaskazini nchini humo, Nestor Mavudisa alisema wanajeshi hao wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria za kijeshi huku akiutaka Umma kuwa watulivu.

Wikiendi iliyopita, mapigano kati ya vikosi vya Serikali dhidi ya waasi hao yanaonekana kupoa japo kuliripotiwa mirushiano ya risasi katika Hifadhi ya Taifa iliyopo takriban kilometa 30 kutoka Mji wa Bukavu, jambo linalohisiwa kuwa huenda waasi hao wameukaribia mji huo.

Kundi la M23, linalotajwa kuwa na silaha za kisasa na zenye uwezo mkubwa linadaiwa kuundwa na idadi kubwa ya jamii ya Kitutsi, lenye makazi yake Mashariki mwa DRC. Hata hivyo, Serikali ya Rais Felix Tshisekedi wa DRC imekomalia madai kuwa waasi hao wanafadhiriwa na Serikali ya hasimu wake, Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts