Februari 10, 2025, inaweza kuwa siku mbaya katika historia ya kisiasa kwa mwanazuoni Dk Godfrey Malisa baada ya kufukuzwa uanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Hata hivyo, ninachokiona ni kwamba kada huyo hakuwa amesoma alama za nyakati.
Nasema hakusoma alama za nyakati kwa kuwa kilichomfukuzisha uanachama hakitofautiani sana na kilichomfukuzisha Bernard Membe (sasa marehemu), nacho ni kugombea urais kupitia CCM, akitaka kumpinga John Pombe Magufuli mwaka 2020.
Tofauti ni kwamba Membe alitangaza hadharani kuwa atachukua fomu kushindana na Magufuli ndani ya CCM, wakati huo Magufuli alikuwa anaelekea kugombea muhula wa pili na wa mwisho katika uchaguzi mkuu wa 2020.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 na marekebisho yake, nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho iko wazi kwa mwanachama yeyote. Hata hivyo, utamaduni wa chama umekuwa ni kumwachia rais aliyeko madarakani kukamilisha mihula yake miwili.
Membe, ambaye alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na ni mmoja wa makachero wabobezi, alitaka kwenda kinyume na utamaduni huo kwa kuchukua fomu ya kuwania urais dhidi ya Rais Magufuli.
Februari 28, 2020, Kamati Kuu ya CCM ilitangaza kumfukuza Membe kwa kile kilichoelezwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa wakati huo, Humphrey Polepole, kuwa ni mwenendo mbaya wa maadili tangu mwaka 2014.
Hata hivyo, Membe alipohojiwa baada ya uamuzi huo alisema: “Tatizo ni urais. Wasipindishe pindishe. Mara ooh maadili sijui fanya nini. Shida kubwa ni urais.” Alisisitiza kuwa hata alipoitwa mbele ya Kamati ya Maadili aliwaambia atagombea.
Safari hii, Dk Malisa hakuwa ametangaza nia ya kuchukua fomu, bali alipinga uamuzi wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliompitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwania muhula wa pili.
Katika mkutano huo uliofanyika Januari 19, 2025, jijini Dodoma, ilitolewa hoja kwamba kwa kuwa Mkutano Mkuu ndicho chombo cha juu ndani ya CCM, wajumbe waridhie kumpitisha mgombea wa urais wa chama kwa uchaguzi wa 2025.
Wajumbe wa mkutano huo walimpitisha Rais Samia kwa asilimia 100 ya kura, baada ya wajumbe 1,924 kumpigia kura za ndiyo. Vilevile, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alipitishwa kuwania muhula wa pili na Balozi Emmanuel Nchimbi akachaguliwa kuwa mgombea mwenza.
Baada ya maamuzi hayo, Mchungaji Malisa alijitokeza kupitia video mbalimbali akipinga kuwa mchakato huo ulikiuka Katiba ya CCM na Katiba ya Tanzania. Alidai kuwa wanachama wengi wa CCM walimwelewa na walikubaliana naye kuwa chama kipitie upya jinsi utaratibu ulivyotumika kuwapitisha Samia, Mwinyi, na Nchimbi.
Katika hoja zake, alidai kwamba wanachama wa CCM walinyimwa haki ya kugombea nafasi ya urais na kwamba wapo wenye hasira na maamuzi hayo, ambazo wataonyesha katika uchaguzi mkuu wa 2025.
Kulingana na Katiba ya CCM, Ibara ya 100(5) inaeleza kuwa kazi mojawapo ya Mkutano Mkuu ni kuchagua jina moja la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pengine Mchungaji Malisa hakutambua kuwa utaratibu wa kutoa fomu, wanachama kuomba, na mchujo kuanzia Kamati Kuu, Halmashauri Kuu hadi Mkutano Mkuu, ulifuatwa. Pengine hapa ndipo anapodai Katiba ilivunjwa.
Lakini huenda hakusoma Ibara ya 99(2), inayoeleza kuwa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ndicho kikao kikuu chenye madaraka ya mwisho. Sasa, ikiwa wajumbe 1,924 wameafiki, yeye ni nani wa kupinga?
Tuseme CCM ingefuata utaratibu wa kutoa fomu kwa wanachama kujitokeza, lakini Malisa alisahau kuwa CCM ina utamaduni wake wa kumwachia rais aliyeko madarakani kuhudumu kwa mihula miwili.
Ni kweli Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inasema kila raia ana haki ya kupiga kura na kuchaguliwa, lakini Mchungaji Malisa akumbuke kuwa lazima udhaminiwe na chama cha siasa. Wenye chama chao wamesema Samia, unashindaje hapo?
Nimkumbushe Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Roosevelt, aliyesema: “In politics, nothing happens by accident. If it happens, you can bet it was planned that way.” Katika siasa, hakuna kinachotokea kwa bahati mbaya; ikiwa kimetokea, basi kilipangwa hivyo.
Hili lililotokea Dodoma kwa jina la Rais Samia, Dk Mwinyi, na Balozi Nchimbi kupitishwa kuwa wagombea wa CCM halikutokea kwa bahati mbaya. Wapo waliolipanga litokee hivyo katika mkutano huo.
Kwa wachambuzi wa siasa, hatua hiyo ilichukuliwa ili kuzima vuguvugu la makada wa CCM waliotaka Rais Samia asipitishwe moja kwa moja bali apitie mchakato wa kura za maoni.
Kundi hilo ndilo lililokuwa likidai kuwa hii siyo Serikali ya awamu ya sita bali ni ya tano inayomaliza muda wake, hivyo Samia alipaswa kushindanishwa na wengine. Lakini hadharani, wanaufyata mkia na hawajitokezi.
Ukimsikiliza Mchungaji Malisa, anadai kuwa wanachama wengi hawakuridhishwa na mchakato huo na wanataka urejelewe. Hata hivyo, nataka nimwambie kuwa atajikuta amebaki peke yake, kwani hao ‘wanachama wengi’ hatimaye hawataonekana.
Wenye CCM yao walishafanya maamuzi. Ndugu yangu Malisa, hata ungelalamika wapi, CCM ina wenyewe, na wenyewe ni hao walioamua. Ndio maana nilianza kwa kusema hukusoma alama za nyakati, alama zilizoanzia kwa kada mwenzako, Bernard Membe.
Waswahili wana msemo: “Unapokula na kipofu, kamwe usimshike mkono.” Ndugu yangu Malisa alipojiunga na CCM baada ya kupitia Tanzania Labour Party (TLP) na Chama cha Kijamii (CCK), hakujua kuwa CCM ina utamaduni ulio juu ya Katiba yake.
Utamaduni wa kumwachia Rais wa CCM kumaliza mihula miwili haupo katika Katiba ya CCM, bali ni desturi ya muda mrefu.
Kaka yangu Malisa alipaswa kusoma alama za nyakati. Hata Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema CCM itatoa fomu moja tu kwa nafasi ya urais, na fomu hiyo ni ya Rais Samia. Kwa hiyo, kilichotokea ndicho kingetokea tu.