Dar es Salaam. Mshtakiwa Felista Mwanri (70) na wenzake, wanaokabiliwa na mashtaka ya kusafirisha tani moja ya dawa za kulevya aina ya bangi, wamehoji sababu za upelelezi wa kesi yao kuchukua muda mrefu kukamilika.
Washtakiwa hao wafikia hatua hiyo, muda mfupi baada ua upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Wakili wa washtakiwa hao, Fabian Mruge ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Februari 10, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili kutajwa.
” Mheshimiwa hakimu, washtakiwa hawa wamefikishwa miezi mitano wakiwa rumande huku upelelezi wake ukiwa bado haujakamilika” alidai Mruge na kuongeza.
” Naomba upande wa mashtaka wafanye jitihada za makusudi ili upelelezi wa kesi hii ukamilike kwa sababu hawa ni watuhumiwa na sio wafungwa” alidai wakili Mruge.
Akijibu hoja hiyo, wakili wa Serikali Eva Kassa, alidai kuwa wamsikia maombi yao na watauafikisha kwa mamlaka husika ili upelelezi wa kesi hiyo uweze kukamilika kwa haraka.
Wakili Kassa ametoa majibu hayo, mbele ya hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini.
Kutokana na upelelezi kutokukamilika, Kassa amedai mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mhini amekubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 24, 2025 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wapo rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana.
Mbali na Mwanri ambaye ni mkazi wa Luguruni, washtakiwa wengine ni mtoto wa Felista aitwaye Richard Mwanri (47), Athuman Mohamed maarufu kwa jina la Makame (58) mkazi wa Tanga, Juma Chappa (36) mkazi wa Kiwalani na Omary Mohamed (32) ambaye ni dereva na Mkazi wa Buza, Dar es Salaam.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 28, 2024 eneo la Tairo Luguruni barabara ya Kwembe ndani ya Wilaya ya Ubungo.
Siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja walikutwa walisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 1,815, kinyume cha sheria.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao wamefishwa Mahakama hapo, Septemba 10, 2024 na kusomewa shtaka lao ambalo halina dhamana kwa mujibu wa sheria.