Wazazi Waishtaki TikTok Haina Huruma – Global Publishers

(Kutoka kushoto kwenda kulia: Wazazi Hollie Dance, Lisa Kenevan, Liam Walsh na Ellen Roome)

 

Familia nne kutoka Uingereza zinazoushtaki mtandao wa kijamii wa TikTok kwa madai ya kusababisha vifo visivyo vya haki vya watoto wao zimeituhumu kampuni hiyo ya teknolojia kwa kukosa huruma.

Katika mahojiano ya kipekee kwa kipindi cha Sunday with Laura Kuenssberg cha BBC One, wazazi hao walisema wanachukua hatua za kisheria dhidi ya kampuni hiyo ili kupata ukweli kuhusu kile kilichowakuta watoto wao na kuwawajibisha wahusika.

Wazazi wanaamini kuwa watoto wao walifariki dunia baada ya kushiriki katika mchezo waliouona TikToki uliosambaa kwenye jukwaa hilo la video mnamo mwaka 2022.

TikTok imesisitiza kuwa inakataza kuweka maudhui na michezo hatari. Kampuni hiyo pia imezuia utafutaji wa video na alama za reli (hashtags) zinazohusiana na mchezo huo ambao wazazi wanadai ulisababisha vifo vya watoto wao.

Kesi ya wazazi hao ilifunguliwa rasmi nchini Marekani siku ya Alhamisi, Februari 6, ikidai kuwa Isaac Kenevan (13), Archie Battersbee (12), Julian “Jools” Sweeney (14), na Maia Walsh (13) walifariki dunia wakati wakijaribu kuufanya mchezo huo uliojulikana kama “blackout challenge”, mchezo waliouona kupitia TikTok.

Madai hayo yaliwasilishwa katika Mahakama Kuu ya Jimbo la Delaware na Social Media Victims Law Center, shirika la Marekani linalowawakilisha waathiriwa wa mitandao ya kijamii, kwa niaba ya mama yake Archie, Hollie Dance; mama yake Isaac, Lisa Kenevan; mama yake Jools, Ellen Roome; na baba yake Maia, Liam Walsh.

Katika mahojiano maalum na BBC, Bi. Kenevan aliituhumu TikTok kwa kuvunja “kanuni zake yenyewe.” Katika kesi hiyo, familia hizo zinadai kuwa jukwaa hilo lilivunja sheria kwa njia kadhaa, ikiwemo kuruhusu au kuendeleza maudhui hatari yanayoweza kusababisha madhara makubwa ya kimwili.
Bado haijafahamika ni kiasi gani cha fidia wanachodai.

Related Posts