Wananchi Manyara kulipia maji kabla ya matumizi

Babati. Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) mkoani Manyara imeanza kusambaza mita za maji za malipo kabla ya matumizi ili kuiwezesha jamii kunufaika na huduma hiyo na kuondokana na mrundikano wa madeni.

Akizungumza leo Februari 10, 2025 kwenye ziara ya ukaguzi wa majaribio ya mita hizo mkoani Manyara, mwenyekiti wa kamati ya fedha na utawala ya bodi ya wakurugenzi Ruwasa, Aloys Mvuma amesema bodi ya maji itahakikisha kuwa mradi huo unakuwa endelevu na msaada zaidi kwa jamii.

“Ili kufikia matamanio ya utoaji huduma ya maji kama ilipangwa, tumefanikisha hudumu hii kwa kusambaza mita za maji za malipo kabla ya matumizi kwa kufanya majaribio na kuonekana ina tija,” amesema Mvuma.

Amesema Ruwasa imebuni mbinu hiyo ikiwa na lengo endelevu la kutoa huduma ya maji kwa wananchi huku ikibainishwa kuwa majaribio ya mita iliyofungwa katika Kijiji cha Gidas inawanufaisha wananchi 4,972 ambapo wananchi wanatumia mfumo wa kadi kupata huduma hiyo.

Wananchi wa eneo hilo walionufaika na mradi huo wamesema mita hizo zimekuwa na msaada kwa jamii na kuongeza mapato kwa idara husika kwani mtu analipia huduma ya maji kabla ya kuyatumia na linaondoa ukakasi na mrundikano wa madeni ikilinganishwa na mita za awali.

Mmoja kati ya wanufaika wa huduma hiyo, Venance Ombay ameipongeza Ruwasa kwa kuja na ubunifu huo kwani una tija na thamani ya fedha zao inaonekana kabla ya matumizi.

“Niwapongeze Ruwasa kwa ubunifu huu, sisi wananchi ambao tumeanza kutumia huduma hiyo tunaiona ni nzuri na yenye thamani kubwa kwetu kwani haina konakona wala longolongo katika kupatiwa huduma ya maji,” amesema Ombay.

Akitoa taarifa ya hali ya huduma ya maji katika Mkoa wa Manyara, Meneja wa Ruwasa wa mkoa huo, James Kionaumela amesema upatikanaji wa maji Manyara ni asilimia 75.5.

Kionaumela ameongeza kwamba Wilaya ya Babati inaongoza kwa upatikanaji wa maji kwa asilimia 80.9 na Wilaya ya Kiteto ikiwa nyuma kwa asilimia 64.

Amelezea changamoto kubwa zinazoukabili mkoa wa Manyara ni pamoja na ukosefu wa usafiri katika wilaya za Simanjiro na Hanang’, jambo linalosababisha utendaji kazi kutofanyika Kwa wakati.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Mariam Muhaji amesema mkoa huo bado unahitaji huduma ya maji hasa kwa wananchi wanaoishi vijijini.

Muhaji amesisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na Ruwasa katika kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na huduma ya maji.

Akihitimisha ziara yake aliyoambatana na wajumbe wa bodi ya Ruwasa, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Bodi ya Wakurugenzi Ruwasa, Aloys Mvuma amesema amepokea changamoto zote zinazoikabili Ruwasa Mkoa wa Manyara na kuahidi kuwa atamshauri mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ili alipatie ufumbuzi wa haraka.

Related Posts