Aliyewazuia Dube, Mzize afichua siri, amtaja Chama

YALE makali ya washambuliaji wa Yanga, Clement Mzize na Prince Dube waliyoyaonyesha mechi saba zilizopita katika Ligi Kuu Bara, kipindi cha Kocha Sead Ramovic, yamezimwa leo Jumatatu na JKT Tanzania.

Waliofanya kazi kubwa ya kuzima ubora huo ni mabeki wa JKT wakiongozwa na nahodha Edson Katanga na Wilson Nangu waliocheza pacha beki wa kati katika mchezo  uliozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar na kumalizika kwa matokeo ya 0-0.

Katanga na Nangu walifanya kazi kubwa kuwazuia Dube na Mzize ambao mechi saba zilizopita chini ya Ramovic walifunga jumla ya mabao 14 kati ya 28, kila mmoja akifunga saba.

Katika moja ya tukio la kumzuia Dube ambaye ni mchezaji pekee mwenye hat trick hadi sasa katika ligi msimu huu, jezi yake ilichanika na kulazimika kuibadilisha mapema tu dakika ya nane.

Sasa basi, Nangu aliyetangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, amefichua siri ya kufanikiwa kuwazuia washambuliaji hao na Yanga kwa ujumla ambayo hii ni mara ya pili inatoka uwanjani bila kufunga bao kwenye ligi msimu huu baada ya kufanya hivyo walipofungwa 1-0 na Azam, Novemba 2, 2024.

“Tulipokuwa mazoezini, tulikuwa tunakumbushana mmoja anapoenda kukaba wengine tuzibe nafasi, nadhani ndio kitu kilichotusaidia sana leo kutoruhusu bao kwani tunafahamu Yanga ina wachezaji ambao ukiwapa nafasi tu wanakuliza.

“Lakini pia kocha huwa anatuambia tunapocheza nyumbani tupambane kuhakikisha hatupotezi mechi, tukishindwa kupata alama tatu basi tuondoke na moja ndio maana hadi sasa msimu huu hatujapoteza nyumbani na imekuwa ngumu wapinzani kufunga bao kwetu,” amesema beki huyo aliyewahi kuichezea TMA ya Arusha inayoshiriki Championship.

Rekodi zinaonyesha JKT TZ katika mechi nane za nyumbani msimu huu imeshinda tatu na sare nne, haijapoteza, imefunga mabao saba na kuruhusu matatu, ina clean sheet sita.

Wakati nyumbani ikiwa hivyo, ugenini imecheza mechi 11, imeshinda moja, sare nne na kupoteza sita. Imefunga mabao manne na kuruhusu 11.

Nangu amesema mbali na kuwazuia washambuliaji hao, pia ilikuwa rahisi kumzuia Clatous Chama asitengeneze nafasi kwa wenzake au kufunga kutokana na kuufahamu uchezaji wa nyota huyo Mzambia.

“Sisi mabeki huwa na kawaida ya kuwasoma wachezaji hatari, ukiangalia dakika 45 za kwanza Chama hakuwa na madhara kwa sababu nilimsoma muda mrefu.

“Kwanza Chama ni mchezaji ninayempenda, hivyo huwa namuangalia uchezaji wake.

“Anapokuwa na mpira lazima apunguze kwanza mtu ndio apige kitu ambacho tulikijua mapema ndio maana tulimdhibiti hadi akatolewa,” amesema Nangu aliyebainisha tuzo ya mchezaji bora aliyoipata ni maalum kwa mama yake mzazi.

Katika mchezo huo, Chama mwenye asisti mbili katika ligi msimu huu, alifanya shambulizi moja la hatari karibu la lango la JKT Tanzania ambalo mabeki walikuwa imara kulizuia huku mara tano alizojaribu kuingia na mpira kwenye boksi aliishia kupoteza kabla ya kutolewa   zilipomalizika dakika 45 za kwanza, nafasi yake akaingia Stephane Aziz Ki ambaye hakuwa na madhara.

Related Posts